Sethi alilia mahakama kumwona wakili

24May 2019
Hellen Mwango
DAR
Nipashe
Sethi alilia mahakama kumwona wakili

MFANYABIASHARA Habinder Sethi anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kumpa kibali cha kuonana na wakili wake mahabusu ya gereza la Ukonga kwa sababu miezi sita sasa imepita bila kuwasiliana naye.

Seth na mwezake James Rugemarila, walifikishwa kwa mara ya kwanza katika mahakama hiyo Juni 19, 2017, wakikabiliwa na mashtaka 12 yakiwamo ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha, hivyo kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27

Bilionea huyo alitoa madai yake jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Awali, Wakili wa Serikali Wankyo Simon, alidai kuwa kesi hiyo ilipangwa jana kwa ajili ya kutajwa na kwamba upelelezi bado haujakamilika.

Hata hivyo, Sethi aliomba mahakama imruhusu kutoa malalamiko yake na hatiaye  ilimkubalia.

"Mheshimiwa hakimu, wakili wangu anapokuja gerezani kupata maelekezo yangu, maofisa wa gereza wanamzuia. Naiomba mahakama hii imruhusu wakili wangu aje nizungumze naye kuhusu mustakabali wa kesi yangu. Nina miezi sita sasa sijapata haki yangu ya kisheria," alidai Sethi.

Kutokana na madai hayo, Hakimu Shaidi aliwaagiza maofisa wa magereza wamruhusu wakili wake ili aonane  na mshtakiwa huyo kwa kuwa ni haki yake ya msingi kuonana naye.

Alisema kesi hiyo itatajwa Juni 10, mwaka huu, itakapokuja kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa warudishwe rumande.

Sethi na Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu , kughushi, kutoa nyaraka za kughushi.

Katika shtaka la kwanza, washtakiwa wanadaiwa kuwa kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19 , 2014 jijini Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Katika shtaka la pili la kujihusisha na mtandao, washtakiwa hao kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19,2014 jijini Dar es Salaam wakiwa si watumishi wa umma wanadaiwa kutekeleza mtandao huo wa uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.

Katika shtaka la tatu, Sethi anadaiwa kuwa Oktoba 10, 2011 katika mtaa wa Ohio Ilala jijini Dar es Salaam. akiwa na nia ya ulaghai, alighushi fomu namba 14 ya usajili wa kampuni na kuonesha yeye ni Mtanzania anayeishi Kitalu namba 887 Mtaa wa Mrikau, Masaki wakati akijua ni uongo.

Habari Kubwa