Shinyanga wafanya kikao cha tathimini MTAKUWWA

14May 2022
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe
Shinyanga wafanya kikao cha tathimini MTAKUWWA

SERIKALI mkoani Shinyanga imefanya kikao cha kutathimini utekelezaji wa mpango mkakati wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto MTAKUWWA.

Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Zuwena Omary.

Mpango mkakati huo wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto Tanzania (MTAKUWWA) ulianza mwaka (2017/18-2021/22), lakini  Mkoa wa Shinyanga ulianzisha mpango wake mkakati wa miaka mitano, kuanzia (2020-2025) ili kuhakikisha vitendo vyote vya ukatili vinakwisha hasa mimba na ndoa za utotoni.

Kikao hicho kimefanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa mkuu wa mkoa wa Shinyanga na kukutanisha waratibu wa MTAKUWWA kwa kila halmashauri, na wadau ambao wanahusika moja kwa moja kwenye utekelezaji wa mpango huo wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Zuwena Omary, akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho, alisema kutokana na jitihada za wadau kuendelea kupambana kutokomeza matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa kushirikiana na Serikali, imesababisha mkoa huo kushuka kutoka nafasi ya kwanza katika matukio ya ukatili hadi nafasi ya tano kitaifa.

Alisema kwa mujibu wa utafiti wa maendeleo ya watu na afya (TDHS) (2010) ilionekana mkoa huo kuongoza kitaifa kwa tatizo la ndoa za utotoni asilimia 59 na mimba za utotoni asilimia 34.

Aidha, alisema kwa mujibu wa utafiti kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI), ambao waliufanya mwaka (2020-21), mkoa huo umeshuka katika matukio yote ya ukatili kutoka kushika nafasi ya kwanza kitaifa hadi ya tano.

“Matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika Mkoa huu wa Shinyanga kiasi kikubwa yanasababishwa na mila, desturi kandamizi, uelewa mdogo wa haki za binadamu, na kutotambua athari za ukatili,”alisema Omary.

“Wote mliohudhuria kikao hiki ni wadau muhimu katika mapambano dhidi ya kupinga ukatili wa wanawake na watoto, natoa wito kwenu muendelee kuelimisha jamii juu ya madhara ya mila na desturi kandamizi, na kutoa elimu ya malezi na makuzi kwa wazazi. “Naamini jamii ikielimika na kuheshimu haki na utu wa kila binadamu, itasaidia kumaliza kabisa matukio ya ukatili na hatimaye kuwa na jamii salama,”aliongeza.

Katika hatua nyingine, aliyapongeza mashirikia yasiyo ya kiserikali na wadau wa maendeleo, kwa kazi kubwa ambayo wameifanya ya mapambano dhidi ya ukatili wa wanawake na watoto, kuwa kwa kiasi kikubwa wamesaidia katika mapambano hayo ya kupinga ukatili mkoani humo.

Kwa upande wa wajumbe waliohudhuria kikao hicho, kwa nyakati tofauti wakizungumza kwenye majadiliano, wamesema matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto kuendelea mkoani humo, yanatokana na sababu mbalimbali ikiwamo mila na desturi pamoja na jamii kutotoa ushahidi Mahakamani ili wahusika wapewe adhabu na kuwa fundisho kwa wengine.

Naye Mratibu wa mpango huo wa kitaifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWWA) mkoani Shinyanga Tedson Ngwale, alitaja dira ya taifa ya kutokomeza ukatili huo kuwa ni jumuishi ikiwamo Magereza, Polisi, Mahakama na wadau wengine wa kupinga vitendo vya ukatili.

Alitaja pia maeneo nane ya mkakati huo katika kupambana na matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, kuwa ni kuimarisha uchumi wa Kaya, kupinga mila na desturi kandamizi, mazingira salama sehemu za umma, malezi makuzi na mahusiano ya familia, utekelezaji na usimamizi wa sheria, utoaji huduma kwa wahanga wa ukatili.

Mazingira salama shuleni na stadi za maisha, pamoja na uratibu ufuatiliaji na tathimini.

Katika kikao hicho kimehudhuliwa na Ofisi ya Mashitaka ya Serikali mkoa wa Shinyanga, Mahakimu, Mawakili, Jeshi la Polisi, Waratibu wa Mtakuwwa, Wakurugenzi wa Halmashauri wadau kutoka Shirika la Msaada wa kisheria PACESH, Mfuko wa Ruzuku wa wanawake Tanzania (WFT-Trust) na Mwenyekiti wa Baraza la watoto Taifa Nancy Kasembo, na kikao hicho kimefadhiliwa na Shirika la mpango wa maendeleo duniani UNFPA.

Habari Kubwa