Serikali yatoa mwongozo utatuzi wa changamoto sekta ya elimu nchini

11Apr 2017
Asraji Mvungi
ARUSHA
Nipashe
Serikali yatoa mwongozo utatuzi wa changamoto sekta ya elimu nchini

SERIKALI imetoa mwongozo wa kitaifa utakaowezesha wadau wa elimu zikiwamo taasisi binafsi kuepuka kufanyakazi ambazo zimeshafanywa na serikali kuunganisha nguvu katika utatuzi wa changamoto zinazoikabili sekta hiyo.

waziri wa elimu, profesa joyce ndalichako.

Akizungumza mjini hapa jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania, Elia Kibga, alisema miongoni mwa mambo muhimu na yaliyopo kwenye mwongozo huo ni kubainisha maeneo yenye changamoto zinazohitaji msaada wa wadau walio tayari kusaidia na kuondoa tatizo la wadau hao kupoteza nguvu na muda kufanya mambo ambayo tayari yameshafanywa.

"Limekuwa ni jambo la kawaidia kuona tatizo moja ambalo lingeweza kutatuliwa na mdau ama taasisi moja linafanywa na wadau na taasisi nyingi, huku kukiwa na matatizo mengine mengi ambayo yangeweza kufanywa na wadau hao."

"Cha ajabu zaidi unakuta hata serikali nayo inalifanya jambo hilo hilo ama ilishalifanya na likakamilika, huku ni kupoteza nguvu na rasilimali, mwongozo huu utaondoa yote hayo kwani kwa sasa wadau wote watapewa maelekezo ya maeneo ya kusaidia ama yanayohitaji kufanyiwa kazi," alisema Kibga.

Baadhi ya wadau wa elimu wanaoshirikiana na serikali kutatua changamoto mbalimbali katika sekta ya elimu, walisema mpango huo ukitekelezwa kwa vitendo na kusimamiwa vizuri utaondoa matatizo mengi na kupata ufumbuzi na pia utaokoa matumizi mabaya ya misaada inayotolewa na wahisani.

Mmoja wa wahisani wa sekta ya elimu kutoka Marekani, David Avence, alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye bahati kubwa ya kuwa na wahisani na wadau wengi wenye uwezo wa kusaidia sekta mbalimbali ikiwamo ya elimu, ambao kukiwa na utaratibu mzuri wa kuwawezesha kutekeleza majukumu yao matatizo mengi yaliyopo yatapata ufumbuzi.

Habari Kubwa