Shirika la WoteSawa lazindua mradi usawa wafanyakazi za ndani

25Apr 2021
Neema Emmanuel
MWANZA
Nipashe Jumapili
Shirika la WoteSawa lazindua mradi usawa wafanyakazi za ndani

SHIRIKA lisilokuwa la kiserikali la WoteSawa limezindua mradi unaolenga kuchochea usawa kwa Wanawake  wafanyakazi wa Nyumbani.

Hayo yamebainishwa na Demitila Faustine, Afisa mradi wa usawa kwa wanawake wafanyakazi wa nyumbani. Alisema, lengo lao ni kuongeza uelewa kuhusu masuala ya afya ya uzazi na huduma za afya na kuwaongezea wigo katika ushiriki wa masuala ya uongozi na ushirikishwaji katika kufanya maamuzi.

Alisema ili kupunguza na kuondoa vitendo vya ukatili na kuongeza usawa na haki katika masuala ya kiuchumi, zaidi ya wafanyakazi wa nyumbani 150 watafikiwa pamoja na makundi mbalimbali katika jamii wakiwemo watendaji wa serikali,maofisa ustawi ,dawati la jinsia na maofisa elimu.

"Mradi utakuwa wa mwaka mmoja gharama yake ni million 116.4 na utafanya kazi katika Mkoa wa Mwanza na  Kagera na tutawafikia wafanyakazi wanawake wanaofanya kazi za ndani ili kutambua haki zao ili kufikia dunia yenye usawa na kupunguza aina zote za ukatili na unyanyasaji" alisema Faustine.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Afisa Tarafa Sengerema, Fadhil Abel alisema mradi huo utasaidia kuwafumbua macho wafanyakazi ili kusimamia na kufatilia haki zao kwani wengi wanapitia changamoto nyingi ikiwemo unyanyasaji wa kingono hasa kwa baba wenye nyumba na ndugu.

Naye Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Sengerema, Jovitha Ezekiel alisema Jeshi la Polisi litaanda mikakati mbalimbali itakayowaunganisha wadau hasa wa afya ili kuhakikisha jamii nzima inaelewa nini maana ya ukatili pia kupinga usafirishaji haramu ya watoto wadogo kufanya kazi na kutumikishwa pia jamii kuwa wepesi kutoa taarifa pale wanapoona kuna viashiria vya ukatili ama tukio linapotokea.

Habari Kubwa