Shahidi aeleza Sabaya, wenzake walivyovamia duka, kuchukua pesa

22Jul 2021
Allan lsack
Arusha
Nipashe
Shahidi aeleza Sabaya, wenzake walivyovamia duka, kuchukua pesa

SHAHIDI wa pili wa upande wa Jamhuri, Numan Jasini (17), katika kesi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, leo alipanda kizimbani kukamilisha ushahidi wake.

Julai 20, mwaka huu, shahidi huyo alishindwa kufika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Arusha ambako kesi hiyo inaendelea kunguruma, kutokana na sababu za kiimani kwa kuwa ilikuwa sikukuu ya Eid el Haji.

Katika kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi Odira Amworo, Sabaya (34) na wenzake wawili, Sylvester Nyegu (26) na Daniel Mbura (38), wanakabiliwa na mashtaka matatu ya unyang’anyi wa kutumia silaha.

Wakili Mkuu wa Serikali, Tumaini Kweka, alimhoji shahidi huyo kama ifuatavyo;-

Swali: Baada ya mabaunsa wa Sabaya kumweka chini ya ulinzi na kumsachi Bakari Msangi nini kiliendelea?

Jibu: Wakati wakimpiga Bakari Msangi, Sabaya alikuwa anamwambia kwamba amekwenda kuwasaidia magaidi wenzake na Bakari alikuwa anapiga kelele kuomba mshamaha lakini waliendelea kumpiga. Aliwaambia walinzi wake wampige kipigo kizito sana na Bakari aliishiwa nguvu na kulala chini.

Swali: Nini kilichosababisha alale chini?

Jibu: Baada ya kipigo aliishiwa nguvu na Sabaya aliagiza wamsimamishe na kumkalisha.

Swali: Nini kiliendelea baada ya kumkalisha?

Jibu: Sabaya alitoa silaha aina ya bastola na kumnyooshea huku akimwambia atammaliza kwa kuwa ana kiherehere sana na Bakari aliomba wasimuue kwa sababu mke wake na mtoto ni wagonjwa sana.

Baada ya hapo, Sabaya aliwaagiza walinzi wake kumfungua pingu Bakari kwa kuwa alikuwa amefungwa pingu kama walivyoagizwa. 

Swali: Hebu ieleze mahakama ni wakati gani Bakari alifungwa pingu?

Swali: Wakati akiwa chini ya ulinzi alifungwa pingu na baunsa.

Swali: Ni nani alitoa agizo la kufungwa pingu?

Jibu: Agizo la kufungwa pingu lilitolewa na kiongozi wao ambaye ni Sabaya.

Swali: Baada ya kufunguliwa pingu nini kiliendelea?

Jibu: Bakari aliendelea kuomba msamaha na miongoni wao alisogea karibu na mimi kuniambia nimpigie simu Abuu Mansuri.

Swali: Kwa nini alikwambia umpigie simu Abuu Mansuri?

Jibu: Alisema kuna biashara alifanya naye kwa pamoja na yule dada aliyekwenda kununua bidhaa Februari 8 na 9, mwaka huo.

Swali: Na wakati ukipiga simu huyo dada alikuwa wapi?

Jibu: Alikuwa chini ya ulinzi.

Swali: Na ulipompigia simu Abuu Mansuri alikwambiaje?

Jibu: Alisema hawezi kuja dukani kwa kuwa hajisikii vizuri na muda ulikuwa umekwenda.

Swali: Baada ya majibu hayo nini kiliendelea au kilitokea?

Jibu: Sabaya alichukua simu yangu na kumwambia Abuu Mansuri nakupa dakika tano uwe umefika hapa. Baada ya alikata simu na aliniambia kwamba nimpigie Mohamed Saad, na akifika atatuachia huru kwa kuwa hatuhitaji sisi.

Swali: Baada ya kukwambia umpigie ulimpigia?

