Shamhuna, Ngwilizi wafariki dunia

21May 2019
Romana Mallya
DAR
Nipashe
Shamhuna, Ngwilizi wafariki dunia

WANASIASA wakongwe nchini, Ali Juma Shamhuna na Brigedia Jenerali mstaafu Hassan Ngwilizi, wamefariki dunia.

Taarifa zilizopatikana jana zilieleza kuwa Ngwilizi alifariki dunia jana katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo, Dar es Salaam, wakati Shamhuna alifariki dunia juzi visiwani Zanzibar.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, alitangaza jana kuwa Ngwilizi, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, alifariki dunia jana katika Hospitali Kuu ya Jeshi ya Lugalo alikokuwa akipatiwa matibabu.

Katika uhai wake, Ngwilizi alitumikia Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kuanzia mwaka 1968 hadi 1993 katika nafasi mbalimbali hadi Brigedia Jenerali.

Pia aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, Mbunge wa Kuteuliwa na baadaye Mbunge wa Mlalo, Lushoto mkoani Tanga kwa miaka 10 kuanzia mwaka 2005 hadi 2015.

Ndani ya Bunge aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Maraka ya Bunge na pia Mwenyekiti wa Kamati ndogo ya Bunge iliyoundwa Julai 2 mwaka huo kuchunguza kashfa iliyomhusisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini na Nishati, Eliakim Maswi, akiwatuhumu baadhi ya wabunge kula rushwa kutoka kwenye kampuni ya mafuta.

Kwa upande wake, Shamhuna ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri Kiongozi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,  alizikwa jana Donge Kaskazini Unguja na wakati wa uhai wake alishika nyadhifa tofauti ndani ya serikali.

Shamhuna ambaye pia aliwahi kuwa Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Zanzibar  aliwahi kuwa Waziri wa Elimu, Mafunzo ya Amali na Waziri wa Maji, Ardhi, Nyumba na Nishati (Zanzibar).

Mwaka 2010 hadi 2012 alikuwa Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo Zanzibar, mwaka 1981 alikuwa Mwakilishi wa Kwahani mjini Unguja.

Shamhuna alizaliwa Januari 1, mwaka 1944 na alifariki dunia akiwa Fuoni Wilaya ya Magharibi, Unguja.

Habari Kubwa