Shinyanga yajivunia mafaniko miaka 60 ya uhuru

08Dec 2021
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe
Shinyanga yajivunia mafaniko miaka 60 ya uhuru

SERIKALI mkoani Shinyanga, imejivunia mafanikio ya miaka 60 ya uhuru kwa kuimarisha huduma katika Sekta mbalimbali, ikiwamo uboreshaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru mkoani humo, ambapo kilele chake ni kesho Decemba 9, ambayo yatafanyika Jijini Dar es salaam katika uwanja wa uhuru.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, amebainisha hayo leo wakati Mkoa huo ulipokuwa ukiadhimisha miaka 60 ya uhuru, ambapo kilele chake kinafanyika kesho katika uwanja wa uhuru Jijini Dar es salaam.

Akizungumza wakati wa utoaji hotuba Mkuu huyo wa Mkoa, amesema  tangu mwaka 1961 nchi ya Tanzania kupata Uhuru kipindi hicho ilikuwa ikiitwa Tanganyika, katika mkoa huo kulikuwa na Hospitali moja, lakini mpaka mwaka huu (2021) kuna Hospitali nane, Zahanati kutoka 10 hadi 232, vituo vya Afya vipo 25.

“Wakati nchi inapata uhuru mwaka 1961 huduma za afya zilikuwa kwa kiwango cha chini, ambapo Zahanati zilikuwa zikipatikana sehemu maalumu za misionari na kwenye maeneo ya watemi, lakini mpaka sasa tunapozungumza zimeenea kwenye maeneo mengi ya jamii, na Serikali inaendelea kujenga huduma za afya zaidi,”amesema Mjema.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko, akizungumza kwenye maadhimisho hayo ya miaka 60 ya uhuru mkoani Shinyanga.
Watumishi wa Serikali wakiwa kwenye maadhimisho hayo ya miaka 60 ya uhuru.

“Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan umetoa kiasi cha Sh. bilioni 7.7 kwa ajili ya kuimarisha Sekta ya Afya mkoani Shinyanga, na wananchi wa mkoa huu mnakila sababu ya kumpongeza Rais Samia kwa kuleta miradi ya afya na kuimarisha afya zenu,” ameongeza.

Aidha akizungumzia Sekta ya elimu, amesema mkoa huo kabla ya uhuru ulikuwa na shule za msingi 52 kutoka Taasisi za kidini na Mgodi wa Madini ya Almasi Mwadui, lakini kwa sasa kuna shule za Msingi 646, za Serikali 586 binafsi 60.

Kwa upande wa shule za Sekondari, alisema ilikuwapo shule moja ya Shybush, lakini kwa sasa kuna shule za Sekondari 160, za Serikali 130, na Shule 30 ni za watu binafsi, ambapo pia Mkoa huo umejipanga kujenga Shule nyingine ya Sekondari kwa ajili ya wasichana tu.

Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga Magesa Donald akizungumza kwenye maadhimisho hayo ya miaka 60 ya uhuru.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa, amesema wanaendelea kutoa huduma za maji safi na salama kwa wananchi, na kuongeza mitandao ili wananchi wapate huduma hizo, ikiwamo na kuboresha miundombinu ya barabara, ambapo kwa miaka ya nyuma kabla ya uhuru hali ilikuwa mbaya tofauti na sasa.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akizungumza kwenye maadhimisho hayo ya miaka 60 ya uhuru, amewataka wananchi wa mkoa huo kuendelea kupanda miti kwa wingi ilikukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Aidha viongozi wengine waliohudhulia kwenye maadhimisho hayo ni Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga Donald Magesa, katibu wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Agnes Bashemu, Mkuu wa wilaya ya Kishapu Jonas Mkude, Mkuu wa wilaya ya Kahama Festo Kiswaga na Mbunge wa Jimbo la Msalala Iddi Kassimu.

Habari Kubwa