Shule iliyosahaulika kwa miongo mingi yafufuka

08Oct 2017
Ashton Balaigwa
Nipashe Jumapili
Shule iliyosahaulika kwa miongo mingi yafufuka

SHULE ya Msingi Maguruwe yenye miaka 75 iliyokuwa mahututi kwa kutelekezwa, imefufuka baada ya kupata wadau wa kuijengea madarasa mapya.

Licha ya mwaka jana serikali kuanzisha kampeni ya madawati shule hiyo haina madawati hadi sasa na jitihada zinafanyika kuwaomba wadau kusaidia.

Maguruwe iliyoko wilayani Mvomero, mkoa wa Morogoro ilionekana kama imetelekezwa kutokana na wanafunzi kusomea kwenye madarasa yaliyobomoka yasiyo na madirisha, huku wakiwa chini kwa kukosa madawati.

Shule hiyo iliyojengwa mwaka 1942 na Waingereza, licha ya kuwa na upungufu huo pia inakabiliwa na tatizo la uhaba wa walimu.
Kwa sasa kuna walimu wanne lakini pia mwalimu mkuu hana ofisi, aidha inaikabiliwa na matatizo lukuki na kwamba madarasa yanayotumika ni matatu.

Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tanzania (CDTF), ndiyo iliyojitosa kujenga madarasa mapya matatu pamoja na ofisi ya walimu kwa gharama ya Shilingi milioni 45 na kuahidi kukamilisha kazi hiyo mwishoni mwa mwezi huu.

Akizungumza wakati wa kukagua ujenzi Mkurugenzi Mtendaji wa CDTF ,Henry Mgingi,alisema kuwa waliamua kujenga madarasa ya shule hiyo baada ya kuombwa na wanakijiji walipowatembelea mwanzoni mwa mwaka huu.

Alisema tayari ujenzi wa madarasa katika shule hiyo umefikia kwa kiwango cha asilimia 95 na kilichobaki ni shughuli ndogo ambazo zinatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi huu na kukabidhiwa uongozi wa kijiji hicho.

Mwalimu Mkuu Alex Gervas,alisema shule hiyo ina wanafunzi 343 lakini madarasa yanayotumika ni matatu ambayo wanafunzi hao wanapokezana kwa zamu na kuwa kuna mahitaji ya madarasa matano pamoja na ofisi za walimu .

Hata hivyo, alisema pamoja na upungufu huo wanafunzi wa shule hiyo wengi wanalazimika kukaa chini kutokana na kukosa madawati na kutaka wadau wengine kusaidia shule hiyo kutatua changamoto ya madawati baada ya kukamilika kwa ujenzi wa majengo hayo.

Diwani wa Kata ya Bunduki iliko shule hiyo,Prosper Mkunule,alisema shule hiyo imetelekezwa kwa muda mrefu na majengo yake kuwa katika hali mbaya licha ya kuwasilishwa kwa taarifa katika ngazi za juu.

Ngazi hizo ni pamoja na uongozi wa Halmashauri ya Mvomero lakini mpaka sasa hakuna mafanikio yoyote ya kujengwa kwa miundombinu iliyokuwa taabani.

Alisema kuwa kutokana na uchakavu wa miundombinu na ukosefu wa madawati,aliamua kuwasiliana na CDTF ambayo ilikubali kusaidia.

Habari Kubwa