Jibu: Nilimpigia hakupatikana na nilimjibu hivyo na Sabaya aliniambia nitafute namna yoyote na nilimwomba atuachie. Alinijibu kwamba mhusika akifika hapo dukani atatuachia huru.

Swali: Baada ya hapo nini kiliendelea?

Jibu: Aliagiza mabaunsa wake waniweke chini ya ulinzi na kunilazimisha niendelee kupiga simu.

Swali: Baada ya kukuweka chini ya ulinzi nini kiliendelea?

Jibu: Aliniambia nimpigie tena simu Mohamed Saad, nilipiga simu lakini haikupatikana, hivyo aliniambia nimpige tena Abuu Mansouri.

Swali: Baada ya kukwambia umpigie simu nini kiliendelea?

Jibu: Mjomba wangu Hajirini Saada alisema yeye atampiga simu Abuu Mansuri.

Swali: Wakati huo Hajirini Saada yeye alikuwa wapi?

Jibu: Tulikuwa naye chini ya ulinzi hapo dukani.

Swali: Je, baada ya Hajini kusema atapiga simu nini kiliendelea?

Jibu: Alipiga simu na baada ya muda Abuu Mansuri alifika dukani.

Swali: Alipofika nini kiliendelea?

Jibu: Alifunguliwa mlango na kuingia na baada ya hapo walimweka chini ya ulinzi na kumsachi.

Swali: Umesema kwamba Msangi alishikiwa silala. Baada ya hapo nini kilitokea?

Swali: Mmoja wa walinzi walichukua silaha hiyo na kututishia na kutushachi.

Swali: Kwa hiyo unataka kuieleza mahakama kwamba silaha ilihama kutoka kwa Sabaya na kwenda kwa mlinzi wake?
Jibu: Ndio. Baada ya hapo waliendelea kumhoji Abuu Mansuri.

Swali: Sabaya alimwambiaje Abuu Mansuri?

Jibu: Sabaya alimwambia Abu Mansuri huyu dada unamfahamu na Februari 8 ulikwenda naye wapi? Alimwambia kwamba alimsindikiza benki kubadilisha fedha. 

Swali: Je, Sabaya alimjuaje Abuu Mansuri?

Swali: Mmoja wa walinzi wake walikuwa na faili lenye picha ambayo inamwonyesha huyo dada akiwa amefuatana na Abuu Mansuri.

Swali: Baada ya kumhoji kwa muda Abuu Mansuri nini kiliendelea?

Jibu: Sabaya ambaye ndio kiongozi aliwaagiza walinzi wake kumpiga ili kumtoa ‘lock’ Abuu Mansuri. 

Swali: Katika ushahidi wako huko awali ulisema kuna mtu anaitwa General huyu ndio alisema Abuu Mansuri apigwe na huyu General ni nani?

Jibu: Ndio, General (Sabaya) ndiye alitoa agizo hilo na baada ya hapo aliagiza Abuu kupigwa kipigo kizito na walipomaliza aliagiza afungwe pingu moja na Bakari Msangi na walinzi hawakufahamu namna ya kuwafunga na kiongozi wao akawa anawaelekeza kufunga.

Swali: Baada ya kuwaelekeza namna ya kufunga pingu?

Jibu: Sabaya alitoka na baadhi ya walinzi wake walifunga mlango na wengine walibaki ndani dukani wakiendelea kupekua duka.

Swali: Wakati huo Bakari Msangi na Abuu Mansuri walikuwa wapi?

Jibu: Tulikuwa nao ndani wakiwa wamefungwa pingu na waliwekwa mbele yetu.

Swali: Baada ya kiongozi wao kutaka na kurudishia duka nini kiliendelea?

Jibu: Aliporejea alianza kuwaachia watu waliowekwa chini ya ulinzi akiwamo Ali, Mzee Salimu, Abuu Mansuri, Bakari Msangi. 

Swali: Hebu isaidie mahakama katika ushahidi wako. Umesema Sabaya aliagiza Bakari na Mansuri nini kiliendelea baada ya kufungwa pingu moja?

