Shahidi adai alipigwa jiwe na kupoteza fahamu

16May 2019
Hellen Mwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Shahidi adai alipigwa jiwe na kupoteza fahamu

SHAHIDI wa tatu, Koplo Rahimu Ramadhani, katika kesi ya uchochezi inayomkabili Mwenyekiti Taifa wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), -

Freeman Mbowe na wenzake wanane, amedai mahakamani siku ya tukio alipigwa jiwe shingoni na kumsababishia kupoteza fahamu wakati akiwazuia waandamanaji wa chama hicho.

Kadhalika alidai kuwa maandamano hayo yaliongozwa na Mbowe, Halima Mdee na washtakiwa wengine watano ambao hawafahamu majina yao.

Koplo Ramadhani alitoa madai hayo jana wakati akitoa ushahidi wake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam iliyoketi chini cha Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Upande wa Jamhuri uliongozwa Mawakili wa Serikali Wakuu, Faraja Nchimbi, Paul Kadushi na Mawakili wa Serikali, Wankyo Simon na Jackline Nyantori.

Akiongozwa na Wankyo, shahidi huyo alidai kuwa Februari 16, 2018 aliingia kazini saa 12:00 asubuhi na kituo chake cha kazi ni Oysterbay, jijini Dar es Salaam.

Alidai kuwa aliingia kazini na kupangwa doria mahali tofauti katika mkoa huo wa kipolisi.

"Kati ya saa 11 na 11:15, alasiri tukiwa eneo la Mwenge mimi na makostebo wanne na afande wetu Inspekta Mohammed Mzelengi tulisimama barabara ya ITV tukijadili tuelekee wapi kuendelea na kazi," alidai na kuongeza:

"Kupitia redio upepo tulipokea maelekezo kutoka kwa afande Dotto akitutaka tuelekee katika viunga vya Buibui kuongeza nguvu ya ulinzi, tulipofika eneo hilo nilimwona Mbowe akimnyang'anya kipaza sauti mgombea akitoa maelekezo kuwashinikiza viongozi wenzake kufanya maandamano," alidai Koplo Ramadhani.

Alidai kuwa alisikia wananchi wakiitikia maelekezo kwamba ‘lazima tuandamane kwenda kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni' alinukuu shahidi.

Koplo Msangi alidai, mbowe baada ya kuwatangazia wanachama wake waandamane, alishuka chini na kushikana mikono na viongozi wenzake waliokuwapo eneo hilo na kuandamana wakipitia barabara ya Mwananyamala, Kinondoni Studio hadi Kawawa.

Alidai kuwa wandamanaji walikuwa wameshika mawe, marungu na chupa za maji na walipofika eneo la Mkwajuni, polisi walitoa ilani ya kuwataka watawanyike, lakini walikaidi.

Alidai, waandamanaji hao waliwarushia polisi mawe na marungu na yeye alipigwa jiwe eneo la shingoni na baada ya hapo hakufahamu kilichoendelea na kujikuta yupo hospitali amelazwa.

Alidai alilazwa katika hospitali ya polisi iliyopo Barabara ya Kilwa na aliposhtuka alikumbuka kwamba alikuwa na silaha aina ya SMG ambayo wakati huo hakuwa nayo.

Alidai kuwa kesho yake alimwuliza bosi wake kuhusu silaha yake akafahamishwa kwamba ilirejeshwa Kituo cha Polisi Oysterbay.

Wakili wa utetezi, Peter Kibatala alimhoji kama ifuatavyo:

Kibatala: Shahidi utaratibu wa Jeshi la Polisi ukoje askari anapokabidhiwa silaha anaruhusiwa mtu mwingine kuirejesha?

Shahidi: inategemea na mazingira ya askari.

Kibatala: Ieleze mahakama kama inaruhusiwa au hairuhusiwi?

Shahidi: Inawezekana kurudishwa na mtu mwingine inategemea na mazingira ya mhusika.

Mbali ya Mbowe, washtakiwa wengine ni, Mbunge wa Bunda Ester Bulaya, Mbunge wa Tarime Mjini Esther Matiko, Katibu Mkuu Taifa ,Katibu Mkuu Taifa,Vicent Mashinji, Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Taifa, Zanzibar, Salum Mwalimu, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Kawe, Mdee na John Heche.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Februari mosi na Februari 16, mwaka  jana na wenzake wakiwa Kinondoni, Dar es Salaam kwa pamoja walikula njama na wengine ambao hawapo mahakamani ya kutenda kosa la jinai ikiwamo kuendelea na mkusanyiko isivyo halali na kusababisha chuki na uchochezi wa uasi.

Ilidaiwa kuwa Februari 16, mwaka huu Bulaya alishawishi kutenda kosa la jinai katika viwanja vya Buibui vilivyopo Kinondoni,jijini Dar es Salaam alishawishi wakazi wa eneo hilo kutenda kosa la jinai kwa kufanya maandamano yenye vurugu.

Ilidaiwa Februari 16,mwaka huu barabara ya Kawawa eneo la Mkwajuni wilaya ya Kinondoni kwa pamoja washtakiwa na wenzao zaidi ya 12, walifanya mkusanyiko na kukaidi amri halali ya ofisa wa jeshi la polisi Gerald Ngiichi na kusababisha kifo cha Akwilina Akwiline na askari polisi wawili Konstebo Fikiri na Koplo Rahim Msangi kujeruhiwa.

Ilidaiwa siku ya tukio la kwanza na la pili, katika viwanja vya Buibui vilivyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam, kwenye mkutano wa hadhara mshitakiwa Heche alitoa lugha ya kuchochea chuki alitamka matamshi kwamba "Kesho patachimbika upumbavu ambao unafanywa kwenye nchi hii...wizi unaofanywa na serikali ya awamu ya tano...watu wanapotea...watu wanauawa, wanaokotwa kwenye mitaro lazima ukome... “alinukuliwa na kudaiwa kuwa maneno yaliyoelekea kuleta chuki kati ya serikali na Watanzania.

Washtakiwa wote waliposomewa mashtaka yao kwa nyakati tofauti walikana.

Habari Kubwa