Shahidi adai kushuhudia unga mweupe mbele ya Nsembo

28May 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Shahidi adai kushuhudia unga mweupe mbele ya Nsembo

SHAHIDI Kelvin Charles (22), amedai mahakamani alishuhudia unga mweupe na wa njano ukifungwa mbele ya Abdul Nsembo (45) na mke wake Shamim Mwasha (41), katika bahasha tano tofauti.

Kadhalika, alidai kuwa baada ya bahasha hizo kufungwa yeye pamoja na washtakiwa wote wawili waliandika majina yao matatu na kutia saini.

Ushahidi huo dhidi ya kesi ya Uhujumu Uchumi namba 4/2020, umesikilizwa katika Mahakama Kuu Divisheni ya Uhujumu Uchumi na Rushwa maarufu kama mafisadi iliyoketi chini ya Jaji Elinaza Luvanda.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Constantine Kakula, shahidi alidai kuwa anafanyakazi katika kampuni ya usafi ya Kishingweni kama mfanyausafi.

Alidai kuwa Mei 2, mwaka huu saa 2:00 asubuhi akiwa anaendelea na kazi ya usafi nje ya jengo la Utumishi Kivukoni, jijini Dar es Salaam, alifuatwa na mwanamke.

"Nikiwa nafanya usafi nilifuatwa na Inspekta Johari akanieleza kwamba anamuhitaji kwenda kushuhudia ufungaji wa vielelezo kwenda kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, alikubali alikwenda ofisini kwake akawakuta washtakiwa wote wawili Nsembo na Mwasha," alidai na kuongeza.

"Alileta vielelezo vikiwa pamoja akaviweka pamoja mezani, nilishuhudia akiviwekea alama moja mpaka tano na A mpaka E, mimi na washtakiwa wote tuliandika majina yetu na tulitia saini juu ya bahasha zote tano," alidai Charles.

Alidai kuwa anawatambua washtakiwa wote kwa sababu alitambulishwa siku alipoitwa na Inspekta Johari kwenda kwenye ofisi zao kwa ajili ya ushahidi huru.

Akihojiwa na mawakili wa utetezi, Nassoro Juma, shahidi alidai kuwa siku ya tukio aliwaona washtakiwa kwa macho na kwamba ulifanyika utambulisho.

Alidai kuwa hajawahi kutoa ushahidi dhidi ya watuhumiwa katika mamlaka hiyo.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kusafirisha dawa hizo za kulevya, Mei mosi, mwaka huu wakiwa eneo la Mbezi Beach, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam kinyume na sheria ya uhujumu uchumi.

Habari Kubwa