Shahidi adai kumkamata Sabaya na bastola, simu 10

08Dec 2021
Allan Isack
Arusha
Nipashe
Shahidi adai kumkamata Sabaya na bastola, simu 10

OFISA Uchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Shaban Hemed (41), amedai walimkamata aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya, akiwa na bastola aina ya Glock 17 ikiwa na magazini mbili zenye risasi 21.

Vilevile, shahidi huyo amedai mahakamani kuwa mbali na bastola hiyo, walimkamata mshtakiwa huyo akiwa na simu zaidi 10 na Ipad moja katika chumba ambacho alikuwa amelala.

Akisilisha ushahidi wake jana, shahidi huyo alidai walimkamata Sabaya usiku wa manane baada ya kugoma kwenda katika ofisi za taasisi hiyo kwa ajili ya kufanyiwa mahojiano.

Ofisa huyo ambaye ni shahidi wa 11 katika kesi ya uhujumu uchumi namba 27 inayomkabili Sabaya na wenzake sita, alitoa madai hayo jana mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Patricia Kisinda.

Mbali na Sabaya washtakiwa wengine katika shauri hilo ni Silvester Nyengu (26), Enock Togolani (41), Watson Mwahomange (27), John Odemba, Jackson Macha (29) na Nathan Msuya (31).

Shahidi huyo alidai alihusika katika uchunguzi wa jalada la kesi hiyo ambalo lilikuwa la Sabaya kulazimisha kupewa rushwa ya Sh. milioni 90 kutoka kwa Francis Mroso.

Alidai tuhuma zilikuwa za matumizi mabaya ya madaraka, utakatishaji wa fedha, kujihusisha na vitendo vya rushwa, kuongoza genge la uhalifu na kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Filex Kwetukia, shahidi huyo alidai Mei 19, mwaka huu, akiwa ofisini kwake makao makuu ya TAKUKURU, majira ya mchana, bosi wake alimtaka ajiandae, kulikuwa na safari ya kwenda mikoa ya Arusha na Kilimanjaro na kwamba Mei 20, mwaka huu, akiwa na maofisa wa taasisi hiyo, waliondoka makao makuu kwenda mkoani Kilimanjaro kwa kazi hiyo.

“Uchunguzi wetu ulikuwa katika sehemu kuu mbili, ambazo ni Wilaya za Hai na Moshi, na tulichunguza taarifa fiche na kuzichakata kwa kuwahoji watu mbalimbali na baada ya hapo Mei 23 mwaka huu, tulikwenda Arusha na kutoa taarifa kwa Mkuu wa TAKUKURU Arusha na tulimweleza sababu ya kwenda na alitueleza kwamba ana jalada la tuhumu hizo ambalo lilihama kutoka polisi.

“Nanukuu maneno ya mkurugenzi alipozungumza na Sabaya kuna uchunguzi unafanyika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, hivyo anatakiwa kufika katika ofisi za mikoa hiyo, na alikubali kwenda lakini hadi kufikia Mei 24, mwaka huu, hakufika.

“Kutokana na kutompata kwenye simu Mei 25, mwaka huu, mkurugenzi alitoa kibali cha kumtafuta na kumkamata.

“Baada ya kupewa kibali cha kumkamata tulianza kukusanya taarifa za kiintelijensia kujua wapi muhusika yupo na tulibaini kwamba miongoni mwa watuhumiwa tunaowatafuta, wapo kituo Kikuu cha Polisi Arusha, ambao ni John Odemba na Daniel Mbura," alidai.

Aliendelea kudai kuwa baada ya kuwachukua watuhumiwa hao kituo cha polisi, waliwahoji na walikiri tukio na Mei 22 na walikubali kupata mgawo wa fedha zilizochukuliwa kupitia maelezo waliyoandika.

“Baada ya kutoka Arusha, tulikwenda Moshi, tulipata mwanga Sabaya anapatikana Dar es Salaam. Na nilitoa taarifa kwa bosi wangu na nilipata kibali cha kwenda kumkamata huko.

"Na kwa mujibu wa taarifa za kichunguzi walikuwa 'Beach Kindimbwi, Mtaa Kolele katika nyumba za malazi za 'MG and Home Estate'.

“Tulifika chumba cha Sabaya namba 101 na 102, sikufanikiwa kuwakuta, walishatoka na baada ya kuwakosa na kujiridhisha, nilifanya mazungumzo na meneja wa apartment hizo, kama anamfahamu alikiri kuwa alikuwapo na vijana wake.

"Meneja huyo alitueleza anamfahamu Sabaya kwa kuwa alimwona katika mitandao na kijamii na alifanya malipo ya kwanza kwa simu yenye jina lake, kiasi cha Sh. 580,000, simu ambayo ilikuwa imebebwa na Silvester Nyegu na malipo ya pili yalikuwa ya Sh. 246,000, ilitumika namba ya Enock Togolani Mkeni na malipo ya tatu yalikuwa ya Sh. 968,000," alidai.

Shahidi huyo alidai kuwa baada ya kujiridhisha walikuwa wameshaondoka eneo hilo, alipitia kitabu cha kumbukumbu za magari yanayoingia na kutoka katika hoteli hiyo, akabaini walitumia gari aina ya Toyota Land Cruser V8 lenye namba za usajili T222 BDW.

Alidai kwamba kwa mujibu wa uchunguzi wao, walibaini walihamia eneo la Oasisi Village kwenye apartment ya Mount Uluguru na walipofika huko waliwakamata watu wanne katika chumba kimoja ambao ni Silvester Nyegu, Watson Mwahomange, Enock Togolani na Onjung' Saitabau na chumba kingine walimkamata Sabaya na mwanamke anayetambulika kwa jina la Jesca Thomas.

“Niliwaeleza dhumuni la kuwakamata ni kuwapeleka katika ofisi za TAKUKURU zilizoko Upanga, Dar es Salaam na walikubali kuongozana na mimi," alidai.

Akihojiwa na Wakili wa Utetezi, Mosses Mahuna, shahidi huyo alidai mahakamani huko kwamba alidai shauri hilo lilikuwa na wapelelezi wengi na kila mmoja alikuwa na nafasi yake ya kupeleleza katika kesi hiyo.

Alidai kuwa kabla ya kufika TAKUKURU, jalada hilo lilikuwa polisi kwa hatua za kiuchunguzi.

Habari Kubwa