Shahidi aeleza alivyopigwa, kuteswa na Sabaya

26Jul 2021
Allan lsack
Arusha
Nipashe
Shahidi aeleza alivyopigwa, kuteswa na Sabaya

SHAHIDI wa nne upande wa Jamhuri, Hajirini Saad (32), jana amedai mahakamani kupigwa, kuteswa, kuwekwa chini ya ulinzi pamoja na kulazwa kifudifudi na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya (34), wakati akitenda uhalifu katika duka la Mohamed Saa lililopo eneo la ....

Soko Kuu jijini Arusha.

Wakili Mwandamizi wa Serikali, Abdalah Chavula, ndiye aliyekuwa akimuhoji shahidi huyo ambaye alitaka kujua shahidi anajishughulisha na nini na Februari 9, mwaka huu, alikuwa wapi.

Shahidi alisema ni mfanyabiashara wa mapazia, mashuka, vyandarua na mazuria na siku hiyo alikuwa nyumbani kwake na kuipigiwa simu na kaka Mohamed Saad, akimwambia kuna wateja dukani kwake wanataka kununua mapazia kwa bei ya jumla.

Pia, aliiambia mahakama kuwa alimpigia simu tena kumjulisha simu hiyo ilikuwa ya vitisho na watu waliopiga ni maofisa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), na kumuuliza kama ataweza kwenda dukani kuwaangalia watu hao na alimjibu atakwenda kwa kuwa nyumbani kwake ni karibu na dukani hapo.

Alisema alimuaga mke wake na mtoto, lakini mtoto wake aling’ang’ania aende naye na alimchukua kwenda naye dukani.
Shahidi huyo alisema alipofika alikuta mlango umerudishiwa na aliufungua na kuingia ndani dukani.

Alidai alipoingia tu akavutiwa ndani yeye na mtoto wake kwa kuwa kulikuwa na watu ndani dukani.

Shahidi alidai watu walikuwa wengi dukani wengine hakuwafahamu, lakini alipoatazama vizuri alimuona Mkuu wa Wilaya ya Hai Lenga Ole Sabaya akiwa na watu wengine.

Swali: Shahidi kabda ya siku hiyo, kwenda dukani ulishawahi kwenda kwenye duka hilo mara ngapi?

Jibu: Nimekwenda mara nyingi kwa kuwa ni dukani kwa kaka yangu na wakati mwingine amekuwa akiniachia duka kumsaidia kuuza.

Swali: Kwa unavyolijua duka hilo, kwa urefu lina mita ngapi na upana wake?

Jibu: Duka hilo lina urefu wa zaidi ya mita 10 na upana mita kama nne.

Swali: Je ulipofika ndani ya duka uliona nini huko?

Jibu: Nilimuona DC wa Hai, Ole Sabaya, akiwa na watu wengine huko dukani.

Swali: Pale uliposimama wewe na alipokuwa Sabaya kulikuwa na umbali gani?

Jibu: Kulikuwa na umbali kama wa mita mbili na nusu.

Shahidi alidai alipomuona Sabaya, alimuita Mheshimiwa Ole Sabaya, na yeye (Sabaya) alimuuliza wewe ndio Mohamed Hajirini? Akamjibu hapana sio yeye.

Alidai kuwa Sabaya alimuuliza amefuata nini hapo na akamjibu kuwa kaka yake alimwambia aende kuangalia kama kuna shida imetokea dukani kwa kuwa kuna watu wapo hapo.

Alidai kuwa mmoja wa watu waliokuwapo dukani alimshika mtoto wake na yeye aliwaambia wamuachie mtoto aondoke kwa kuwa hana kosa na kwamba kama wasingefanya hivyo kingenuka kwa kuwa angepigana nao kwa sababu sio kwamba hafahamu sheria.

Shahidi huyo alisema Sabaya aliagiza wamfungulie mtoto wake (mwenye umri miaka minane), aondoke kwenda nyumbani.

Alida geti liligongwa kwa nje watu waliokuwa nje walifungua na mtoto akaruhusiwa kuondoka na Sabaya aliagiza apekuliwe.

Alipopekuliwa alidai walichukuwa simu yake, ufunguo wa pikipiki, vitambulisho na leseni ya udereva.

Alidai baadaye walichukua simu na funguo za pikipiki na kumrudishia leseni na vitambulisho vyake.

Wakili alipomuuliza shahidi kama alishawahi kumuona wapi huyo mtu anayemtaja kwa kumwita Sabaya, alisema
hajawahi kuonana naye bali alimuona kwenye vyombo vya habari.

Swali: Wale watu waliokuwa dukani wanauza wakati huo walikuwa wapi?

Jibu: Nilipovutiwa ndani nilimuona mtu mmoja mzee amelazwa chini na amelala kwa tumbo.

Swali: Je kuna mwanamke ulisema alikuwa amefungwa pingu dukani ulimfahamu?

Jibu: Kwa wakati huo sikumfahamu.

Swali: Je hapo dukani ulishuhudia nini?

Jibu: Nimuona Numan Jasini, mjomba wangu akiwa pembeni yangu na amepigishwa magoti.

Swali: Hebu endelea kuieleza mahakama nini kiliendelea au kilijiri huko dukani?

Jibu: Walimgeuza mtu mmoja ambaye alikuwa kwa tumbo chini ya sakafu ndio nikamtambua kuwa ni mzee Salimu ambaye ni fundi umeme na anatutengenezeaga vitu.

Swali: Baada wewe kuwekwa chini ya ulinzi huyo, Sabaya alisemaje?

