Serikali yatishia kuvunja halmashauri jiji la Tanga

29Feb 2016
Lulu George
Nipashe
Serikali yatishia kuvunja halmashauri jiji la Tanga

SERIKALI imetishia kuivunja Halmashauri ya Jiji la Tanga iwapo hawatamaliza migogoro ya kisiasa iliyoababisha Baraza la Madiwani kushindwa kufanya vikao mbalimbali.

MAKAMU WA RAIS Samia Suluhu Hassan

Hatua hiyo imeelezwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alipokuwa akizungumza na viongozi wa serikali, siasa na watendaji wa mkoa wa Tanga, katika ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani hapa.

“Mpaka sasa Tanga Jiji hakuna uongozi uliosimama. Sasa hatuwezi kwenda kwa mwendo huu, wananchi wanahitaji maendeleo na kurudia uchaguzi hatuwezi. Kilichobaki ni kuivunja halmashauri mpaka hapo muda wa kufanya uchaguzi kwa mujibu wa Katiba ya nchi utakapotimia,” alisema.

Tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais, Oktoba, mwaka jana, na uchaguzi wa Meya Desemba, mwaka huo, Baraza la Madiwani wa Jiji la Tanga halijakutana kutokana na kuzuka kwa vurugu za uchaguzi wa meya, baada ya msimamizi wa uchaguzi kumtangaza Mustaph Mhina (CCM) kuwa mshindi wa nafasi hiyo badala ya Rashid Jumbe wa CUF.

Kwa mara ya kwanza tangu kupata uhuru, Jimbo la Tanga limekwenda kwa upinzani, hatua ambayo iliwashangaza wakongwe wengi wa siasa.

Kutokana na mgogoro huo, Samia alisema mkoa huo una mipango mbalimbali ya maendeleo lakini haiwezi kutekelezwa, hivyo kuwataka viongozi wa mkoa kutafuta namna ya kumaliza changamoto hizo kwa haraka.

“Jiji ni kioo cha mkoa mzima. Sasa kama wazee hawatakaa kitako na viongozi kutafuta suluhu, basi hii mipango yenu yote ya kufufua viwanda itakuwa ndoto tu kwa sababu hapa mjini hakuko shwari na tunalitambua hilo,” alisema.

Samia alielezea kusikitishwa kwake na biashara ya magendo iliyokithiri mkoani hapa hivyo kuiagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kuhakikisha inatumia kila mbinu ya kudhibiti ili kuimarisha mkoa kiuchumi.

Kuhusu na chakula, Samia alisisitiza kuwa serikali haitamvumilia mkuu yeyote wa mkoa wala wilaya, ambaye atatoa malalamiko ya kukosekana kwa chakula kwenye eneo lake kwak uwa kwa kufanya hivyo atakuwa amejifukuzisha kazi.

“Kiongozi ambaye atalalamikia kukosekana kwa madawati au chakula kwenye eneo lake ajue hicho ni kipimo cha awali kwamba ameshindwa kazi.

Badala ya kutulalamikia ajiondoe kazini, hilo kwetu halina mjadala na nilikuwa nasubiri tu mseme hamna madawati. Natumaini kwenu yapo lakini kama mmenidanganya msije kunilalamikia,” alisema.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mwantumu Mahiza, alisema hali ya chakula kufikia mwezi huu, haikuwa ya kuridhisha kutokana na kuchelewa kunyesha kwa mvua msimu wa mwaka 2014/2015 na hata ziliponyesha hazikuwa na mtawanyiko mzuri.

Mahiza alisema hali hiyo imesababisha upungufu wa chakula unaokadiriwa kufikia tani 125,418 katika baadhi ya maeneo ya wilaya za Tanga, Lushoto, Mkinga, Kilindi, Korogwe na Handeni.

Habari Kubwa