Shahidi adai maneno yalimfanya kuichukia polisi

17May 2019
Hellen Mwango
DAR
Nipashe
Shahidi adai maneno yalimfanya kuichukia polisi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imeambiwa na shahidi wa Jamhuri, Mashaka Duma, katika kesi ya uchochezi inayomkabili, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, kwamba yeye ni shabiki wa mbunge huyo, anaposikia sauti yake anafurahi na anapomuona kwenye televisheni.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe.

Alidai kuwa alipomsikia akizungumzia mauaji ya Uvinza Kigoma, aliamini na kuwachukia polisi.

Mashaka alitoa madai hayo jana katika mahakama hiyo wakati akitoa ushahidi wa Jamhuri mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, anayesikiliza kesi hiyo.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka, shahidi alidai roho yake imetulia baada kutoa hisia zake mahakamani kwamba analichukia Jeshi la Polisi kwa kitendo wanachodaiwa kukifanya Uvinza Kigoma.

Shahidi mwingine, Shabani Hamisi, amedai kitendo cha Tundu Lissu, kushambuliwa kwa risasi na hajawahi kukamatwa mtu kuhusiana na tukio hilo kilimfanya aamini maneno ya mshtakiwa kuwa Kigoma Uvinza kuna watu waliuawa.

Alidai polisi walipokuwa wakipita na gari lao Manzese walikuwa wakizomea kwamba wauaji hao.

Akihojiwa na Wakili wa Utetezi, Peter Kibatala, kuhusu watu waliokamatwa kwa kuzomea polisi, alidai hakuna aliyekamatwa.

Shahidi huyo aliangalia Youtube akiwa Kimara Korogwe, Dar es Salaam. Kesi itaendelea kesho saa tatu asubuhi.

Awali aliposomewa maelezo ya awali, Zitto alikana kwamba Oktoba 28, 2018 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za makao makuu ya chama cha ACT-Wazalendo kwa nia ya kuleta chuki miongoni mwa wananchi wa Tanzania dhidi ya Jeshi la Polisi, alitoa maneno ya uchochezi.

Zitto alikana maneno ambayo anadaiwa kuyasema: "Watu ambao walikuwa ni majeruhi katika tukio la mapambano baina ya wananchi na polisi, wakiwa wamekwenda hospitali kupata matibabu katika kituo cha afya cha Nguruka, polisi wakapata taarifa kuwa kuna watu wanne wamekwenda hospitali kituo cha afya Nguruka kupata matibabu wakawafuata kule wakawaua”.

Jamhuri inadai maneno hayo yalikuwa ni ya uchochezi yenye kuleta hisia ya hofu na chuki.

Mshtakiwa anadaiwa kutoa maneno kwamba: 'Lakini tumefuatilia kwa kina jambo hili, taarifa ambazo tumezipata kutoka kijijini Mpeta Nguruka, Uvinza ni mbaya ni taarifa ambazo zinaonyesha wananchi wengi sana wameuawa, na Jeshi la Polisi, pamoja na kwamba Afande Sirro wamekwenda kule, halijatoa taarifa yoyote kuhusu wananchi...kama hawa Wanyantuzu walivamia eneo la Ranchi, kuna taratibu za kisheria za kuchukua nasiyo kuwauwa, wananchi wengine sana wamekufa'.

Inadaiwa Zitto katika mkutano huo huo alitoa waraka kwa umma ikiwa na maneno ya kichochezi kwa nia ya kuleta chuki kwa Watanzania dhidi ya polisi.

Pia Zitto anadaiwa alitoa maneno yafuatayo: 'Tumekuwa tukifuatilia kwa kina yanayojri yote huko Uvinza ...tunasikitika kusema kuwa taarifa tunazozipata kutoka Uvinza zinaogofya mno, kwani tunaambiwa kuwa wananchi zaidi ya 100 wa kabila la Wanyantuzu wamepoteza maisha kwa kupingwa risasi na polisi, wengine wakisemwa kuuawa hata wakiwa kwenye matibabu hospitalini baada ya kujeruhiwa kwenye purukushani na Jeshi la Polisi’.

Habari Kubwa