Serikali yatoa maagizo mazito

26Apr 2019
Na Waandishi Wetu
Nipashe
Serikali yatoa maagizo mazito

SERIKALI imeelekeza mamlaka zote na wananchi wote wa mikoa ya Lindi, Mtwara na mikoa ya jirani kuchukua hatua za tahadhari ikiwamo kuwahamasisha wananchi wanaoishi kando ya Bahari ya Hindi ili kujiepusha na baa linaloweza kutokea.

Baadhi ya wakazi wa Mtwara wamehamia katika Uwanja wa Ndege wa Mtwara na eneo la JWTZ, Kikosi cha Naliendelee, ikiwa ni sehemu ya kujihami dhidi ya Kimbunga Kenneth kiLIchotabiriwa kuukumba mkoa huo.

Vilevile, imeagiza shughuli zinazofanywa kando na ndani ya Bahari ya Hindi, hususan shughuli ndogo ndogo za uvuvi  na usafirishaji wa anga na majini, kusimama.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, alitangaza maagizo hayo alipotoa kauli ya serikali jana bungeni jijini Dodoma kuhusu Kimbunga cha Keneth.

Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) ilitangaza Jumatatu kuwa kimbunga hicho kilikuwa kilomita 450 kutoka pwani ya Mtwara na kilikuwa na kasi ya kilomita 130 kwa saa.

TMA ilieleza kuwa kimbunga hicho kilitarajiwa kuongeza nguvu zaidi jana mchana kikifikia kilomita 170 kwa saa na kingekuwa kilomita 150 kutoka pwani ya Mtwara.

Akitoa kauli ya serikali kuhusu kimbunga hicho, Waziri Mhagama alisema kufuatia utabiri huo, kuna uwezekano mkubwa kimbunga na mafuriko kutokea katika mikoa ya Mtwara na Lindi na mikoa mingine ya jirani.

“Kwa msingi huo, kunatarajiwa kutokea kimbunga chenye kasi ya kilomita 130 kwa saa katika uelekeo wa mashariki kwa umbali wa kilomita 175 kutoka pwani ya Mtwara, kimbunga hicho kinatarajiwa kuendelea kusogea kuelekea pwani ya kusini ya nchi yetu na kitaambatana na mafuriko kwa sababu mikoa ya Lindi na Mtwara ipo chini ya usawa wa bahari," alisema.

“Hali hiyo inatarajiwa kuleta athari mbalimbali ikiwa ni pamoja na mafuriko na upepo mkali vinavyoweza kupelekea athari na uharibifu wa makazi, mazao shambani, miundombinu kutokana na kuongezeka kwa kina cha maji katika Bahari ya Hindi.

"Shughuli za usafirishaji wa anga na majini zinaweza kuathirika hasa kwa mikoa ya Lindi na Mtwara kutokana na hali mbaya ya hewa inayotabiriwa.”

Alisema serikali imeelekeza mamlaka zote na wananchi wote wa mikoa ya Lindi, Mtwara na mikoa ya jirani kuchukua hatua za tahadhari ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha wananchi wanaoishi kando ya Bahari ya Hindi.

“Tunaendelea kusisitiza kamati za maafa katika ngazi zote katika maeneo husika kwa mujibu wa sheria tuliyonayo, kufuatilia kwa karibu na kwa kina jambo hili, naendelea kuelekeza uongozi wa ngazi zote kutoka katika mikoa ya Lindi na Mtwara kutoa tahadhari katika mitaa mbalimbali pamoja na hatua mbalimbali za kuchukuliwa," aliagiza.

Alisema serikali imetoa rai kwa taasisi mbalimbali za umma na taasisi binafsi kuendelea kufuatilia na kujiandaa kutoa misaada mbalimbali ya kibinadamu endapo hali hiyo itajitokeza.

Waziri Mhagama ambaye pia ni Mnadhimu wa Shughuli za Serikali Bungeni, alisema pamoja na kazi nzuri inayoendelea kufanyika kwa sasa, serikali inaendelea kuelekeza hatua stahiki zichukuliwe ili kupunguza madhara makubwa ya kimbunga na mafuriko kama yatatokea kama ilivyotabiriwa na TMA.

“Serikali kwa kuzingatia Sheria yetu ya Maafa Na. 7 ya Mwaka 2015 na kanuni za usimamizi wa maafa ya mwaka 2017, inaendelea kusisitiza kamati za maafa kupitia ngazi ya vijiji mpaka wilaya kuhakikisha tunakuwa pamoja na kushirikiana na wananchi katika kuhakikisha tunakabiliana," aliagiza.

Alisema Ofisi ya Waziri Mkuu na hasa idara ya maafa itaendelea kuchukua hatua stahiki kuhakikisha wananchi wanakuwa salama.

HALI ILIVYO KUSINI

Hamaki ilitanda miongoni mwa wananchi wengi wa mikoa ya Lindi na Mtwara kutokana na taarifa ya uwezekano wa kimbunga hicho kuyakumba maeneo yao.

Shughuli mbalimbali za kibinadamu pia ziliendelea kusimama huku serikali ikitangaza mapumziko kwa wafanyakazi na wanafunzi ili kutoruhusu athari kutokea dhidi yao.

