Shahidi adai alikimbia mihemko ya Chadema

04Jul 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Shahidi adai alikimbia mihemko ya Chadema

KOPLO Charles wa Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, amedai mahakamani katika kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)-

-kwamba mihemko ya wafuasi wa chama hicho, ilisababisha akimbilie kwenye gari la jeshi hilo kunusuru kamera yake ya video.

Aidha, alidai kuwa mihemko hiyo ilisababishwa na hamasa aliyoitoa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kutoa kauli ya kuwapandikiza chuki wafuasi hao dhidi ya serikali.

Ushahidi huo aliutoa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba, wakati akisikiliza ushahidi wa Jamhuri dhidi ya vigogo tisa wa Chadema akiwamo Mbowe.

Katika ushahidi huo, jopo la Jamhuri liliongozwa na Mawakili wa Serikali Wakuu, Faraja Nchimbi, Paul Kadushi, Dk. Zainabu Mango, Mawakili wa Serikali Jacqueline Nyantori, Wankyo Simon na Salim Msemo.

Akiongozwa na Wakili Kadushi,  shahidi alidai kuwa Februari 16, 2018  alipangiwa kazi kama mwandishi wa habari kuripoti habari za mkutano wa kufunga kampeni wa Chadema katika viwanja vya Buibui vilivyoko Kinondoni, Dar es Salaam.

Alidai kuwa alijiandaa na vitendea kazi vyake ikiwamo kamera ya kupiga picha za video na ilipofika saa 10 jioni, alifika katika viwanja hivyo kwa ajili ya kuanza kazi.

"Nilipofika watu walianza kukusanyika na mshereheshaji alitangaza kwamba viongozi wakuu wa chama wameshafika. Baada ya muda wabunge na viongozi wakuu walipanda jukwaani nilimsikia Mbowe akitoa kauli za kufanya hamasa ya kuichukia serikali," alidai.

“Wanachama walipata hamasa na mihemko iliyosababisha wapate jazba ya kuichukia serikali na vyombo vya ulinzi na usalama. Wananchi waliokuwa wamekaa walinyanyuka na kuhamasika, mimi na waandishi wenzangu tulitawanyika pale tuposimama karibu na jukwaa, nilikimbilia kwenye gari la polisi kunusuru kamera," alidai Koplo Charles.

Aliendelea kudai kuwa alifika ofisini salama na alikwenda kumpa taarifa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa (RCO) na akamwagiza kutunza picha za video alizopata kwenye mkutano huo kwa kuwa atatumia kama kielelezo na kwamba tayari bosi wake huyo alishafungua kesi dhidi ya vigogo wa Chadema.

Jopo la utetezi liliongozwa na Wakili Profesa Abdallah Safari, Peter Kibatala, John Mallya na Hekima Mwasipu.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine ni Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya; Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko;  Katibu Mkuu wa Chadema, Vicent Mashinji; Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu  Zanzibar,  Salum Mwalimu,  Mbunge wa Kibamba, John Mnyika;  Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Februari Mosi na Februari 16, mwaka huu Mbowe na wenzake wakiwa Kinondoni, Dar es Salaam kwa pamoja walikula njama na wengine ambao hawapo mahakamani ya kutenda kosa la jinai ikiwamo kuendelea na mkusanyiko isivyo halali na kusababisha chuki na uchochezi wa uasi.

Ilidaiwa kuwa Februari 16, mwaka jana, Bulaya  alishawishi kutenda kosa la jinai katika viwanja vya Buibui vilivyoko Kinondoni, Dar es Salaam kwa kuwataka  wakazi wa eneo hilo kufanya maandamano yenye vurugu.

Pia ilidaiwa kuwa Februari 16, mwaka jana katika barabara ya Kawawa eneo la Konondoni Mkwajuni kwa pamoja washtakiwa na wenzao zaidi ya 12, walifanya mkusanyiko na kukaidi amri halali ya ofisa wa Jeshi la Polisi Gerald Ngiichi na kusababisha kifo cha Akwilina Akwiline na askari polisi wawili Konstebo Fikiri na Koplo Rahim Msangi kujeruhiwa.

Ilidaiwa siku ya tukio la kwanza na la pili,  katika viwanja vya Buibui, kwenye mkutano wa hadhara, Heche alitoa lugha ya  kuchochea chuki alitamka matamshi kwamba: "Kesho patachimbika upumbavu ambao unafanywa kwenye nchi hii...wizi unaofanywa na serikali ya awamu ya tano... watu wanapotea... watu wanauawa  wanaokotwa kwenye mitaro lazima ukome...", ambayo yanadaiwa yalielekea kuleta chuki kati ya serikali na Watanzania.

Washtakiwa wote waliposomewa mashtaka yao kwa nyakati tofauti walikana.