Shangwe mgawo mabilioni ya IMF sekta ya elimu 

24Oct 2021
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe Jumapili
Shangwe mgawo mabilioni ya IMF sekta ya elimu 

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, ameweka wazi namna zitakavyotumika Sh. bilioni 368.9 za sekta ya elimu kati ya Sh. trilioni 1.3 zilizotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa mapambano dhidi ya UVIKO-19.

Kati ya fedha hizo, wizara hiyo imepata Sh. bilioni 64.9 ambazo zitaelekezwa kwenye maeneo makuu matatu huku akibainisha kuwa wanafunzi wenye Uhitaji maalum vyuo vikuu watanunuliwa bajaj, vishikwambi na vifaa saidizi vingine.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini hapa kuhusu mpango na matumizi ya fedha hizo, Prof. Ndalichako alisema: "Kati ya Sh. bilioni 368.9 kama alivyosema Waziri wa Tamisemi, Sh. bilioni 304 zimepelekwa kwenye mambo mbalimbali ikiwamo kujenga madarasa 15,000 ambapo kati ya hayo, madarasa 12,000 ni kwa ajili ya kupokea wanafunzi ambao watajiunga na kidato cha kwanza mwaka 2022, madarasa 3,000 ni kwa ajili ya kuondoa kadhia ya shule shikizi ambazo zilianzishwa kiholela."

Alifafanua eneo la kwanza ni kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi wenye uhitaji maalum ambapo Sh. bilioni 1.47 zitatumika.

“Serikali imepanga kuchapisha vitabu kwa ajili ya wanafunzi 353 wasioona na wenye uoni hafifu 3,591 wa elimu ya sekondari ambapo Sh. milioni 707 zimetengwa ili kuwa na uwiano wa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja kwa elimu ya sekondari,” alisema.

Alibainisha vitabu vitakavyochapishwa vitajumuisha nakala 93,366 za vitabu vya ziada vya maandishi yaliyokuzwa kwa ajili ya wanafunzi wenye uoni hafifu na nakala za vitabu vya nukta nundu 9,178 kwa ajili ya wasioona kwenye shule za sekondari.

“Pia serikali itawezesha ununuzi wa vifaa saidizi kwa wanafunzi 410 wenye uhitaji maalum walioko katika vyuo vikuu 11 vya serikali ambapo Sh. milioni 770 zimetengwa," alisema.

Waziri huyo alisema vifaa vitakavyonunuliwa kwa ajili ya wanafunzi hao ni bajaj, vishikwambi, kompyuta mpakato na vifaa vingine wezeshi kulingana na mazingira yao.

Alitaja eneo jingine la pili ni kuimarisha elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ambapo kiasi Sh. bilioni 57.9 zitatumika ikiwamo kukamilisha ujenzi na kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwenye vyuo 25 vya ufundi stadi wilaya Sh. bilioni 28.76.

Alisema ukamilishaji wa vyuo utawezesha ongezeko la takriban wanafunzi 30,000.

“Serikali imepanga kukamilisha ujenzi na kuweka samani kwenye vyuo vinne vya VETA vya ngazi za mikoa Njombe, Rukwa, Simiyu na Geita Sh. bilioni 18.7 zimetengwa, vitaongeza nafasi za wanafunzi 5,600,” alisema.

Pia alisema Sh. bilioni 1.04 zitajenga mabweni katika Chuo cha Ualimu wa Ufundi Morogoro, Sh. bilioni 6.8 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na mitambo ya kujifunzia vyuo 34 vya maendeleo ya wananchi na wanachuo 9,804 watanufaika.

“Katika kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji kwa vitendo Chuo cha Ufundi Arusha kitapata Sh. bilioni 2.6 kwa ajili ya kujenga jengo la kitaaluma lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 911 na walimu 81," alisema.

Prof.Ndalichako alisema eneo la tatu linahusisha Sh. bilioni 5.44 zilizotengwa kuimarisha mazingira ya utoaji elimu ya ualimu kwa kujenga madarasa 41, kumbi tatu za mihadhara na mabweni 15.

Waziri huyo aliagiza watendaji wa wizara na taasisi kukamilisha miradi hiyo Mei 30, mwakani, ununuzi wa vifaa vyote uzingatie bei ya soko na matokeo ya utekelezaji wa miradi yaendane na thamani ya fedha zilizotolewa.

“Katibu Mkuu aandae mfumo wa uratibu, usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ili kubaini changamoto na kuchukua hatua stahiki kwa wakati, na kila mwezi taarifa za utekelezaji zitolewe,” aliagiza.

Alionya kuwa fedha hizo sio za kulipana posho ya aina yoyote huku akisisitiza atachukua hatua kwa watakaoongeza bei ya bidhaa zisizoendana na bei ya soko kwenye miradi hiyo.

Habari Kubwa