Shirika lafungua kesi korti Kuu kumshitaki Ndugai

20May 2020
Allan lsack
ARUSHA
Nipashe
Shirika lafungua kesi korti Kuu kumshitaki Ndugai

Shirika la Uraia na Msaada wa Sheria (Cilao), limefungua kesi namba sita ya mwaka 2020, Mahakama Kuu kanda ya Arusha, kumshitaki Spika wa Bunge, Job Ndugai kumruhusu Cecil Mwambe, kuendelea na shughuli za Bunge ilhali amepoteza sifa za ubunge.

Mkurugenzi wa Shirika la Uraia na Msaada wa Sheria ( Cilao), akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, kuhusu kufungua kesi katika Mahakama Kuu kanda ya Arusha , kumshitaki Spika wa Bunge, Jobu Ndugai kumruhusu Mbunge wa Jimbo la Ndanda kuendelea na shughuli za kibunge wakati amepoteza sifa za kuwa Mbunge. Picha : Allan lsack

Mbali na Ndugai, Shirika hilo pia limemshitaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Ndanda Cicil Mwambe.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo Mei 20,2020, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Odero Odero, amesema shirika hilo limefungua kesi hiyo, kuiomba Mahakama kuu kutoa tafsiri kuhusu kitendo cha Spika Ndugai kumrejesha bungeni Cecil Mwambe wakati alijiuzulu nafasi  yake ya ubunge na uanachama wa Chadema na kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM).

Hata hivyo, amesema kabla ya kufungua kesi hiyo, shirika hilo lilikusanya maoni ya Watanzania 3,000, waliopinga kitendo cha Spika Ndugai kumrejesha bungeni Mwambe, hivyo shirika hilo limefungua kesi kwa niaba ya Watanzania na watu wote wanaopenda utawala wa sheria katika nchi ya Tanzania.

 

Habari Kubwa