Shule za DC Makonda zasuasua

27Feb 2016
Christina Mwakangale
Dar
Nipashe
Shule za DC Makonda zasuasua

Ujenzi wa shule sita za sekondari uliokusudiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, tangu mwishoni mwa mwaka jana ili kuchukua wanafunzi waliokosa nafasi za kuingia kidato cha kwanza umeendelea kusuasua kutokana na matatizo ardhi.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda.

Desemba mwaka jana, Makonda alitangaza ujenzi wa shule sita za sekondari katika kata zote ambazo hazina sekondari.

Hatua hiyo imelenga kuwezesha wanafunzi 3,000 ambao walifaulu mtihani wa darasa la saba na kukosa nafasi za kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu, wajiunge na masomo ya sekondari katika awamu ya pili.
Muhula wa masomo kwa shule za nchini ulianza Januari 13, mwaka huu.

Ingawa ujenzi wa shule nne katika kata za Mbezi Juu, Kimara, Mzimuni na Ubungo umeendelea, shule hizo hazijakamilika ili kuchukua wanafunzi hao mwaka huu na kumewapo kwa changamoto ya viwanja kwa kata mbili, Ofisa Uhusiano manispaa, Sebastian Mhowera aliiambia Nipashe jana.

Kata za Saranga na Magomeni zimekwama kuanza ujenzi huo kutokana na kukosa eneo, na sasa Manispaa ya Kinondoni imeiomba Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, kuipa kibali cha kubadili matumizi ya ardhi, alisema.

Mhowera alisema wakandarasi wanaendelea na ujenzi wa shule katika kata nne hizo, huku Manispaa ikiendelea kusubiri kibali kutoka wizarani.

"Tatizo kubwa ni maeneo ya ujenzi wa shule," alisema Mhowera na kueleza zaidi, "inabidi matumizi ya ardhi kwa baadhi ya maeneo yabadilishwe.

"Kama ilikuwa ni eneo kwa ajili ya soko au matumizi mengine, matumizi yapewe kipaumbele katika ujenzi wa shule."
Ufaulu wa darasa la Saba ya mwaka jana, ulipanda ikilinganishwa na mwaka 2014, hivyo changamoto kubwa kuwa ni uhaba wa madarasa kwa baadhi ya manispaa.

Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), lilisema watahiniwa 518,034 kati ya watahiniwa 763,602, waliofanya mtihani huo mwaka jana, walifaulu kwa kupata alama 100 na zaidi kati ya alama 250, sawa na asilimia 67.84.

Mwaka 2014 watahiniwa 451,392 kati ya watahiniwa 792,118 waliofanya mtihani walifaulu sawa, na asilimia 56.99, hivyo kuwapo na ongezeko la ufaulu kwa asilimia 10.85.

Habari Kubwa