Shein ataka vyama kunadi sera kwa amani

01Aug 2020
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Shein ataka vyama kunadi sera kwa amani

RAIS wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, amevitaka vyama vya siasa kupitia wagombea wao kujinadi kwa wapigakura kwa kutangaza ilani na sera za vyama vyao na kuhubiri amani, umoja na mshikamano.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, baada ya kumalizika kwa Baraza la Eid El Hajj katika ukumbi wa mitihani wa Shule ya Sekondari Bumbwini, wilaya ya Kaskazini (B), mkoa wa Kaskazini Unguja jana. PICHA: OMR

Akilihutubia jana Baraza la Iddi el-Hajj huko Bumbwini Wilaya Kaskazini B Unguja, alisema ni matarajio yake makubwa kuwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu, utakuwa huru na haki kutokana na kukamilika kwa maandalizi mengi mapema sana.

Hata hivyo, alisema uchaguzi huru na haki utatokana na wanasiasa wenyewe kujiepusha na kauli zenye lengo la kupandikiza chuki na uhasama.

“Huu ni mwaka wa uchaguzi ifikapo Octoba 28. Matarajio yangu makubwa ni kwamba vyama vya siasa kupitia wagombea wao vitajinadi kwa wapigakura kwa kutangaza ilani na sera huku msisitizo mkubwa ni kuhubiri amani na utulivu,” alisema.

Dk. Shein aliwataka viongozi wa vyama vya siasa kutekeleza majukumu yao ya kufanya kampeni katika kipindi chote kwa kuzingatia sheria na kanuni za uchaguzi kupitia Tume ya uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

“Uchaguzi unaongozwa na sheria na kanuni ambazo viongozi wa vyama vya siasa vyote mnazijua kwa sababu mmefikia makubaliano na kusaini (kutia saini) matamko hayo… nataka myazingatie kwa makini sana,” alisema.

Pia alisema kipindi cha harakati za kampeni za uchaguzi mkuu kitumiwe kama kipimo cha kutafuta viongozi, kisiwe cha kusababisha mifarakano na kupandikiza chuki za kisiasa.

Dk.Shein alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha Waislamu na waumini wengine kwa ujumla kwamba katika Kurani, Mwenyezi Mungu amewataka waja wake na kuwaambia washikamane na si kufarakana.

Kwa Dk. Shein, hiyo ilikuwa hotuba yake ya mwisho katika Baraza la Iddi kutokana na kumaliza muda wake wa kuwapo madarakani miaka 10 baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu.

Alisema sherehe hizo zimekuwa zikifanyika katika sehemu mbalimbali Unguja na Pemba ambazo zimekuwa zikitoa nafasi na fursa kwa Waislamu kujumuika na viongozi wao katika kufanya ibada.

''Sherehe hizi za baraza la Idd-el-Hajj ndizo za mwisho kwangu kufuatia (kutokana na) kumaliza muda wangu wa kuwapo madarakani. Ni utaratibu mzuri ambao umetuwezesha sisi Waislamu kujumuika pamoja na kubadilisha mawazo kwa ajili ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazotukabili,” alisema.

Hata hivyo aliwapa pole Waislamu nchini ambao walikuwa katika matayarisho ya kuhuduria ibada ya Hijja huko Makka na kushindwa kutekeleza dhamira zao kutokana na janga la corona linazozikabili nchi mbalimbali duniani.

Alizitaka taasisi zinazoshughulikia safari ya ibada ya Hijja kufanya maandalizi ya mapema kwa mahujaji walioshindwa kufanya safari hiyo ili kutekeleza ibada hiyo kipindi kingine.

Dk. Shein alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupambana na ugonjwa wa corona ambao kwa sasa umetokomezwa huku ikiwa hakuna hata mgonjwa mmoja katika vituo vilivyotengwa kulaza wagonjwa hao.

Aliwataka wananchi kuchukuwa tahadhari zaidi kwa sababu ugonjwa huo upo katika baadhi ya nchi jirani huku baadhi ya shughuli muhimu zikilazimika kusitishwa kutokana na tishio lake.

Kadhalika, Aliwataka Waislamu hao kuwa na subra na uvumilivu kwani hiyo ndiyo mitihani ya Mwenyezi Mungu ambayo waja wake lazima kukabiliana nayo.

Naye Mufti wa Zanzibar, Sheikh Saleh Kabi, alimpongeza Dk Shein kwa uongozi wake bora katika kipindi cha miaka kumi ikiwa ni kigezo cha mfano wa kuiga.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Samia Suluhu Hassan, mgombea wa nafasi ya urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk. Hussein Ali Mwinyi, na mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano.

Habari Kubwa