Sheria kuasili watoto yapigiwa chapuo

22Jan 2020
Ibrahim Joseph
Dodoma
Nipashe
Sheria kuasili watoto yapigiwa chapuo

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, ameshauri kufanyika kwa mabadiliko ya sheria ya kuasili watoto ili kuwasaidia watoto 900,000 wanaoishi kwenye mazingira magumu.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, akitoa taarifa ya utekelezaji wa Bajeti ya Wizara (Fungu 52), kwa kipindi cha nusu mwaka 2019/2020, kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, jijini Dodoma jana. PICHA: OFISI YA BUNGE

Ushauri huo aliutoa jana alipokuwa akiwasilisha taarifa ya miezi sita ya utekelezaji ya Wizara hiyo kwa Kati ya Bunge ya Huduma za Maendeleo ya Jamii.

Waziri Mwalimu alishauri sheria ya kuasili mtoto kufanyiwa marekebisho ili kuwasaidia na kupunguza idadi kubwa ya watoto zaidi ya 900,000 wanaoishi kwenye mazingira magumu.

“Sheria hii ni ngumu nchini tofauti na nchi za jirani kama Ethiopia, ,Kenya na baadhi ya nchi zingine… ina mashariti magumu na haijaweka masharti rahisi kwa wazawa kumsaili mtoto na kukaa naye,” alisema.

Alibainisha kuwa kwa taarifa za wizara hiyo zilizopo, Julai hadi Desemba mwaka 2019, ni watoto 13 tu ndio waliopata huduma ya kuasiliwa kati ya watoto 900,000 wanaoishi katika mazingira magumu nchini.

Pia, alisema sheria hii ikifanyiwa marekebisho, itasaidia kupunguza wizi wa watoto mitaani na hospitalini kwa sababu itamruhusu mtu kumchukua mtoto kwa masharti rahisi na kukaa naye kama mtoto wake wa kumzaa.

Alisema katika mabadiliko hayo, wananchi wazawa watapewa kipaumbele katika kuwaasili watoto hao tofauti na watu kutoka mataifa ya kigeni.

Alisema masharti ya kuasili mtoto yapo kwenye sheria ya mtoto ya mwaka 2019 na imeainisha masharti ya Watanzania na wageni wanaohitaji kuasili mtoto hapa na nje ya nchi pamoja na adhabu zake kwa wanaokiuka masharti yaliyowekwa kisheria.

Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia, alisema Tanzania ni kubwa na kuna idadi kubwa ya watu, hivyo sheria ikifanyiwa mabadiliko itasaidia watoto hao kutunzwa na familia zinazohitaji watoto.

Nkamia alisema watoto hao ni nguvu kazi ya Taifa, hivyo wakitunzwa wataishi mazingira waliozaliwa nayo pamoja na kulisaidia taifa kiuchumi kwa siku za mbele.

Mbunge wa Viti Maalumu, Salma Kikwete, alishauri jamii kuendelea kutunza watoto wao hasa kuhakikisha wanalindwa kila eneo ili kuwaepusha na watu wabaya.

Alisema kutokana na uwapo wa taarifa za watoto kufanyiwa vitendo vya ukatili na baadhi ya watu, kila familia ichukue jukumu la kuwalinda ili kukomesha vitendo hivyo.

Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia, alisema sheria hiyo inatakiwa kuwa na mazingira rafiki kwa watu wote ili kuwasaidia watoto wanaoasiliwa kuishi katika mazingira bora.

Habari Kubwa