Shein ataja siri ya ardhi kwa maendeleo

23Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Zanzibar
Nipashe
Shein ataja siri ya ardhi kwa maendeleo

RAIS wa Zanzibar, Dk.Ali Mohamed Shein, amesema matumizi mazuri ya ardhi na usimamizi bora wa mazingira ni misingi muhimu katika maendeleo ya taifa lolote duniani.

RAIS wa Zanzibar, Dk.Ali Mohamed Shein, picha mtandao

Dk. Shein aliyasema hayo jana katika mkutano wa mwaka wa Jumuiya ya Majaji na Mahakimu wa Nchi za Afika Mashariki unaofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Madinat Al Bahr, Mbweni mjini Zanzibar.

Alisema mkutano huo umekuja wakati mwafaka wakati changamoto kadhaa zinazohusiana na ardhi na mazingira zimekuwa zikiibuka katika nchi za Afrika Mashariki.

Kuongezeka kwa idadi ya watu sambamba na kukua kwa uchumi, alisema kumeleta changamoto nyingi katika sekta ya ardhi na mazingira katika nchi hizo na kutolea mfano migogoro ya ardhi ambayo imeikumba miji na vijiji ambayo baadhi hujumuisha wananchi na wawekezaji.

Alisema iwapo hali hiyo itaendelea itakuwa tishio kwa maendeleo ya kiuchumi na usalama kwa nchi za Afrika Mashariki huku akieleza alivyovutiwa na maudhui ya mwaka huu yasemayo ‘’Ardhi na Mazingira kwa Maendeleo Endelevu ya Afrika Mashariki”.

Dk. Shein alielezea kuvutiwa na maudhui hayo ambayo yamekuja wakati mwafaka kutokana na nchi nyingi za Afrika Mashariki kuweka mikakati ya makusudi katika kuimarisha mazingira na matumizi mazuri ya ardhi.

Kutokana na mada zitakazojadiliwa katika mkutano huo wa siku nne, alisema ana matumaini makubwa kuwa mkutano huo utatoa mbinu na njia mbadala za kutatua changamoto zilizopo.

Kwa upande wa Zanzibar, Dk. Shein alieleza hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutatua migogoro ya ardhi huku akisisitiza kuwa Zanzibar ardhi yote ni mali ya serikali kama ilivyoelezwa katika sheria namba 12 ya mwaka 1992.
Kuhusu mazingira, alieleza changamoto mbalimbali zinazosababishwa na shughuli za kibinadamu pamoja na athari za kimaumbile hasa mabadiliko ya tabianchi.

Dk. Shein alieleza haja kwa jumuiya hiyo ikashirikiana na taasisi mbalimbali za serikali katika masuala ya kimazingira hasa ikizingatiwa kwamba uchumi wa nchi za Afrika Mashariki unaendelea kukua katika sekta nyengine mpya ikiwemo sekta ya mafuta na gesi ambayo imethibikika kwamba imekuwa ikileta changamoto nyingi za mazingira katika nchi za Afrika pamoja na zile nchi za Mashariki ya Kati.

Alisisitiza kwamba taaluma ya sheria inahitajika katika kusimamia sekta hizo mpya ili kwenda sambamba na ukuaji wa sekta hizo mpya.