Shahidi amaliza ushahidi kesi ya Sabaya

29Jul 2021
Allan lsack
Arusha
Nipashe
Shahidi amaliza ushahidi kesi ya Sabaya

SHAHIDI wa sita wa Jamhuri, Bakari Msangi (38), amekamilisha ushahidi wake mahakamani  huku akidai aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, alifanya uhalifu wa kuteka nyara watu, kupiga, kutesa, kutishia kuua kwa silaha na kupora baadhi ya vitu na fedha, vitendo ambavyo si vya ...

kibinadamu na kiungwana.

Shahidi huyo ambaye ni Diwani wa Kata ya Sombetini, jijini Arusha, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), alitoa madai hayo jana mahakamani mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Odira Amworo.

Mbali na Ole Sabaya (340, washtakiwa wenzake ni Sylvester Nyegu (26) na Daniel Mbura (38). Wote wanakabiliwa mashtaka matatu ya unyang'anyi wa kutumia silaha.

"Uhalifu wa kupigwa, kunyanyaswa, kuteswa, kutishiwa kuuawa, kutishiwa silaha, kuwekwa chini ya ulinzi na kulazwa kifudifudi siyo mambo mazuri ya kutendewa au kufanyiwa binadamu," alidai shahidi huyo.

Akihojiwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka, alidai kuwa baada ya uhalifu huo Februari 16, mwaka huu, alikwenda Kituo kikuu cha Polisi Arusha kuandikisha maelezo ya vitendo vya uhalifu alivyofanyiwa na Sabaya.

"Nilifika kituoni nilipokelewa na askari wakiwa kama tisa na kupelekwa katika eneo la wazi ambalo kulikuwa na watu wengi ambao ni wanaume wamesimama kwenye mstari wakiwa wameangalia chini na mmoja wa askari ambaye ni kiongozi wao, aliniambia kuwa wanachokifanya ni gwaride la utambulisho la kumtambua mtu aliyenitendea uhalifu siku ya Februari 9, mwaka huu.

"Aliniambia watu tisa waliokuwa mbele yangu natakiwa kupita mbele au nyuma yao halafu nikimtambua mtu nimshike bega  na baada ya kuwatazama watu hao nilifanikiwa kumtambua Deogratius Peter. Nilipomtambua, mmoja wa askari alitoa agizo mimi kutolewa nje ya geti na aliniambia kwamba wataniita tena.

"Kiongozi huyo wakati tunakwenda katika gwaride la utambuzi aliniambia kuwa watu hao ambao natakiwa kwenda kuwatambua wanatuhumiwa kuhusika na tukio la uhalifu la Februari 9, mwaka huu, katika duka la Mohamed Saad."

Bakari Msangi, alidai baada ya kutolea nje ya geti baada ya dakika 20 kupita, aliitwa tena akiwa ameambatana na askari aliokuwa nao nje ya geti na kiongozi wa askari hao alimweleza kwamba anatakiwa kuwatambua watu wengine ambao wanatuhumiwa kutenda uhalifu.

"Awamu ya pili katika gwaride la utambuzi walikuwa watu 11 waliosimama kwenye mistari niliwazunguka nyuma na mbele yao nilimfahamu mtu mmoja anaitwa Daniel Mbura na nilimshika bega na baada ya hapo niliambiwa niende katika Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya kwa ajili ya kujaza baadhi ya fomu na kuchukuliwa maelezo.

"Watu hawa nilifanikiwa kuwatambuwa katika gwaride la utambuzi kwa kuwa ndio walikuwa karibu yangu pale dukani kwa Mohamed Saad Hajirini wakati wakitenda uhalifu wa kuvamia, kupiga, kutesa, kunyanyasa na kuwaweka watu chini ya ulinzi, hivyo ilikuwa rahisi sana kwa mimi kuwafahamu.

"Baada ya kuwatambua nilimalizia kuandika maelezo ya ziada na nilipomaliza waliniambia naweza kuondoka na endapo polisi wakinihitaji tena watanijulisha ili kufika kituoni hapo," alidai.

Hata hivyo, shahidi huyo,  alimtambua mshtakiwa wa tatu Daniel Mbura, kwa kumshika bega mahakamani, akidai kuwa siku ya gwaride la utambuzi awamu ya pili kituo cha polisi pia alimtambua mshtakiwa huyo kwa kuwa alikuwa mmoja wa watu waliokuwa katika tukio la kufanya uhalifu.

Msangi, baada ya kukamilisha kutoa ushahidi wake, alihojiwa na wakili wa utetezi, Moses Mahuna, kwa kumuuliza kama mmiliki wa duka, Mohamed Saad, alimweleza Sabaya yuko dukani kwake anapiga watu na shahidi huyo aliithibitishia mahakama kuwa alipewa taarifa hiyo.

Wakili huyo pia alimhoji shahidi huyo akiwa diwani mzoefu alipaswa kuchukua hatua gani baada ya kuona tukio hilo na kudai kuwa hakwenda dukani huko kama diwani bali kama rafiki na ndugu wa mmiliki wa duka na cheo chake alikiacha nje ya duka.

Kuhusu kwa nini hakushirikisha viongozi wa kata na mtaa wa eneo hilo, alidai kuwa alikwenda dukani kuwasaidia rafiki na ndugu zake na hakwenda kama diwani.

Pia Wakili alimhoji shahidi huyo kwa nini alivamia eneo ambalo hakupaswa kuwepo na kujibu kwamba hakuvamia bali alifungua mlango alioagizwa na mmiliki wa duka kwenda kuangalia watu waliokuwa dukani.

Wakili pia alimhoji shahidi kwa kumuuliza ni kweli kwamba lengo la Sabaya kwenda dukani ilikuwa kwa ajili kumpata mmiliki wa duka ambaye anatuhumiwa kufanya biashara haramu.

Katika swali hilo, shahidi alijibu kwamba Sabaya alimweleza kuwa alikwenda kwenye duka hilo kwa kuwa aligizwa na Hayati Rais Dk. John Magufuli kwa kuwa watu hao wanafanyabiashara ya kuhujumu uchumi.