Jibu: Baada ya muda General Sabaya, aliporejea aliagiza wafunguliwe pingu waliokuwa wamefungwa mikononi.

Swali: Baada ya watu kuruhusiwa kuondoka nini kiliendelea dukani kwenu?

Jibu: Sabaya aliendelea kunihoji mimi na mjomba wangu Hajirini Saad huku wakiendelea kupekuwa na kuchukua  nyaraka na mashine za kielektroniki EFD na kuchukua baadhi ya simu ambazo walizichukua kwa watu waliowapekua.

Pia waliendelea kupekua kaunta lakini sikuona walichochukua kwa kuwa nilipokuwa nimekaa ingekuwa vigumu kuwaona niliona walichukua simu na nyaraka zilizokua juu ya meza.

Swali: Hapo kaunta walipokuwa wanasachi mnawekaga nini?

Jibu: Kuna masanduku mawili moja la kuweka fedha za mauzo na lingine nyaraka.

Swali: Je, moja ya masaduku hayo siku hiyo yalikuwa na kiasi gani cha fedha?

Jibu: Sanduku la kuhifadhia fedha siku hiyo lilikuwa na Sh. 2,769,000

Swali: Je, ulijuaje kuna kiasi hicho cha fedha?

Jibu: Tayari nilikuwa nimeshafanya hesabu na kufahamu kiasi cha pesa kilichokuwapo kwenye sanduku.

Swali: Je, uliiambia mahakama baada ya hapo  mmliambiwa mfunge duka ilikuwaje?

Jibu: Tulifunga duka tukisimamiwa na walinzi wa kiongozi huyo na tulipotoka nje tulimuona sehemu akiwa anaangalia dagaa. Mjomba wangu Hajirini akamwomba Sabaya amnunulie ndizi mbivu kwa kuwa alikuwa amefunga na alitununulia ndizi mbili moja yangu na nyingine ya mjomba wangu. Baada ya hapo walinzi walitusimamia tukapanda kwenye gari.

Swali: Je, mlipandishwa kwenye gari wewe na nani?

Jibu: Tulipanda kwenye gari mimi na Hajirini tukiwa na  Sabaya na walinzi wake watatu,  mmoja akiwa kwenye gari upande wa dereva na wengine walikaa nyuma.

Swali: Baada ya kuingia kwenye gari nini kiliendelea?

Jibu: Msafara wa magari matatu ulitoka tukaanza kuzungushwa  mitaa ya Soko Kuu na Bondeni kisha wakatupeleka hadi karibu na jengo la nyumba yetu.

Swali: Baada ya kufika nyumbani kwenu nini kiliendelea?

Jibu: Alishuka mmoja wa walinzi wakaanza kuulizia geti la kuingilia kwetu.

Swali: Baada ya kuulizia nini kilitokea?

Jibi: Mmoja wa walinzi walinipatia simu yangu wakaniambia nipige simu nyumbani wafungue mlango.

Swali: Baada ya kuambiwa hivyo ulifanya nini?

Jibu: Nilimpigia mama yangu kumwambia asifungue mlango na wakati huo Sabaya alikuwa nje ya geti letu.

Swali: Wakati unaletewa simu kuambiwa upige kule kwenye gari ulikuwa na nani?

Jibu: Nilikuwa mimi mjomba wangu na walinzi watatu wa Sabaya.

Swali: Upo katikati ya walinzi watatu ukaambiwa upige simu ulipata wapi ujasiri wa kuzungumza hayo?

Jibu: Nilizungumza kwa lugha ya kiarabu hivyo hawakuelewa nimemwambiaje. Baada ya kuzungumza  hayo niliwaeleza kwamba simu ya mama yangu haipatikani kwa mmoja wa walinzi. Tuliondoka na msafara wa magari matatu kuelekea Kituo Kikuu cha Polisi cha Arusha.

Swali: Baada ya kuingia kituo cha polisi nini kiliendelea?

