Serikali yatenga trilioni 2 kusaidia kaya masikini

05Dec 2019
Cynthia Mwilolezi
ARUSHA
Nipashe
Serikali yatenga trilioni 2 kusaidia kaya masikini

SERIKALI imetenga Sh.Trioni 2  kwa ajili ya kusaidia  Kaya maskini zilizopo katika halmashauri zote nchini, kupitia Mpango wa Kunusuru kaya maskini (TASAF) utakaoanza utekelezaji wake  awamu ya tatu kipindi cha pili   Januari mwakani 2020.

Akizungumza jana katika Kijiji cha Khusumay kilichopo wilayani Karatu, wakati wa ziara ya Kamati ya Uongozi wa Tasaf Taifa, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu Dk.Moses Kusiluka alisema  fedha hizo zitatumika awamu hiyo baada ya Tasaf awamu ya tatu  kipindi cha kwanza kuisha muda wake mwaka huu.

Alisema lengo la serikali kutoa fedha hizo ili kusaidia wananchi waondokane na umaskini kwa kujikwamua kiuchumi katika kubuni miradi mbalimbali.

Katibu  Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu Dk.Moses Kusiluka (Mwenye suti ndani shati jeupe) akipiga picha na mmoja wa mnufaika (Bibi mwenye kilemba) wa mpango wa kunusuru kaya maskini (Tasaf)   katika kijiji cha Khusumay wilayani Karatu baada ya kutembelea kaya hizo leo.

“Kimsingi mpango huu umefanikiwa kwa sababu changamoto ni chache ukilinganisha na mafanikio yaliopatikana na kila tunapotembelea kuongea na walengwa tunaona wamepiga hatua na wanafurahi mpango huu na hili ndio lengo la serikali,”alisema.

Dk.Kisiluka alisema  katika awamu ijayo serikali itahakikisha walengwa wote waliobainika kuwa kaya maskini lakini hawakuwekwa katika mpango huo wanawekwa awamu ijayo.

Mmoja wa wanufaika wa mradi wa Tasac Sophia Saragu (mwenye sweta la bluu) akiwa na watoto wake  katika nyumba anayoishi kijijini Khusumay wilayani Karatu.

Alitaja changamoto chache zilizojitokeza ikiwa na pamoja na baadhi ya maeneo kulegalega kwa wasimamizi wa mpango na kusababisha uwepo wa watu wasiostahili kuingizwa, japo viongozi waligundua kupitia uhakiki na kuwaondoa.

“Lakini awamu ijayo hatutakuwa na changamoto hii sababu tumeboresha mfumo na taarifa zote zipo kwa njia ya teknolojia ya mtandao na tukibaini msimamizi yoyote amekiuka na kwenda kinyume na sheria na taratibu za mpango tunamchukulia hatua stahili,”alisema.

Nyumba ya walimu iliyojengwa na Tasaf Shule ya Sekondari ya Baray katika kijiji cha Khusumay wilayani Karatu.

Aidha alisema moja ya mafanikio waliyopata ni  wananchi wengi waliosaidiwa katika mpango huo siku za nyuma wameboresha maisha kupitia kilimo cha mahindi,mtama,alizeti,ngwala na mazao mengine,pamoja na ufugaji wa Kuku,Mbuzi, Ng’ombe na Nguruwe.

Hata hivyo alisema sambamba na maboresho mbalimbali wanayofanya ili kumaliza changamoto zilizojitokeza, pia watafanya mabadiliko ya watumishi hasa wale waliofanya vibaya katika kipindi cha kilichopita na kuingiza wapya.

Dk.Moses Kusiluka (mwenye suti na miwani katikati ya wanafunzi) akikabidhi mbuzi wanafunzi wa shule ya Baray iliyopo kijijini Khusumay baada ya kukabidhiwa yeye (Dk.Kusiluka) na wanufaika wa Tasaf kijijini hapo kama zawadi ya kumahukuru kwa kuwakomboa kiuchumi.

Aliwaasa watu wote waliopata fedha na watakaopata kutumia vema fedha hizo kufanya kazi kwa  nguvu zao zote ili wapige hatua kama lengo la serikali lilivyo.

Mkurugenzi wa Tasaf Taifa, Ladislaus Mwamanga alisema Tasaf awamu ya tatu kipindi cha kwanza walikuwa katika halmashauri 44 nchini, lakini baada ya kuona wahitaji wapo kila eneo nchi nzima kipindi cha pili cha utekelezaji wa mpango huo watatekeleza halmashauri zote 185 nchini ili  kaya zote zinazostahili zinufaike.