SGA yapata tuzo ya juu maonyesho ya madini

03Oct 2021
Na Mwandishi Wetu
GEITA
Nipashe Jumapili
SGA yapata tuzo ya juu maonyesho ya madini

KAMPUNI ya ulinzi ya SGA Security imepongezwa kwa maendeleo yake ya kiteknolojia katika kutekeleza majukumu yake yaliyoiwezesha kushinda tuzo kwenye maonyesho ya nne ya teknolojia kwenye Sekta ya Madini yaliyofanyika mkoani Geita hivi karibuni.

Katika maonyesho hayo ambayo yalifunguliwa rasmi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kushirikisha kampuni zaidi ya 400 kutoka ndani na nje ya Tanzania, kampuni hiyo iliibuka mshindi katika kipengele cha teknolojia katika usafirishaji na usalama.

Akizungumzia mafanikio ya kampuni hiyo, Waziri wa Madini, Doto Biteko, alipongeza maendeleo yake ya kiteknolojia ambayo alisema ni ya miaka mingi na yamepelekea kampuni nyingi ya madini kuwa na imani nayo, hivyo kuingia nayo mikataba ya ulinzi.

"Nitoe wito kwa uongozi wa kampuni hii kuendelea kuwa na uhusiano mzuri na ushirikiano wa dhati na serikali katika kuhakikishia ulinzi na usalama wa madini yetu dhidi wale wenye nia mbaya”, alisema.

Waziri Biteko aliishukuru kampuni huyo kwa kukubali kuwa moja wapo ya wadhamini wa maonyesho hayo ya kila mwaka na ambayo hushirikisha wadau wa sekta ya madini kutoka ndani ya nje ya nchi ambao hufanya maonyesho yanayohusiana na shughuli wanazofanya katika sekta hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Geita ambao ndiyo wenyeji wa maonyesho hayo, Rosemary Senyamule, aliipongeza SGA kwa mafanikio hayo na kuwataka wachimbaji wadogo na wakubwa kutumia huduma za teknolojia ya hali ya juu katika nyanja za ulinzi zinazotolewa na kampuni hiyo.

"Kwa kushirikiana na kampuni ya SGA mtajihakikishia ufanisi zaidi na ulinzi wa kutosha wa mali zenu hata kama hamtakuwa ameneo ya ofisi zenu na machimboni”, alisema na kuongeza kampuni nyingine hazina budi kuiga mfano wa SGA," alisema.

Makamu wa Rais wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML), Simon Shayo, alipongeza SGA kwa kuwekeza kwenye teknolojia ya ulinzi.

"Wengine wanadhani suala la ulinzi ni la mlinzi aliyebeba rungu au silaha nyingine, la hasha kuna zaidi ya hayo; SGA imewekeza kwenye teknolojia ya kisasa katika ulinzi jambo linalowatofautisha na kampuni nyingine”, alisema.

 SGA Tanzania, Eric Sambu, alibainishwa kufurahishwa kwake kutokana na mafanikio ya kampuni hiyo kutambuliwa na wadau mbalimbali ikiwamo Serikali, mafanikio ambayo alisema walistahili kuyapata kutokana na kujituma kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo.

Aliwapongeza wafanyakazi wa kampuni hiyo kwa kuonyesha uwezo na mafanikio ya kiteknolojia ya kampuni hiyo ya ulinzi ambayo alisema huwapa wateja wake thamani halisi ya huduma wanazolipia ili kuzipata.

SGA ni kampuni kongwe ya ulinzi nchini iliyoanzishwa mwaka 1984, ikijulikana kama Group 4 Security. Kwa sasa imeajiri wafanyakazi zaidi ya 5,000 nchi nzima.

Habari Kubwa