Serikali yatoa sababu kuzibana NGO

15Dec 2018
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali yatoa sababu kuzibana NGO

SERIKALI imesema kuanzishwa kwa kanuni mpya za asasi za kiraia hakukuwa na nia mbaya na lengo ni kuimarisha uwazi na uwajibikaji.

atibu Mkuu wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, ambaye anashughulikia Maendeleo ya Jamii , Wazee na Watoto, Dk. John Jingu. picha na mtandao

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, ambaye anashughulikia Maendeleo ya Jamii , Wazee na Watoto, Dk. John Jingu.

Dk. Jingu alikuwa akizungumza wakati akifungua mkutano wa  baraza la asasi zisizo za kiserikali (NaCONgo) kwa ajili ya kujadili  masuala mbalimbali.

Alisema walianzisha kanuni hizo baada ya serikali kubaini kuwa baadhi ya asasi za kiraia zimekuwa zikitumia vibaya fedha za wafadhili kwa kujinufaisha na kwenda kinyume na makusudio ya wafadhili.

Jingu alisema wafadhili wana nia nzuri ya kuleta fedha kwa ajili ya maendeleo mbalimbali kama kujenga visima, zahanati na shule lakini asasi nyingi hawafanyi yale ambayo wafadhili wanayataka bali wanatumia fedha hizo kujinufaisha.
 
Alisema kanuni hizo zitasaidia kuziba mianya ya wizi na kuongeza uwajibikaji kwa asasi za kiraia.

 "Moja ya kanuni inasema asasi ziainishe vyanzo vya mapato na namna ya kutumia hizo fedha. hakuna tatizo katika hiyo kanuni kwa sababu Bunge lenyewe linaweka wazi matumizi na mapato ya serikali," alisema

 Naye Katibu wa Baraza, Ismail Suleiman alisema wameshakusanya maoni kuhusu sera mpya na wanaimani serikali itaingiza maoni yao katika hiyo sera.

Mwanzoni mwa wiki hii asasi zisizo za kiserikali zilitishia kuipeleka serikali mahakamani endapo haitaboresha kanuni mpya walizowekewa kwa kuwa  wamewekewa masharti magumu ambayo hayatekelezeki.