Jibu: Kiongozi huyo alishuka kwenye gari na kuzungumza na askari na baadaye tuliandika maelezo. Tulipomaliza tuliambiwa tumeachiwa kwa dhamana na siku ya Februari 10. Tulitakiwa kuripoti kituoni majira ya saa 10:00 jioni tukiwa na Mohamed Saad.

Swali: Baada ya kupatiwa dhamana nini kiliendelea?

Jibu: Tulipewa simu zetu mimi na Hajirini Saad na askari aliyechukua maelezo yetu alitupa lifti ya kutubeba kwa kutumia gari lake mpaka nyumbani kwetu.

Swali: Kwa kusaidia mahakama wakati mnaambiwa mfunge duka ilikuwa majira gani?

Jibu: Nakumbuka giza lilikuwa limeshaanza kuingia na sikumbuki ilikuwa saa ngapi.

Swali: Hawa watu ambao walikuja dukani kwenu ukiona utawatambua?

Jibu: Ndio nitawatambua watu hao kwa kwa kuziangalia sura zao na miili yao.

Swali: Pale waliposimama askari magereza pembeni yao, kuna watu watatu wamekaa. Je, umeshawahi kuwaona popote au unawafahamu?

Jibu: Watu hawa watatu ndio walikuja dukani kuvamia Februari 9.

Swali: Kuna watu uliwatambua waliofika dukani?

Jibu: Wa kwanza ni Ole Sabaya alikuwa kiongozi wao akitoa maagizo yote. Wa pili ni Sylvester alinikabidhi simu yangu kuwaambia watu wa nyumbani wafungue mlango na watatu ni Daniel tulipanda naye gari moja.

Swali: Je, mtu wa kwanza na wapili pale dukani uliweza kuwatambua?

Jibu: Kwa pale dukani sikuweza kumtambua mtu wa kwanza wa pili na watatu kutokana na vurugu zilizotokea hapo dukani. Lakini nilipotoka nao nje ya duka niliwatambua vizuri wote.

Swali: Na mliporejeshwa nyumbani nini kilitokea?

Jibu: Ferbuari 10 majira ya saa 10:00 nilipokea simu kutoka kwa Bakari Msangi. Anieleza kwamba natakiwa kwenda kituo cha polisi kuandika maelezo kutokana na tukio lililotokea Februari 9 na baadaye nilimwambia baba yangu akanisindikiza kwenda kituoni. Nilimkuta askari anayeitwa Onuku aliandika maelezo.

Swali: Je, baada ya kuandika hapo nini kilitokea?

Jibu: Kutokana na kutokea kwa jambo hilo, tulikwenda kuomba kibali polisi cha kufungua duka. Baada ya hapo Februari 12, Ali Saad, mimi kwa pamoja na askari polisi (Onuku), tulifungua duka.

Swali: Hebu ieleze Mahakama baada ya kifungua duka mlikuta katika hali gani?

Jibu: Tulikuta vitu vimevurugika yakiwamo makapeti na pembeni ya kaunta kulikuwa na damu.

Swali: Kwa upande wa kaunta na vitu mlivyoviacha ilikuwaje?

Jibu: Tulipoangali baadhi ya nyaraka na fedha za mauzo Sh. 2,769,000 hatukuzikuta kwenye sanduku la kuwekea hela.
Swali: Baada ya kwenda polisi nini kilifuata?

Jibu: Baada ya polisi kufanya upelelezi wao Februari 12, kwa kuwa muda ulikuwa umekwenda, Februari 13 tuliruhusiwa kufungua duka kuendelea na biashara.

Swali: Baada ya kufungua nini kilichofuata nini kilitokea?

Jibu: Nilijaribu kumpigia mjomba wangu Mohamed Saad sikumpata kwenye simu. Lakini Februari 17 alinipigia mwenyewe na nilimweleza kiasi hicho cha fedha kilichoibiwa.

Habari Kubwa