Shule iliyougua moto yapata msaada wa vifaa

26Jul 2021
Lilian Lugakingira
Muleba
Nipashe
Shule iliyougua moto yapata msaada wa vifaa

SHULE ya Sekondari ya Seminari ya Kiislamu ya Jakaya Kikwete, iliyoko wilayani Muleba mkoani Kagera, ambayo mabweni mawili yanayotumiwa na wanafunzi wa kike yaliteketea kwa moto na kusababisha uharibifu wa majengo na vifaa vya wanafunzi, imepatiwa msaada wa vifaa vya ujenzi wenye thamani ya ..

Shs. Mil 10/-

Akikabidhi vifaa hivyo ambavyo ni mifuko ya saruji 170, magodoro 43, mashuka 87, madaftari makubwa na madogo 600, sare za shule na mabegi ya kuhifadhia nguo, mkuu wa wilaya ya Muleba, Toba Nguvila amesema kuwa serikali imefikia uamuzi wa kutoa msaada wa vifaa hivyo, ili kuwawezesha wanafunzi kuendelea na masomo bila usumbufu.

Nguvila amewataka wanafunzi wa shule hiyo ambao vifaa vyao vimeungua kwa moto kutokata tamaa na badala yake waendelee kusoma kwa bidii ili waweze kufaulu mitihani na kutimiza malengo yao ya baadae, na kwamba serikali inaendelea kutafuta misaada zaidi ili kuhakikisha mabweni yote yanarejeshwa katika hali ya kawaida.

Naye afisa elimu sekondari wa wilaya hiyo Jered Muhile amewataka wanafunzi hao kuwa na subira wakati serikali ikiendelea kufanya jitihada za kudhibiti majanga kama hayo yasitokee tena, maana mbali na kuharibu mali pia yanahatarisha maisha ya wanafunzi.

Mkuu wa shule hiyo Yasin Mikidad aliishukuru serikali kwa msaada huo unaolenga kuwawezesha wanafunzi kuendelea na masomo kwa wakati na kutumia fursa hiyo kuwasihi wanafunzi kuendelea kuwa wavumilivu katika kipindi hiki ambacho uongozi wa shule na serikali wanaendelea kutafuta misaada kwa ajili yao.

Mabweni mawili ya shule ya sekondari ya Seminari ya Kiislamu ya Jakaya Kikwete yenye wanafunzi 138 wa kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne, yaliteketea kwa moto Julai 23 mwaka huu, saa saba mchana wakati wanafunzi hao wakiendelea na somo la dini ya Kiislamu.