Jibu: Alikuwa akituambia sisi tunabadilisha fedha kigeni (Dola) na aliendelea kutuambia kwamba sisi ni wauhujumu uchumi na tumeshirikiana na dada yule kuiba dola 70,000 huko Moshi mkoani Kilimanjaro.

Swali: Nini sasa kilifuata baada ya matamshi hayo?

Jibu: Walimtisha na kumuamsha huyo dada wakimwambia kwamba alikwenda dukani hapo kubadilisha Dola ambazo walishirikiana kuziiba kule Moshi.

Swali: Hebu ieleze mahakama sakata hilo, lilivyokuwa likiendelea ulichukua hatua gani?

Jibu: Numan, alikanusha kwa kumwambia Sabaya kuwa hawabadilishi Dola na Sabaya aliagiza dada huyo afunguliwe pingu aliyokuwa amefungwa.

Swali: Umesema huko ndani aliingia mtu mwingine ni nani na ulimtambuaje?

Jibu: Aliingia Bakari Msangi, Diwani wa Kata ya Sombetini na nilimfahamu kwa kuwa ni mtu ambaye tunasali naye msikiti mmoja.

Alipoingia Bakari alisalimia kwa kusema Mheshimiwa Lengai Ole Sabaya habari yako, lakini hakujibiwa kitu. Alirudia kusalimia kwa mara nyingine, lakini hakujibiwa.

Shahidi alidai kuwa Sabaya alimuuliza Bakari kwani hafahamu cheo chake na yeye ni nani? Alimtaka kumuita kwa jina la DC Lengai Ole Sabaya.

Swali: Je baada ya Sabaya kuitikia salamu hiyo nini kilitokea?

Jibu: Alimuuliza Bakari yeye ni nani na amekwenda kufanya nini hapo dukani na Bakari alimwambia kuwa yeye ni Diwani wa Sombeni na amepigiwa simu na na rafiki yake Ali Saad kuwa Sabaya yupo dukani kwake.

Swali: Je siku hiyo muonekano Sabaya ulikuwaje?

Jibu: Alikuwa mweusi, mrefu wa wastani, mnene, alikuwa amevaa kaunda suti ya rangi ya bluu na miwani.

Swali: Sasa shahidi huyo mtu unaweza kumtambua kama yupo humu ndani mahakamani hebu nenda ukamshike bega kama umemuona.

Swali: Je Sabaya aliagiza upewe simu yako ili ufanye nini?

Jibu: Alinipa simu ili kumpigia simu Mohamed Hajirini ili aende dukani kwa kuwa walikuwa wamuhitaji.

Pia, shahidi alidai Sabaya, alimwambia Msangi amsalimie kwa kumuitwa Jenerali DC Sabaya, na baada ya kumsalimia kama alivyotaka alimwambia kwa nini anashirikia na Waarabu.

Alidai wameshirikiana na yule dada kuiba Dola 70,000 na wamekuwa wakimbadilishia kwenye duka hilo na kuwaambia wao ni majambazi na wauhujumu uchumi.

Pia alikwenda kuchukua begi la mkononi la yule dada na alifungua na kutoa kati ya Dola 100 au 200.

Shahidi alidai Msangi alimwambia yeye ni Mkuu wa Wilaya ya Hai, na Arusha kuna DC, TRA na vyombo vya dola na akiangalia hapo hawaoni hata mmoja wao.

Alidai Sabaya aliwaagiza walinzi wake kumtoa lockup Msangi kwa kumpiga kipigo kizito. Alipigwa makofi ya masikioni na usoni na kichwani alilia sana kwa sauti kwa kusema Mheshimiwa Sabaya, anampiga kwa kosa gani na waliendelea kumpiga hata alipoanguka chini walimsimamisha tena na kuendelea kumtembezea kipigo.

Kabla ya kupigwa Sabaya aliwaagiza walizi wake kumsachi Msangi na walimchukulia waleti na simu yake, lakini alirukia kwenye mguu wa Sabaya huku akimwomba msamaha akimueleza kwamba mke na mtoto wake ni wagonjwa.

“Lakini aliagiza walinzi wamtoe na waendelee kumpiga sehemu za usoni na kichwani na Msangi alipiga sana kelele kutokana na kipigo alichopigwa.”

“Bakari Msangi alilia kwa kusema Meya wa Manispaa na Moshi (Juma Raibu) mdogo wangu ni rafiki yako.
Shahidi alidai kipigo kilitendeka kwa zaidi ya nusu saa.

Alidai pia Sabaya alikuwa ameshika bastola nyeusi aliyokuwa akipokeza na walinzi wake kuwatishia na walikuwa wamebeba ‘radio call’ ambayo waliitumia kuwasiliana na watu wengine waliokuwa nje ya duka.

“Siku hiyo nilikuwa nimefunga niliomba maji, lakini walininyima kwa kuwa mimi ni mtu wa ibada nilitabasamu nikiwa nimekaa chini kufikiria kile kilichotea na mmoja wa walinzi wa Sabaya alisema Mheshimiwa huyu anacheka inaonekana anaona kuwa jambo hili siyo la muhimu,” alidai shahidi.

Alisema mtu aliyezungumza maneno hayo alikuwa mnene wa wastani na mrefu wa saizi ya kati, ana rangi ya maji ya kunde.

Shahidi alidai kuchukuliwa na kuingizwa kwenye chumba ya kuhifadhia majora ya vitambaa na na Sabaya aliagiza apigwe ili atolewe ngewe.

Pia, alidai kuwaambia walinzi wake waendelee kumpiga kwa kuwa kipigo hakikutosha, pia alimwaniambia nimwite kwa jina la General More Power, nilitekeleza alichotaka nilimwambia hii ni dunia leo kwangu kesho kwako.