Shahidi adai Mbowe alishawishi maandamano

15May 2019
Hellen Mwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Shahidi adai Mbowe alishawishi maandamano

SHABAN Abdallah (19), amedai mahakamani katika kesi ya uchochezi inayowakabili vigogo tisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwa alimwona Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe,-

Freeman Mbowe.

akiwahamasisha wananchi kuendelea kuandamana kuwasogelea askari hata baada ya tangazo la kuwaamuru kutawanyika kutolewa.

Abdallah ambaye fundi wa kuchomea vyuma na mkazi wa Kinondoni Moscow, Dar es Salaam, ni shahidi wa pili wa upande wa Jamhuri katika kesi hiyo, alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Paul Kadushi, shahidi huyo alidai kuwa Februari 16, 2018 asubuhi alikuwa katika eneo lake la kazi Kinondoni Moscow anakoendesha shughuli zake za kumwingizia kipato kwa kutengeneza vitanda na vyuma.

Siku hiyo, alidai kuwa saa 11 jioni, alipewa fedha na bosi wake kwa ajili ya kwenda Mkwajuni kununua vifaa vya kazi na alifika dukani kwa mtu aliyemtaja kwa jina la baba John na kununua vitu hivyo.

"Nikiwa pale dukani wakati tunaendelea kufanya hesabu kabla ya kuchukua mzigo, kwa mbali tulisikia vurugu lakini hatukuzifuatilia sana. Muda ulivyozidi kwenda vurugu zilizidi kutusogelea, tulitoka dukani na kwenda nje kuangalia tukaona watu wengi katikati ya barabara wakitokea eneo la Morocco wakielekea Magomeni huku wakiwa wameshika mawe na marungu," alidai.

"Waandamanaji hao walionekana kuwa katika hali ya ugomvi na shari. Walikuwa wakiimba 'Hatupoi mpaka mmoja afe watatuua'. Kwa kuwaangalia mimi na baba John tuliweza kuwatambua kuwa ni watu wa Chadema kwa kuwa walikuwa wamevaa sare za chama hicho, skafu na bendera huku viongozi wao wakiwa mbele. Nilimwona  na kumtambua Mbowe, Halima Mdee, John Mnyika na Esther Matiko," alidai shahidi huyo.

Alidai kuwa wakati wakiendelea kuwaangalia waandamanaji hao waliona gari la askari likija nyuma yao huku likiwatangazia watawawanyike lakini waliendelea kuandamanakulisogelea gari la askari na kuanza kuwarushia chupa za maji na mawe.

Akifafanua zaidi, alidai kuwa alipoangalia, alimwona Mbowe akiwahamasisha wananchi kuendelea kuandamana kuwasogelea askari huku wakiwa na viongozi wengine.

"Baada ya waandamanaji kukaidi amri ya polisi tusikia askari wakipiga mabomu ya mochozi na kila mtu alitawanyika kukimbilia njia yake," alidai Abdallah.

Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa kesho ushahidi wa Jamhuri.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine ni katibu Mkuu wa Chadema Djk. Vincent Mashinji; Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya; Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko;   Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa; Naibu Katibu Mkuu Zanzibar; Salum Mwalimu; Mbunge wa Kibamba, John Mnyika;   Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na John Heche wa Tarime Vijijini.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Februari Mosi na Februari 16, mwaka jana, wakiwa Kinondoni, Dar es Salaam, kwa pamoja walikula njama ya kutenda kosa la jinai ikiwamo kuendelea na mkusanyiko isivyo halali na kusababisha chuki na uchochezi wa uasi.

Ilidaiwa kuwa Februari 16, Bulaya alishawishi kutenda kosa la jinai katika viwanja vya Buibui vilivyopo Kinondoni, jijini Dar es Salaam alishawishi wakazi wa eneo hilo kutenda kosa la jinai kwa kufanya maandamano yenye vurugu.

Ilidaiwa Februari 16, barabara ya Kawawa eneo la Kinondoni Mkwajuni, kwa pamoja washtakiwa walifanya mkusanyiko na kukaidi amri halali ya ofisa wa jeshi la polisi Gerald Ngiichi na kusababisha kifo cha Akwilina Akwiline na askari polisi wawili Konstebo Fikiri na Koplo Rahim Msangi kujeruhiwa.

Ilidaiwa siku ya tukio la kwanza na la pili, katika viwanja vya Buibui vilivyoko Kinondoni jijini Dar es Salaam, kwenye mkutano wa hadhara mshitakiwa Heche alitoa lugha ya kuchochea chuki alitamka matamshi kwamba "Kesho patachimbika upumbavu ambao unafanywa kwenye nchi hii...wizi unaofanywa na serikali ya awamu ya tano...watu wanapotea...watu wanauawa wanaokotwa kwenye mitaro lazima ukome... “alinukuliwa na kudaiwa kuwa maneno yaliyoelekea kuleta chuki kati ya serikali na Watanzania.