Shinyanga kuanzisha usafiri wa mabasi ya wanafunzi kuwaepusha ujauzito

10Apr 2021
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Shinyanga kuanzisha usafiri wa mabasi ya wanafunzi kuwaepusha ujauzito

SERIKALI mkoani Shinyanga, inatarajia kuanzisha usafiri wa mabasi ya wanafunzi kuwapeleka shule, ili kuwaepusha na vishawishi vya kuomba lift na kuambulia ujauzito na kuacha masomo.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Telack akizungumza kwenye kikao cha majadiliano namna ya kutokomeza mimba na ndoa za utotoni:PICHA NA MARCO MADUHU

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack, amebainisha hayo leo kwenye kikao cha majadiliano cha kutokomeza mimba na ndoa za utotoni, kilicho andaliwa na Shirika la Msichana Initiative ambalo linatetea haki za watoto hapa chini.

Amesema moja ya mikakati ya Mkoa huo katika kutokomeza mimba za wanafunzi, ni kuanzisha usafiri wa mabasi ambayo yatakuwa yakiwabeba kwenda shule na kurudi, ili kuwaepusha na vishawishi kwa wanaume ambao huwapatia lifti na kufanya nao mapenzi.

"Moja ya changamoto ambayo inasababisha watoto wetu kupewa ujauzito ni hizi lifti za kwenda shule, na ndio maana tunatarajia kuanzisha usafiri wa mabasi ya wanafunzi wa shule za Serikali, ili kuwaokoa na mimba za utotoni," amesema Telack.

"Usafiri huu wa mabasi utaanza na Shule za Barabara ya Olshinyanga na Viwandani, ambapo ndipo kwenye changamoto ya usafiri, na baada ya hapo tuta angazia maeneo mengine ili kulinda usalama wa watoto wetu," ameongeza.

Wajumbe wakiwa kwenye kikao hicho.

Katika hatua nyingine Telack amepiga marufuku watoto wa kike kwenda kuchunga mifugo maporini, jambo ambalo limekuwa likisababisha kukutana na vishawishi na kuambulia ujauzito.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Msichana Initiative Rebeka Gyumi, amesema wamefanya kikao hicho mkoani Shinyanga wakiwamo na Champion wa kupinga mimba na ndoa za utotoni, kwa lengo la kubadilishana mawazo nini kifanyike ili kutokomeza kabisa mimba hizo.

Mkurugenzi wa Shirika la Msichana Initiative Rebeka Gyumi akizungumza kwenye kikao hicho.

Aidha baadhi ya champion walioshiriki kwenye kikao hicho ni Mbunge wa Jimbo la Nkasi Aida Kenani, Mbunge Mwakilishi wa vijana Taifa kutoka mkoani Mwanza Ng'wasi Kamani, pamoja na Aliyekuwa Miss Tanzania 2005 Nancy Sumari.

Mbunge wa Jimbo la Nkasi , kushoto Aida Kenani, akifuatiwa na Mbunge Mwakilishi wa Vijana Taifa kutoka mkoani Mwanza Ng'wasi Kamani, akifuatia Mkurugenzi wa Shirika la Agape John Myola, na kulia ni Miss Tanzania 2005 Nacy Sumari wakiwa kwenye kikao hicho.

Habari Kubwa