Shahidi adai kupokea fedha za uuzaji kiwanja kwa Gugai

11Jul 2019
Hellen Mwango
Nipashe
Shahidi adai kupokea fedha za uuzaji kiwanja kwa Gugai

SHAHIDI wa 20 katika kesi ya kutakatisha fedha inayomkabili Mhasibu Mkuu wa zamani wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Godfrey Gugai, amedai mahakamani kuwa alipokea Sh. milioni 80 na si 60 kama zilivyoandikwa kwenye mkataba wa mauziano.

Godfrey Gugai.

Kadhalika, shahidi huyo, Abubakar Hamisi (46), amedai kuwa mkataba huo ulikuwa wa mauziano ya kiwanja kilichoko Boko Uninio, Dar es Salaam na kwamba anamfahamu Gugai kwa sababu ni jirani yake.

Ushahidi huo ulisikilizwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam chini ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba.

Katika kesi hiyo, upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Awamu Mbwagwa.

Shahidi alidai kuwa anamfahamu Gugai kwa sababu ni jirani yake na pia aliwahi kufanya naye biashara.

"Tulifanya makubaliano kati ya familia yetu na ile ya Gugai ya kuuziana kiwanja namba 64 block C kilichoko Boko Ununio kwa Sh. milioni 80 na si milioni 60 zilizoandikwa kwenye mkataba wa mauziano," alidai.

“Familia zote mbili zilifanya makubaliano, Gugai alimwita mwanasheria wake alikwenda kuandaa mkataba. Jioni tulikwenda nyumbani kwake, tulipousoma tuliuafiki tukalipwa fedha." alidai Abubakar.

Aliendelea kudai kuwa mauziano hayo yaliyofanyika nyumbani kwake akiwa na mwanasheria, uliandikwa hivyo ili kupata nafuu ya kodi.

Shahidi huyo aliiomba mahakama kupokea mkataba huo wa mauziano ya kiwanja kama kielelezo baada ya kuutambua kwa majina na saini.

Upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Semi Malimi, ulipinga kupokewa kwa mkataba huo akiadai ni nakala na si halisi.

"Nakala yoyote inayotolewa mahakamani lazima iwe halisi kwa mujibu wa sheria kifungu 67(1) na kama ni nakala yapo mazingira yanayoruhusu ipokewe." alidai wakili Malimi.

Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 11, 2019 atakopotoa uamuzi kama kielelezo hicho kipokewe au la.

Gugai na mwenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka 43, yakiwamo 19 ya kughushi, 23 utakatishaji fedha na moja ni kumiliki mali zilizozidi kipato halali, ambalo linamkabili Gugai.

Mbali na Gugai, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasin Katera.

Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa mahakamani Novemba 16, 2017 na walinyimwa dhamana kutokana na shtaka la utakatishaji kutokuwa na dhamana.

Gugai anakabiliwa na kosa la kumiliki mali kinyume na kipato chake, ambapo alitenda kosa hilo kati ya January 2005 na Disemba 2015.

Inadaiwa kuwa akiwa Takukuru Dar es Salaam, Gugai alikuwa akimiliki mali za zaidi ya Sh. bilioni 3.6 ambazo hazilingani na kipato chake huku akishindwa kuzitolea maelezo.

Habari Kubwa