Nipashe ilishuhudia jana wananchi wa Mkoa wa Mtwara wakilazimika kukusanyika maeneo maalum yaliyotengwa kwa tahadhari ambayo ni Uwanja wa Ndege Mtwara, Shule ya Sekondari Sabasaba na maeneo mengine ili kujiepusha na athari zinazoweza kusababishwa na kimbunga hicho.

Katika maeneo hayo wanawake na watoto wao, wazee walionekana wakiwa ni miongoni mwa wengi walioacha makazi yao na kwenda kujihifadhi sehemu salama.

Tangu asubuhi ya jana, hali ya hewa mkoani humo ilikuwa ikibadilikabadilika na mvua zikiendelea kunyesha huku Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi, akieleza kuwa kadri kimbunga hicho kinaposogea mvua, zitaongezeka zaidi.

Dk. Kijazi alisema kimbunga hicho kitadumu kwa siku mbili hadi Jumamosi na tofauti na vimbunga vingine, kitatua nchi kavu na kurudi baharini.

"Wakati mwingine kimbunga kinapotua nchi kavu kinapotea lakini hiki kitarudi baharini, kikirudi baharini tunaomba wananchi waendelee kufuatilia taarifa za TMA ili kujua kimerudi eneo gani na kama kitaleta athari ukanda wetu au la," alisema.

Dk. Kijazi alisema endapo kitadumu eneo la Msumbiji, ni dhahiri kuwa na Tanzania iendelee kuchukua tahadhari.

Alisema kimbunga hicho kitakuwa na upepo wa kilomita 140 baharini na zitafika kilomita 170 na kitakapotua nchi kavu kitakuwa kilomita 100 kwa saa.

“Kilomita 100 kwa saa ni kazi kubwa ya upepo ambayo inaweza kusababisha athari nyingi,” alisema.

Alisema kimbunga hicho ni cha kwanza chenye nguvu kinachoelekea Pwani ya Msumbiji na kuleta athari Tanzania.

Dk. Kijazi, akielezea kitaalam hali ilivyokuwa Mtwara kupitia picha ya satelaiti jana mchana, alisema kimbunga hicho kilikuwa kimekaribia kuelekea mpakani mwa Tanzania na Msumbiji.

Alisema wamefuatilia katika mifumo yote ya hali ya hewa na kuona kitaleta athari baadhi ya maeneo hasa ya kusini mwa nchi.

Dk. Kijazi alisema hadi majira ya saa tisa alasiri jana, kilikuwa kimefika latitudo 11.9 kusini na longitudo 40.2 mashariki.

Alisema eneo hilo lina umbali wa 177 kutoka maeneo ya Mtwara na kitaongezeka nguvu hadi kilometa 140 kwa saa.

“Utabiri unaonyesha hadi kufikia kesho (leo) alfajiri, kitatua maeneo ya Pwani ya Msumbuji takribani latitudo 12.3 kusini, longitudo 39.4 mashariki na hali hii ni sawa na kilometa 237 kutoka Pwani ya Mtwara,” alisema.

 “Ni muhimu kwa sasa wananchi waendelee kufuatilia taarifa hizi na kuchukua hatua kulingana na maelekezo, kwa sababu yapo maeneo ambayo yameelekezwa waende, mvua tangu asubuhi ya leo (jana) zimenyesha, wasione ni mvua ndogo kwa sababu kadri kimbunga kinavyokuja na mvua zitaongezeka zaidi."

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa, alitangaza mapumziko kwa wafanyakazi na wanafunzi huku watumishi wengine kwenye taasisi za afya, polisi na Shirika la Umeme (Tanesco) wakitakiwa kuendelea na utekelezaji wa majukumu yao.

MELI, BOTI

Wakati huo, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) limetoa tahadhari kwa wamiliki na manahodha wa vyombo vya usafiri wa majini, likiwataka kuegesha vyombo vyao ili kusalimisha maisha ya watumiaji na mali kwa ujumla.

Kaimu Mkurugenzi wa Tasac, Japhet Loisimaye, alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa ni vyema kuzingatia tahadhari iliyotolewa na TMA kuhusu kimbunga hicho.

“Nasi tumeamua kuweka msisitizo kwa kuwa mojawapo ya jukumu la Tasac ni kuhakikisha vyombo vyote vya majini vinakuwa salama,” alisema Loisimaye.

“Tunawasihi wananchi kuwa wavumilivu kwa siku hizi tatu, wasije kufikiri ikipita Aprili 26 (leo) inayohofiwa kuwa na madhara hayo zaidi kwamba hali itakuwa shwari, bali inabidi kuongeza siku mbili zaidi kujiridhisha ndipo waendelee na shughuli zao."

Kamishna wa Operesheni wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Billy Mwakataga, katika taarifa yake jana, alisema wamejipanga na wako imara kuhakikisha wanatoa huduma bora, sahihi na kwa wakati wote wa tukio la kimbunga hicho.

“Wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari katika kipindi hiki na kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri kutoka TMA na kusikiliza vyombo vya habari ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza,” alisema.

Pia alisema kutokana na kimbunga hicho kikali kinachoambatana na mvua kubwa, kuna uwezekano wa mawe makubwa au udongo kuporomoka milimani au miti kuanguka na kuziba barabara hivyo madereva watumiaji wengine wanapaswa kuchukua tahadhari.

*Imeandikwa na Hamis Nasri (Mtwara), Godfrey Mushi (DODOMA), Romana Mallya na Beatrice Mosses (DAR)

Habari Kubwa