Shahidi: Wasaidizi wa Sabaya walidai ni maofisa wa TISS

30Nov 2021
Allan Isack
Arusha
Nipashe
Shahidi: Wasaidizi wa Sabaya walidai ni maofisa wa TISS

MFANYABIASHARA Francis Mroso (44), amedai alitoa Sh. milioni 90 ili kuokoa maisha yake kwa kuwa vijana waliokuwa wameambatana na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya, walijitambulisha kuwa ni maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS).

Shahidi huyo pia amedai mahakamani kwamba baadhi ya vijana hao walijitambulisha ni maofisa kutoka Mamlaka ya Mapato (TRA) na wanahusika na ukusanyaji wa kodi.

Vilevile, shahidi huyo amedai kwamba Sabaya na vijana wake, walimtishia kwamba wangempoteza endapo angeshindwa kutoa kiasi hicho cha fedha.

Shahidi huyo wa 10 katika kesi ya uhujumu uchumi namba 27, alitoa madai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, Patricia Kisinda, wakati akiendelea kutoa ushahidi wake.

Shahidi huyo alidai Sabaya alimwambia asipotoa fedha hizo, watampoteza, hivyo aliingiwa na hofu ya kupotezwa na kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi ambayo haina dhamana.

Katika kesi hiyo, mbali na Sabaya washtakiwa wengine, katika shauri hilo ni Silvester Nyegu (26), Enock Togolani (41), Watson Mwahomange (27), John Odemba, Jackson Macha (29) na Nathan Msuya (31).

Akihojiwa na Wakili wa Utetezi, Mosses Mahuna, shahidi huyo alidai kwamba kampuni yake ya Mrosso Injector Pump Services imeanza kufanya kazi mwaka 2015.

Shahidi huyo alidai biashara yake imesajiliwa na kuendeshwa kwa kufuata kanuni, sheria na taratibu zote za nchi.

Shahidi huyo alidai kwamba ni utaratibu wake kutoa risiti za kielektroniki wakati anapomaliza kutoa huduma katika biashara hiyo.

Alidai kuwa katika biashara yake hiyo, hajawahi hata siku moja kukwepa kulipa kodi ya serikali wala hajawahi kutoa rushwa.

Alidai katika uendeshaji wa biashara yake, aliwahi kutoa rushwa kwa kulazimishwa kutoa fedha na Sabaya.

"Hapana mimi siyo mtoa rushwa kwa kuwa sikutoa kwa hiari yangu kwa kuwa nililazimishwa kutoa rushwa," alidai shahidi.
Akizungumza mahakamani huko, shahidi huyo alidai kwamba alitishiwa kwamba asipotoa fedha hizo atafunguliwa kesi ya uhujumu uchumi na atapotezwa.

"Vijana wa Sabaya waliniambia kwamba Sabaya, amepewa wadhifa wa kuwa kiongozi wa kikosi kazi maalumu cha kuwakamata watu wanaouhujumu uchumi kwa kanda ya kaskazini na kuwafungulia kesi na kazi ya kushughulika na wakwepaji wa kodi, aliteuliwa kutekeleza jukumu hilo na aliyekuwa Rais Hayati Dk. John Magufuli," alidai.

Shahidi huyo alidai kwamba alitoa fedha hizo kwa kuwa aliyemtishia maisha ni kiongozi ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na ni mteule wa Rais, hivyo alipata hofu.

Alidai kwamba akiwa na watu hao ambao walijitambulisha kuwa maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa, alitoa fedha ili kuokoa maisha yake kwa kutokupotezwa.

"Sikuweza kutoa taarifa polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kuwa nilizuiwa kuzungumza na simu kwa wakati huo," alidai shahidi huyo.

Mroso alidai mahakamani huko kwamba akiwa katika Benki ya CRDB Tawi la Kwa Murombo jijini Arusha, alishindwa kumweleza meneja na watoaji wa huduma wa benki kwa kuwa alikuwa chini ya ulinzi wa vijana wa Sabaya.

"Nilishindwa kupiga kelele kuomba msaada kuwa natishiwa maisha na kulazimishwa kutoa hela kwa kuwa vijana wale walijitambulisha kwangu ni maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa, hivyo nilishindwa kufanya chochote, nilidhani watakuwa ni askari," alidai shahidi huyo.

Alidai kwamba vijana waliokuwa wameambatana naye hadi benki, mmoja ndio alimtambua kwa jina la Watson Mwahomange lakini wengine hakuwatambua kwa majina bali kwa mwonekano wao.

"Wakati tukielekea nyumbani kwangu, Sabaya aliniambia nitoe kiwango hicho cha fedha, vinginevyo wangeondoka na mimi," alidai shahidi huyo.

Alidai kuwa akiwa benki, aliulizwa na mhasibu wa benki hiyo kwamba anatoa kiasi hicho cha fedha alithibitisha kwamba ni kweli kwa kuwa kuna mtu anataka kumlipa.

"Siyo wajibu wa maofisa wa benki hiyo kufahamu, kuuliza, kutaka na kujua kwamba fedha ninatoa benki kwa kazi gani," alidai shahidi.

Habari Kubwa