Serikali yatoa miezi sita

23Mar 2017
Abdul Mitumba
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali yatoa miezi sita

SERIKALI imemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kusimamia na kuhakikisha mchakato wa kuundwa kwa Baraza la Taaluma ya Ustawi wa Jamii unakamilika katika kipindi cha miezi sita.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Dk. Khamis Kigwangalla.

Lengo la serikali ni kuona muswada huo unawasilishwa wakati wa Bunge la Septemba kwa ajili ya kutungwa sheria ya kulitambua rasmi baraza hilo.

Kwa sasa taaluma ya ustawi wa jamii haitambuliwi kisheria nchini, hivyo kutoa fursa kwa baadhi ya watu wasio waaminifu kwa jamii kwamba tabia yao ya huruma kwa wenye mahitaji maalum kuwa ni wana ustawi wa jamii.

Agizo hilo lilitolewa jana na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Dk. Khamis Kigwangalla wakati akizungumza na wadau wa ustawi wa jamii katika maadhimisho ya Siku ya Ustawi wa Jamii Duniani inayoadhimishwa kila Machi 21 kote duniani.

"Namuagiza katibu mkuu wa wizara yangu ambaye kwa bahati nzuri mwakilishi wake yupo hapa leo (jana) aende akaanze mchakato wa kuundwa kwa baraza la hilo ili bunge la Septemba mwaka huu, likapate nafasi ya kupitia muswada na kupitisha kuwa sheria," alisema Dk.Kigwangala.

Agizo hilo la serikali imetokana na ombi la wadau wa taaluma hiyo ambao wameomba kuharakishwa kwa upatikanaji wa baraza hilo ili kuipa heshima na hadhi taaluma ya ustawi wa jamii na kuzuia watu kuwatumia watu wenye shida kama mtaji wa kujipatia kipato.

Awali akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya Magava wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Profesa Lusian Msambichaka amesema chuo hizo kimeanza kutoa taaluma hiyo nchini mwaka 1973 licha ya kwamba kwingineko duniani taaluma hiyo ilianza kutolewa mwaka 1946.

“Kwa sasa kuna maofisa ustawi wa jamii zaidi ya 733, ambapo vyuo kumi vimeanza kuzalisha wataalamu hao ambapo lengo ni kuhakikisha matatizo ya unyanyasaji, utelekezaji wa watoto, unyanyasaji wa kijinsia, matumizi mabaya ya teknolojia ya mawasiliano ya habari na ndoa za utotoni zinakomeshwa kwa kuwatumia maofisa hao," alisema.

Mapema Mwenyekiti wa Chama cha Maofisa Ustawi wa Jamii Tanzania (TASWO), Dk.Zena Mabeyo, alisema maadhimisho hao yanafanyika katika taasisi ya ustawi wa jamii kwa mara ya tatu katika kipindi cha miaka minne, na kwamba mwaka jana yalifanyika jijini Arusha na kuhudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi za Uganda, Kenya, Burundi na Austria ambapo maazimio kadhaa yaliwekwa likiwamo la kuundwa kwa baraza la kitaaluma.

Mwakilishi wanataaluma waalikwa kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Tiba cha Hubert Kairuki, Dk. Theresia Kaijage, aliiomba serikali kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaosomea ustawi wa jamii ili kuharakisha kupatikana kwa maofisa wengi wasaidie wananchi wanyonge.

"Wenzetu wa Afrika Kusini wanafanya hivyo na wamefanikiwa. Walifanya hivyo muda mfupi baada ya kujikomboa kutoka mikononi mwa makaburu na sasa nchi inakwenda vizuri kwa sababu maofisa ustawi wa jamii ni wengi," alisema.

Maadhimisho ya mwaka huu ya siku ya ustawi wa jamii duniani ni kukuza na kuimarisha jamii na mazingira endelevu.

Habari Kubwa