Seth wa IPTL aachiwa huru

16Jun 2021
Kulwa Mzee
Dar es Salaam
Nipashe
Seth wa IPTL aachiwa huru

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemwachia huru Mkurugenzi wa Kampuni ya Kufua Umeme (IPTL), Herbinder Seth, kwa masharti ya kutotenda makosa tena na atakuwa chini ya uangalizi wa mwaka mmoja baada ya kukiri makosa yake na kukubali kulipa Sh. bilioni 26.9.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Kufua Umeme (IPTL), Herbinder Seth (katikati), akitoka kupitia mlango wa nyuma wa jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam leo, baada ya kuachiwa huru. PICHA: JUMANNE JUMA

Seth alitoka eneo la mahakama huku akiwa amezingilwa na ndugu na jamaa waliofika mahakamani hapo akiwamo ndugu yake waliofanana hali iliyowachanganya waandishi wa habari na wananchi wengine kubaini yeye ni yupi kati yao.

Seth alitokea mlango wa nyuma ya mahakama na gari lililombeba lilikuwa limeegeshwa maeneo ya mlango.

Hukumu ya mahakama ilitolewa leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, baada ya mshtakiwa huyo kufikia makubaliano na DPP ya kukiri makosa yake na kukubali kulipa fidia.

Alisomewa shtaka jipya la kujipatia Dola za Marekani 22,198,544.60 na fedha taslimu Sh. 309,461,300,158.27 kwa njia ya udanganyifu.

Baada ya kukiri kosa hilo mahakama ilimtia hatiani na kutoa nafasi kwa upande wa Jamhuri na utetezi kumzungumzia mshtakiwa kabla ya mahakama kutoa adhabu.

Wakili wa Serikali Mkuu, Martenus Marando, alidai mahakamani hapo kuwa hakuna kumbukumbu kwamba mshtakiwa ana makosa mengine aliyowahi kufanya.

"Tunaomba mshtakiwa alipe fedha alizokubali katika mkataba Sh. 26,946,487,420.80 ndani ya miezi 12 ambapo kati ya hizo jana Juni 16, alifanikiwa kulipa fidia ya Sh. milioni 200," alidai na kuomba apewe adhabu kwa mujibu wa sheria.

Wakili wa mshtakiwa, Melchizedek Lutema aliomba mteja wake apewe adhabu ndogo, ni mkosaji wa mara ya kwanza, ana matatizo ya afya na amekaa rumande kwa miaka minne.

Akitoa adhabu, Hakimu Shaidi alisema amezingatia hoja za pande zote mbili, mshtakiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza na amekaa rumande muda mwingi wa kutosha, ameona na kujifunza mengi.

Alisema mshtakiwa alikubali kwa hiari kuingia makubaliano ya kumaliza kesi kwa njia ya muafaka ambayo haiumizi upande wowote.

"Kwa kuzingatia hayo mahakama inakuachia huru kwa masharti ya kutotenda kosa la jinai tena na utakuwa chini ya uangalizi mwaka mmoja," alisema Hakimu Shaidi.

Alisema mahakama ilitoa uamuzi huo ili kumpa nafasi mshtakiwa ya kutimiza makubaliano waliyofikia.

Pia Hakimu Shaidi, alisema hati za kusafiria za mshtakiwa zishughulikiwe kiutawala na endapo utatokea ugumu upande wa utetezi wawasilishe maombi mahakamani.

Kabla ya hukumu, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alisoma mkataba waliokubaliana Juni 11, mwaka huu kati ya DPP na mshtakiwa.

Alidai mshtakiwa alikiri kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na anadaiwa kati ya Novemba 29, mwaka 2013 na Januari 23, mwaka 2014 maeneo ya Benki ya Stanbic Kinondoni na Benki ya Mkombozi Tawi la St Joseph wilayani Ilala kwa udanganyifu alijipatia Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh. 309,461,300,158.27.

Wankyo alidai katika mkataba mshtakiwa amekubali kulipa fidia ya Sh. 26,946,487,420.80 na alishalipa Sh. milioni 200.

Pia mshtakiwa amekubali kuweka dhamana mtambo wa IPTL uliopo eneo la Salasala Block D kiwanja namba 292. Wakili wa Serikali Mwandamizi, Renatus Mkude katika maelezo ya awali alidai kwamba katika akaunti ya Escrow iliyokuwapo Benki Kuu ya Tanzania, kulikuwa na fedha kwa ajili ya malipo ya umeme.

Mshtakiwa aliandika maombi BoT ya kuhamisha Dola za Marekani milioni 22 na Sh. bilioni 309 kwenda katika akaunti mbili tofauti zilizopo Stanbic benki.

BoT ilihamisha fedha hizo ambazo katika uchunguzi zilitakiwa kulipiwa kodi TRA jumla ya Sh. 26,946,487,420.80.

Wakili wa utetezi, Melchisedek Lutema alidai huo ndio ukweli na ndio msimamo wa pande zote mbili.

Juni 2017, Seth katika kesi hiyo alishtakiwa pamoja na mfanyabiashara, James Rugemalira na wakili Makandege Rugemalira, ambaye ni Mkurugenzi wa VIP na mmiliki mwenza wa zamani wa IPTL na Seth ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa PAP, wakidaiwa kutenda makosa hayo katika Jiji la Dar es Salaam na nchi za Afrika Kusini, Kenya na India.

Habari Kubwa