Serikali yatoa kibali ajira zingine maelfu

13May 2022
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Serikali yatoa kibali ajira zingine maelfu

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama, amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia kibali cha ajira kwa kada nyingine ikiwamo watendaji wa vijiji na kata.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama.

Mhagama aliyasema hayo bungeni jana alipokuwa akiongezea majibu katika swali la nyongeza la Mbunge wa Mbulu Mjini (CCM), Zacharia Issaay.

Mbunge huyo alisema kada ya watendaji wa kijiji na mitaa hazijapata kibali ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu ina upungufu wa watumishi hao kwa kipindi cha miaka mitatu sasa kwa zaidi ya asilimia 70.

“Serikali ina mkakati gani wa kuajiri watumishi hawa kwa Halmashuari ya Mbulu?" Alihoji.

Waziri Mhagama alisema Rais alitoa kibali cha ajira 32,604 za mwaka wa fedha 2021/22 na tayari ajira za kipaumbele kwa kada ya afya na elimu na nyingine ambatanishi zimetolewa.

Hata hivyo, alisema kada nyingine za ajira ikiwamo watendaji wa vijiji na kata zitafanyiwa mgawo kwenye ajira 7,792 ambazo zinasimamiwa na ofisi hiyo.

"Mheshimiwa Rais kupitia ofisi yetu ameridhia kada nyingine zilizobakia za watumishi ikiwamo watendaji wa vijiji na kata zifanyiwe mgawo kwenye ajira 7,792 ambazo bado zinasimamiwa na Ofisi ya Rais Utumishi,” alisema.

Awali, akijibu swali hilo, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk. Festo Dugange, alisema kwa sasa serikali imeshatangaza ajira kwenye kada ya elimu na afya za kipaumbele.

Hata hivyo, alisema ajira zingine zitaendelea kutangazwa kwa awamu ili kuhakikisha watumishi wa kada hizo wanaajiriwa na halmashauri zimeendelea kuajiri watendaji hao kwa kutumia mapato ya ndani.

Katika swali lake la msingi, mbunge huyo alihoji lini serikali itaajiri watumishi 40,000 katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kama ilivyopitishwa kwenye Mpango na Bajeti wa mwaka 2021/22.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Dugange alisema katika mwaka wa fedha 2021/22 tayari serikali imekwishatoa Ikama na kibali cha ajira kwa halmashauri zote nchini.

Alisema nafasi za ajira za watumishi 17,412 wa kada ya afya na elimu zimetangazwa na taratibu za kuajiri watumishi hao zinaendelea kukamilishwa.

Alisema ajira za kada zingine zinaendelea kutolewa kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma na halmashauri husika.

Habari Kubwa