Serikali yatoa ufafanuzi ongezeko wenye mafua

19Dec 2021
Getrude Mbago
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Serikali yatoa ufafanuzi ongezeko wenye mafua

SERIKALI imekiri taarifa za kuwapo kwa ongezeko la watu wenye dalili za mafua, kukohoa, maumivu ya mwili na kuchoka, ikifafanua kuwa hiyo ni hali ya kawaida ambayo hutokea kila mwaka (seasonal influenza) na huchangiwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Aifello Sichalwe, Wizara ya Afya na taasisi zake wanaendelea kufuatilia kwa karibu viashiria vya mwenendo wa hali hiyo.

“Wizara inashauri wananchi wenye dalili hizi za kukohoa, mafua, maumivu ya mwili na kuchoka watoe taarifa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili wafanyiwe uchunguzi wa kitaalamu na wapatiwe matibabu stahiki,” alisema Dk Sichalwe katika taarifa yake hiyo.

Aliongeza kuwa pamoja na hali hiyo ya mwenendo wa mafua ya kawaida, wizara inaendelea kukumbusha na kutoa tahadhari kwa kila mtu kuendelea kuchukua hatua zote muhimu za kujikinga na janga la UVIKO-19.

Alishauri kuwa watu wanapaswa kuepuka misongamano isiyokuwa ya lazima, kunawa mikono, kuvaa barakoa na kuhakikisha kuwa kila mtu anapata dozi kamili ya chanjo.

Alisema wizara imeelekeza Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), vyuo vikuu na wataalamu wa afya kuendelea kutoa takwimu na elimu kutokana na utafiti wa kisayansi ambao wamekuwa wakifanya kuhusiana na visa vya mafua, ili kuhakikisha umma unaendelea kupata taarifa za mwenendo wa mafua nchini.

“Ninapenda kuwakumbusha wananchi kuwa ugonjwa wa UVIKO-19 bado upo na huenda maambukizi ya ugonjwa huu yakaongezeka hasa tunapoelekea mwisho wa mwaka unaohusisha kipindi cha msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.

“Hivyo, ni vyema tuzingatie kuchukua tahadhari zote kama zinavyoelimishwa na wataalamu wa afya bila kusahau kuchanja, pia tunatoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za tetesi za viashiria vya magonjwa ya mlipuko kutoka katika jamii kupitia namba ya simu 199 bila malipo,” alisema Dk. Sichalwe.

Jana mchana Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitangaza kuahirisha mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Kagera Sugar na Simba baada ya kupewa taarifa kwamba wachezaji wengi wa timu ngeni walikuwa na dalili hizo za mafua hayo ya msimu na kukohoa.

Habari Kubwa