Shule kuhifadhi washukiwa corona

02Apr 2020
Happy Severine
Simiyu
Nipashe
Shule kuhifadhi washukiwa corona

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka, amesema Mkoa huo hautatumia hoteli kwa ajili ya kuhifadhi watu watakaohisiwa kuwa na maambukizi ya virusi vya corona.

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka, picha mtandao

Mtaka amesema kwamba badala yake watatumia shule za sekondari za bweni.

Alisema wameamua kuchukua uamuzi huo ili kuwapunguzia gharama za kuishi katika hoteli siku zote ambazo watakuwa karantini.
Hata hivyo, Mtaka alisema kwamba utaratibu huo hautawafunga watu wenye uwezo ambao watapenda kwenda hotelini.

Mtaka alisema hayo jana alipokuwa akipokea msaada wa vifaa vya ujenzi wa Shule ya Sekondari Mtaka wilayani Busega kutoka kwa viongozi wa Umoja wa Makanisa 21 ya Kikristo Tanzania Kata ya Lamadi.

Alisema kila wilaya imetenga shule yenye vitanda vya kutosha na mazingira mazuri kwa ajili ya kuwahifadhi washukiwa hao, huku akiwataka wananchi wa Mkoa huo kuendelea kuchukua tahadhari.

“Tumeamua kuwa hatutatumia hoteli kuhifadhi mtu yeyote ambaye atabainika kuwa na maambukizi ya virusi vya corona, tumeamua kutumia shule za sekondari za bweni ...labda mtu mwenyewe aamue kupelekwa katika hoteli zilizoainishwa,” alisema Mtaka.

Katika hatua nyingine, aliwataka wazazi wa wanafunzi wa madarasa ya mitihani mkoani humo kuwafuatilia na kuwasimamia watoto wao kuhakikisha wanajisomea katika kipindi hiki ambacho shule zimefungwa kutokana na tishio la ugonjwa huo.

Habari Kubwa