Shein atuma salamu kifo cha Castro

28Nov 2016
Na Mwandishi Wetu
Zanzibar
Nipashe
Shein atuma salamu kifo cha Castro

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein (pichani), amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Jamhuri ya Cuba, Raul Castro, kufuatia kifo cha Rais mstaafu wa nchi hiyo, Fidel Castro, kilichotokea Ijumaa.

Katika salamu hizo, Dk. Shein alisema kuwa yeye na wananchi wa Zanzibar wamepokea kwa masikitiko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha kiongozi huyo mwana mapinduzi wa Cuba na ulimwengu.

“Wananchi wa Zanzibar tuko pamoja na wananchi wa Cuba kuomboleza kifo cha mwanamapinduzi huyo na tunatoa salamu zetu za rambirambi kwako wewe Mhehimiwa Rais na kwa wananchi wote wa Cuba,” salamu hizo zimeeleza.

Dk. Shein alisema kuwa kifo Fidel Castro ni pigo kubwa kwa nchi zinazoendelea na kuongeza kuwa kiongozi huyo ataendelea kukumbukwa kama alama ya matumaini kwa watu wanaokandamizwa kwa kuwa alitumia muda wote wa maisha yake kuwatumikia.

Dk. Shein alisema kuwa wananchi wa Zanzibar wataendelea kumkumbuka kiongozi huyo kutokana na kuyaunga mkono Mapinduzi ya Januari 12, 1964 na msaada wake katika kuijenga Zanzibar.

Habari Kubwa