Shahidi kesi ya Mbowe afunguka

21Sep 2021
Kulwa Mzee
DAR ES SALAAM
Nipashe
Shahidi kesi ya Mbowe afunguka

INSPEKTA Mahita Omari ameieleza mahakama kuwa madai kwamba mshtakiwa, Adamu Kasekwa alifungwa jaketi usoni kuanzia Moshi hadi Dar es Salaam, siyo kweli kwa kuwa hakuruhusiwa kufanya hivyo.

Shahidi huyo wa pili wa kesi ndogo katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake watatu alitoa ushahidi huo jana Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi mbele ya Jaji Mustapha Siyani.

Akihojiwa na Wakili wa Utetezi, Peter Kibatala, kuhusu madai kwamba mshtakiwa wa pili, Kasekwa aliteswa kabla na wakati anachukuliwa maelezo, Mahita alidai hawaruhusiwi kufanya hivyo.

Wakili Kibatala alihoji kama wanapokuwa katika mahojiano wanaruhusiwa kuwa na bisibisi kumtisha mtuhumiwa atoe maelezo.

Pia, Kibatala alidai kuna taarifa pia mshtakiwa alichomwachomwa na bisibisi huku akiambiwa kama hatatoa maelezo wanayotaka wao watamfanyia walichofanya wakiwa Moshi.

Inspekta Mahita alidai hayo yote hayaruhusiwi kufanyiwa mtuhumiwa na kwamba katika ukamataji walipata ushirikiano kutoka kwa washtakiwa.

Wakili Kibatala alihoji kama Polisi wanaruhusiwa kumfunga pingu mtuhumiwa mikononi na miguuni kisha kumning'iniza kama mshkaki huku wakimpiga kwenye nyayo.

Shahidi alihojiwa kama wanaruhusiwa kumfunga jaketi mtuhumiwa kutoka Moshi hadi Dar es Salaam.

Inspekta Mahita alikanusha tuhuma hizo na kudai kwamba hakukuwa na haja ya kumfunga jaketi, hawakumtesa kwani hawaruhusiwi.

Akihojiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Pius Hillar, kuhusiana na ushahidi wake, aliendelea kusikiliza kwamba polisi hawaruhisiwi kumtesa mtuhumiwa.

Alidai Moshi waliishi katika mazingira mazuri na washtakiwa, waliwapa ushirikiano hadi wanafika nao Dar es Salaam.

Shahidi wa pili alimaliza kutoa ushahidi aliingia shahidi wa tatu, Koplo Msemwa ambaye alidai Agosti 7, mwaka jana alikuwa zamu Kituo cha Polisi cha Kati Dar es Salaam, alikuwa na jukumu la kutunza mahabusu.

Anadai alikabidhiwa mahabusu saa kumi na mbili kasoro asubuhi, alienda kuwahakiki kama idadi aliyokabidhiwa ndio hiyo na akiwa huko alimwona Kamishna Msaidizi wa Polisi, Ramadhan Kingai akiingia akiwa na ASP Jumanne na watuhumiwa wawili.

Msemwa akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga, anadai ACP Kingai alikuwa na askari wengine waliovaa kiraia wakiwa wameshika bunduki na watuhumiwa walikuwa na pingu mikononi, alipewa namba ya jalada akaona ni kesi ya kula njama kufanya vitendo vya kigaidi.