Shahidi afunguka kuwakamata walinzi wa Mbowe

25Jan 2022
Kulwa Mzee
Dar es Salaam
Nipashe
Shahidi afunguka kuwakamata walinzi wa Mbowe

SHAHIDI wa 11, Koplo Goodluck Minja amedai kuwakamata walinzi wa Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, kwa tuhuma za ugaidi haikuwa kumdhoofisha kisiasa wakati wa uchaguzi mkuu 2020.

Hayo yalidaiwa jana Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu mbele ya Jaji Joachim Tiganga wakati akihojiwa na Wakili wa Utetezi, Dickson Matata.

Matata alimuhoji akitaka kujua kama aliwahi kusikia Tundu Lissu kapigwa risasi 16 na kwamba alipigwa akiwa kwenye shughuli za Bunge.

Shahidi anadai aliwahi kusikia taarifa za Lissu kupigwa risasi Dodoma lakini hakuwahi kufuatilia.

Anadai hafahamu kati ya tukio la Lissu kupigwa risasi na tukio la kuwakamata watuhumiwa wa ugaidi Rau Madukani, Moshi kipi kilianza.

Shahidi anadai anafahamu kuwa Mbowe na Lissu ni viongozi wa CHADEMA na kwamba suala la Kiongozi kuwa na ulinzi wa mtu binafsi akiamua anakuwa naye.

Akihojiwa kuhusu suala la kuwakamata walinzi wa Mbowe haikuwa kumdhoofisha Mbowe wakati wa Uchaguzi 2020, alidai haikuwa na lengo la kumdhoofisha katika uchaguzi.

Koplo Goodluck anadai hafahamu Mbowe alikuwa mbunge wa wapi, lakini anafahamu alikuwa mbunge.

Akihojiwa na Wakili Peter Kibatala kuhusu mshtakiwa Adamu Kasekwa maarufu Adamoo alidai hakuna mahali ambapo alijitambulisha Adamoo na hakusikia kama alijitambulisha hivyo.

Anadai walipofika Dar es Salaam Agosti 7, mwaka 2020, wakiwa na mshtakiwa Kasekwa na Mohammed Ling'wenya alikwenda kunawa uso akiwa na vielelezo alivyowakamata navyo zikiwamo simu na bastola.

Anadai alikabidhi kwa Afande Nuru Agosti 7, mwaka 2020, lakini hakusema mahakamani kama risasi zilitolewa katika magazine wakahesabu.

Shahidi anadai mshtakiwa waliyemtafuta bila mafanikio Moshi, Moses alikuwa mwanajeshi lakini hakueleza mahakamani chochote kuhusu kushirikiana na jeshi liweze kusaidia.

Anadai hakueleza pia kuhusu kushirikiana na Interpol ili kumkamata mshtakiwa huyo.

Koplo Goodluck anadai anafahamu shahidi huru hatakiwi kuwa mtu mwenye uhusiano na mtuhumiwa kwa namna yoyote, lakini alikana kuwa shahidi huru waliyemtoa kwenye grosari waliyokamatwa washtakiwa alipishana kauli na Adamoo.

Anadai hakuwahi kusikia kutoka kwa Afande Kingai, Mahita wala Jumanne kuitwa viongozi wa Serikali ya Mtaa katika tukio la kuwakamata watuhumiwa Rau Madukani.

Shahidi anadai hakumwambia Jaji kwanini hakukabidhi vielelezo kwa Afande Nuru saa 12 kasoro alfajiri Agosti 7, mwaka 2020, baada ya kufika na watuhumiwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam wakitokea Moshi.

"Simu za mshtakiwa Halfani Bwire zilichukuliwa na ACP Ramadhan Kingai, nilipewa nishike lakini si kwa makabidhiano.

"Nilizishika kutoka Polisi Chang'ombe hadi Kituo Kikuu cha Polisi, nikiwa njiani sikuwa na mashahidi huru wala mshtakiwa Bwire," anadai shahidi wakati akijibu maswali.

Shahidi anadai Agosti 4, mwaka 2020, ndipo alipisikia kulikuwa na njama za kumdhuru Lengai Ole Sabaya, lakini kabla ya hapo hajawahi kusikia.

Pia anadai kama mpelelezi hajawahi kusikia njama za kuchoma kituo cha mafuta Arusha.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mbowe, Bwire, Kasekwa na Ling'wenya ambao wanashtakiwa kwa kula njama, kufanya vitendo vya kigaidi kati ya Mei mosi na Agosti 5, mwaka 2020.

Habari Kubwa