Shahidi aeleza alivyochunguza miamala katika simu ya Mbowe

14Jan 2022
Kulwa Mzee
Dar es Salaam
Nipashe
Shahidi aeleza alivyochunguza miamala katika simu ya Mbowe

SHAHIDI wa tisa wa Jamhuri, Gladis Fimbari (36) katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, na wenzake watatu, amedai alipewa jukumu la kuchunguza miamala na usajili wa namba tatu za simu.

Fimbari ambaye ni Mwanasheria wa kampuni ya simu za mkononi ya Airtel, amedai kuwa miongoni mwa simu hizo ni pamoja na inayodaiwa kuwa ya Mbowe, Simu nyingine ni ya Luteni Dennis Urio.

Alidai hayo jana Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi mbele ya Jaji Joachim Tiganga wakati akitoa ushahidi kwa kuongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando.

Alidai kuwa Julai 2, 020 akiwa ofisini Morocco, Dar es Salaam, Mkuu wake wa idara alimpa kazi ya kushughulikia miamala ya fedha ya namba tatu.

Shahidi alitaja namba hizo kuwa ni 0782 237913 ambayo katika usajili alidai ilikuwa inamilikiwa na mshtakiwa Halfani Bwire, ya pili 0787 555200 usajili ukionyesha ni ya Luteni Urio na 0784 779944 ambayo katika usajili ilikuwa inamilikiwa na Mbowe.

Katika uchunguzi huo, alidai kuwa alitumia mifumo miwili, wa kwanza wa kupata taarifa za miamala unaoitwa MOBIQUIT unaochukua taarifa na kuhifadhi. Mfumo wa pili alidai unaitwa AGILE, ambao unatumika kupata taarifa za usajili za mteja na katika kazi hizo anatumia kompyuta mpakato au ya kawaida.

Mwanasheria huyo alidai vitendea kazi vimeunganishwa na mifumo ya Airtel na haiwezekani kufanya jambo lolote na pia vimeunganishwa na mfumo wa kutoa taarifa pale inapofanyika kinyume.

Alidai kuwa alipoanza kuchunguza, aliingia kwenye mfumo na kuingiza namba moja ya simu iliyoombwa taarifa yake kisha ikatoa taarifa ambayo aliihakiki kujiridhisha kisha akaichapisha. Alidai kuwa alifanya hivyo kwa namba zote tatu.

Alipohojiwa kama nyaraka alizoandaa akiziona atazikumbuka, alidai atazikumbuka kwa sababu kuna jina lake, saini yake na muhuri wa Airtel.

Fimbari alidai kuwa katika nyaraka hizo aliambatanisha na barua ya maombi kutoka ofisi ya uchunguzi ya Julai Mosi, 2021 iliyoonesha jalada CD/IR/2097/2020 ikiwa na namba tatu zilizoombewa taarifa.

Shahidi aliomba kutoa taarifa hizo kama kielelezo na mawakili wa utetezi, wakiongozwa na Peter Kibatala hawakuwa na pingamizi. Mahakama ilipokea na kuvipa namba vielelezo hivyo.

Katika uchunguzi wake, alidai kuwa Julai 20, 2020 namba 0784 779944 ilifanya muamala kwenda kwenye namba 0787 555200 wa Sh 500,000, muamala wa pili Sh. 199,000 na wa tatu ulifanyika Julai 31, 2020 kutoka namba 0784 779944 kwenda namba 0782 237913 ya Halfani Bwire wa Sh. 80,000.

Luteni Urio ni Mwanajeshi anayedaiwa katika kesi hiyo alitumwa na Mbowe amtafutie makomandoo waliostaafu au waliofukuzwa kazi ili wafanye vitendo vya kigaidi huku maelezo ya onyo ya washtakiwa yakidai kwamba Urio aliwatafutia kazi ya kumlinda Mbowe washtakiwa watatu katika kesi hiyo.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mbowe, Bwire, Adamu Kasekwa na Mohammed Ling'wenya ambao wanashtakiwa kwa kula njama kufanya vitendo vya kigaidi kati ya Mei na Agosti, 2020.

Habari Kubwa