Serikali yatoa msimamo mapenzi ya jinsia moja

28Jun 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali yatoa msimamo mapenzi ya jinsia moja

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju, amesema mapenzi ya jinsia moja hayakubaliki na serikali ilishaweka msimamo wake katika hilo.

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju

Mpanju alisema hayo jana katika mkutano wa wadau wa haki za binadamu uliofanyika jijini Dar es Salaam, kujadili mapendekezo ya tathmini ya utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu, na kuweka mikakati ya kuishawishi serikali kukubali mapendekezo mengine ambayo iliyakataa.

Mpanju ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo, alisema mapendekezo yaliyowasilishwa Mei, mwaka huu, katika mkutano wa Baraza la Haki za Binadamu uliofanyika Geneva, serikali ilikubali mapendekezo 130 na mengine 72 iliyakataa.

“Sehemu ya mapendekezo hayo serikali iliyakataa kwa sababu kuna mengine yako kinyume cha katiba, sheria, mila na desturi zetu, kwani katika mapendekezo hayo yapo yanayotaka mapenzi ya jinsia moja, jambo ambalo haliwezi kukubalika,” alisema.

Aliongeza kuwa: “Wakati mkijadili namna ya kupanga mikakati ya utekelezaji ili serikali ione umuhimu wa kukubali sehemu ya mapendekezo hayo, katika mkutano huu, naomba msijielekeze kwenye yale yaliyo kinyume cha Imani.”

Alisema serikali imefungua milango kwa kushirikiana na tume, hivyo wadau wa haki za binadamu wapeleke serikalini sababu zenye mantiki ili kuona ni mambo gani ambayo serikali inaweza kuyashugulikia na kuyatekeleza.

Naye Onesmo Olengurumwa kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), alisema wadau wamekutana katika mkutano huo kujadili ni kwa namna gani wataishawishi serikali ili kuyakubali mapendekezo yaliyobakia na kuyaweka katika utekelezaji.

Awali, Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Iddi Mapuri, alisema mkutano huo umelenga katika kuweka mikakati ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa mapendekezo hayo.

Mapuri alipongeza mchango mkubwa unaotolewa na wadau wa haki za binadamu katika kuhakikisha masuala ya haki za binadamu yanapata msukumo mkubwa nchini.

www.guardian.co.tz/circulation

Habari Kubwa