Serikali yatenga bilioni 62 kuweka umeme vijiji 384

20Jun 2021
Na Mwandishi Wetu
Mtwara
Nipashe Jumapili
Serikali yatenga bilioni 62 kuweka umeme vijiji 384

SERIKALI imetenga shilingi bilioni 62.146 kwa ajili ya kupeleka umeme katika vijiji 384 vilivyokuwa vimesalia kuunganishiwa umeme katika Mkoa wa Mtwara kwa ndani ya miezi 18.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, wakati wa uzinduzi wa mradi kabambe wa kusambaza umeme vijijini kwa awamu ya tatu mzunguko wa pili mkoani humo, uliofanyika katika kijiji cha Namtumuka.

Amesema, kati ya vijiji 797 vilivyopo mkoani Mtwara, vijiji 413 tayari vimepatiwa umeme na vijiji vilivyosalia 384 vitapatiwa umeme katika Mradi huu ndani ya miezi 18 na hivyo kuweka historia ya mafanikio katika kutekeleza miradi ya kusambaza umeme vijijini.

Kalemani amesema itakapofika Desemba 2022, Tanzania itaandika historia katika vitabu vyake kuwa vijiji vyote vya Tanzania Bara vimepata umeme na kuungana na mataifa mengine duniani yaliyoendelea ambayo yameshaandika historia hii.

Hata hivyo amesema, hadi sasa, zaidi ya vijiji 10,312 vimeshapelekewa umeme na vilivyobakia takribani vijiji 1,956 ndivyo vinapelekewa umeme katika mradi huu.

Habari Kubwa