Shahidi muhimu kesi ya Mdee bado kuhojiwa

12Jul 2018
Hellen Mwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Shahidi muhimu kesi ya Mdee bado kuhojiwa

SHAHIDI wa Jamhuri katika kesi ya madai ya kumtusi Rais John Magufuli, Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Ilala, Davis Msangi, amedai mahakamani hajawahi kumhoji rais huyo kuhusu maneno aliyotamka Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, kwamba “afungwe breki anaongea ovyo ovyo”.

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee.

 

Kadhalika alidai kuwa hakuwahi kumhoji Rais Magufuli alivyojisikia baada ya Mdee kutamka maneno hayo.

Msangi alitoa madai hayo jana wakati akihojiwa na Wakili wa Utetezi, Peter Kibatala, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba anayesikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Mdee anadaiwa kuwa Julai 3, mwaka jana, katika Makao Makuu ya Ofisi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mtaa wa Ufipa, Kinondoni, alitamka maneno kwamba Rais Magufuli “anaongea ovyo ovyo, anatakiwa  afungwe breki”  kitendo ambacho kingeweza  kusababisha uvunjifu wa amani.

Shahidi alidai kuwa anamfahamu Rais na ni mkazi wa Ikulu jijini Dar es Salaam.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya Wakili Kibatala na Shahidi:

Wakili: Shahidi, umewahi kwenda kumhoji Magufuli?

Shahidi: Hapana sijawahi.

Wakili: Umewahi kwenda kumhoji kama maneno aliyotamka Mdee yanamkera au anayafurahia?

Shahidi: Hapana sijawahi kumhoji.

Wakili: Nani aliandika maelezo ya Mdee alipokua polisi?

Shahidi: Aliandika maelezo chini ya koplo Hassan.

Upande wa utetezi ulidai hauna mahojiano zaidi dhidi ya shahidi.

Wakili wa Serikali Mwandamizi,  Patrick Mwita, alidai kuwa anaomba tarehe nyingine ya kuendelea na shahidi wa Jamhuri.

Hakimu alisema kesi hiyo itaendelea kusikilizwa Agosti 7 na 9, mwaka huu.

Mapema Juni 29, mwaka huu, Msangi alitoa ushahidi wake na kudai maneno aliyotamka  Mdee ni ya jinai kupitia mtandao wa kijamii wa Youtube.

 

Habari Kubwa