Shein adokeza ongezeko mishahara

13Jan 2020
Na Waandishi Wetu
Zanzibar
Nipashe
Shein adokeza ongezeko mishahara

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema kutokana na kuongezeka ukusanyaji wa mapato ya serikali, watumishi wasishangae kuongezewa mishahara.

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, akikagua gwaride maalum la Maadhimisho ya Miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar katika Uwanja wa Amaan Zanzibar jana. PICHA: IKULU

Pia amesema ataendelea kushirikiana kikamilifu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli, kuhakikisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unadumu ili nchi iendelee kuwa na amani.

Aliyasema hayo jana visiwani Zanzibar wakati wa sherehe za maadhimisho ya Miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar zilizohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, vyama vya siasa, taasisi na wananchi kutoka Bara na Visiwani.

Hata hivyo, Dk. Shaun hakutoa maelezo zaidi kuhusiana na uwezekano wa watumishi wa umma kuongezwa mshahara.

“Niwahakikishie tu kwamba muungano wetu utaendelea kudumu, mimi na Rais John Magufuli tutaendelea kutekeleza wajibu wetu wa kikatiba na kisheria katika kulinda amani na utulivu wa wananchi pamoja na mali zao na hatutochelea kumchukulia hatua mtu yoyote yule atakayejaribu kuhatarisha amani ya nchi,” alisema Rais Shein.

Miongoni mwa viongozi waliohudhuria ni Rais Magufuli, marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na Amani Abeid Karume pamoja na mawaziri wakuu wastaafu wakiwamo Edward Lowassa, Frederick Sumaye na Mizengo Pinda.

Wengine ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, mawaziri na viongozi wa vyama vya siasa akiwamo Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba.

Katika sherehe hizo, Rais Shein alitaja mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika kipindi cha miaka tisa ya utawala wake katika sekta ya afya, elimu, uchumi na miundombinu.

“Kasi ya ukuaji uchumi iliongezeka kutoka asilimia 4.3 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 7.1 mwaka 2018, pato la taifa limeongezeka kutoka Sh. bilioni 1,768 mwaka 2010 hadi kufikia Sh. bilioni 2,874 mwaka 2018,” alisema Rais Shein.

Alisema lingine ni Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Zanzibar, Dira ya Maendeleo ya mwaka 2020 pamoja na Maendeleo ya Kimataifa.

KUKUA KWA PATO

Rais Shein alisema vilevile, pato la mwananchi nalo limeongezeka kutoka wastani wa Sh. 942,000 sawa na Dola za Marekani 675 mwaka 2010 hadi Sh. milioni 2,323,000 sawa na Dola za Marekani 126,000 mwaka 2018.

MFUMUKO WA BEI

Alisema mfumuko wa bei nao umepungua kutoka asilimia 14.7 mwaka 2011 hadi kufikia asilimia 3.9 mwaka 2018, utekelezaji wa miradi ya maendeleo 304 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 3.42 iliyotengeneza ajira 16,866 hadi mwaka 2018.

SEKTA ELIMU

“Kwenye sekta ya elimu tumefanikiwa kuainisha elimu bure, shule zimeongezeka, idadi ya wanafunzi imeongezeka, hadi mwaka 2019 shule za awali zilikuwa 382 zikiwa na wanafunzi 85,984 ikilinganishwa na mwaka 2010 kulikuwa na shule 238 na wanafunzi 29,782,” alisema Rais Shein.

Alisema shule za msingi zimeongezeka kwamba mwaka 2010 kulikuwa na shule 299 zikiwa na idadi ya wanafunzi 226,812, mwaka 2019 zimeongezeka na kufikia shule 381 zikiwa na wanafunzi 290,510.

Alisema shule za sekondari nazo zimeongezeka, kwamba mwaka 2010 kulikuwa na shule 105 zikiwa na idadi ya wanafunzi 80,208, mwaka 2019 zimefikia shule 284 zikiwa na idadi ya wanafunzi 130,713.

Rais Shein alisema bajeti ya sekta ya afya imeongezeka kutoka Sh. bilioni 10.81 mwaka 2010/11 na kufikia Sh. bilioni 104.24 mwaka 2019/20.

“Idadi ya kusomesha madaktari imeongezeka, kwa sasa daktari mmoja anatibu wagonjwa 6,276 kulinganisha na mwaka 2010 kwamba daktari mmoja alikuwa anatibu wagonjwa 31,838,” alisema Rais Shein.

Alisema serikali ya Zanzibar imejitahidi katika kuongeza mishahara ya watumishi wa umma tangu maka 2010, hali iliyotokana na makusanyo mazuri ya mapato.

Alisema serikali ya Zanzibar imeongeza malipo ya wastaafu kwa mwezi kutoka Sh. 25,000 mwaka 2017 hadi kufikia Sh. 90,000 mwaka 2019.

Imeandaliwa na Rahma Suleiman (Zanzibar) na Gwamaka Alipipi, Dar

Habari Kubwa