Shamim Mwasha, mumewe wafikishwa mahakamani

28May 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Shamim Mwasha, mumewe wafikishwa mahakamani

MMILIKI wa blogu ya  8020 Fashion, Shamim Mwasha (41) na mume wake, Abdul Nsembo (45), wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin Hydrochloride zenye uzito wa gramu 232.70.

MMILIKI wa blogu ya  8020 Fashion, Shamim Mwasha akiwa mahakamani.

Wanafamilia hao walisomewa mashtaka yao jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mfawidhi, Kelvin Mhina.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na 
Wakili wa Serikali, Costastine Kakula.

Kakula alidai kuwa washtakiwa hao, wakazi wa Mbezi Beach, wanatuhumiwa kwa shtaka moja la kusafirisha dawa za kulevya.

Alidai kuwa Mei mosi, mwaka huu, eneo la Mbezi Beach, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, washtakiwa wanatuhumiwa kusafirisha dawa hizo  kinyume cha sheria ya uhujumu uchumi.

Kakula alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, aliomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa.

Wakili wa utetezi, Hajra Mungula, aliomba upande wa Jamhuri kukamilisha upelelezi haraka ili hatua nyingine iweze kuendelea licha ya kwamba jana ndiyo siku ya kwanza kwa kesi hiyo kusomwa mahakamani hapo.

Hakimu Mhina alisema shtaka lao ni la uhujumu uchumi, mahakama yake haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, hadi upelelezi utakapokamilika itahamishiwa Mahakama Kuu, kitengo cha uhujumu uchumi yenye mamlaka ya kuisikiliza.
Alisema kesi hiyo itatajwa Mei 27, mwaka huu, na kuangalia kama upelelezi umekamilika au la.

Washtakiwa wanaendelea kukaa mahabusu mpaka siku ya kwenda tena mahakamani.

Habari Kubwa