Shule zafunguliwa, tahadhari dhidi ya corona yachukuliwa

30Jun 2020
Na Waandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Shule zafunguliwa, tahadhari dhidi ya corona yachukuliwa

JANA wanafunzi wa shule za awali hadi kidato cha nne walirejea shuleni baada ya kupumzika tangu Machi 18, mwaka huu, kutokana na janga la corona.

Wanafunzi hao wamerejea baada ya Rais John Magufuli kutangaza kufunguliwa kwa shule hizo, huku Wizara za Elimu na Afya zikitoa mwongozo wa namna ya kuendelea na masomo kwa kuchukua tahadhari ya corona.

Katika shule wanafunzi walizorejea jijini Dar es Salaam na Dodoma, kulikuwa na maji ya kunawa mikono na kila mwanafunzi kuvaa barakoa isipokuwa wenye matatizo ya kiafya au chini ya miaka nane.

Aidha, katika shule nyingi wanafunzi walionekana wakiwa wamevaa barakoa, huku walimu na wafanyakazi wengine wakichukua tahadhari.

Baadhi ya wanafunzi walirudishwa nyumbani kwa kukosa barakoa, jambo ambalo liliwafanya wakose masomo kwa siku ya jana.

Pia, baadhi ya wazazi wamelalamikia mchanganuo wa kulipa ada kwa robo ya pili huku baadhi ya shule zikiwataka kulipa fedha ya chakula na usafiri kwa ukamilifu wake.

Wazazi wa wanafunzi wa darasa la saba wa Shule ya Atlas iliyopo Madale jijini Dar es Salaam, wamewasilisha malalamiko yao kwa uongozi ikiwamo mchanganuo wa ulipaji ada wa kumalizia robo ya kwanza ya muhula wa pili.

Vilevile wamewasilisha malalamiko kuhusu hali ya mazingira ya shule hiyo na taratibu nyingine zinazotumika.

Mapendekezo hayo yalipokelewa juzi jioni na Makamu Mkuu wa Shule hiyo, Joseph Msafiri, ambaye alifafanua kuwa suala la ulipaji wa ada kwa muhula wa kwanza wazazi halipingiki kutekelezwa na wazazi wote kwa sababu serikali umeusogeza.

Kuhusu muhula wa pili kwa robo ya kwanza, alisema yapo mazungumzo yanayoendelea kwenye uongozi wa shule ili kutoa nafuu kwa wazazi wa wanafunzi wa darasa la saba.

Mambo mengine ambayo wazazi walilalamikia ni kitendo cha shule kufunguliwa na kutangaziwa waanze kuwapeleka watoto Jumapili, lakini mazingira ya shule wameyakuta machafu, huku uongozi ukipaka rangi mabweni siku hiyo.

Akitolea ufafanuzi wa changamoto hiyo, Msafiri alikiri wamewapokea watoto huku shule ikiwa na mazingira machafu na hiyo imetokana na ukosefu wa fedha.

Msafiri alikiri changamoto ya watoto kutopewa maji ya kunywa wakati mwingine na kufafanua kuwa husababishwa pale panapotokea tatizo la huduma hiyo.

Katika hilo wazazi walilalamikia uongozi kuwa licha ya wao kutozwa fedha za kujikimu 'pocket money', lakini inapotokea changamoto hazitumiki hata kununua maji ya watoto.

DODOMA

Katika Shule ya Msingi Makole, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Veronica Mrope, alisema: "Ili kuwaondolea hofu wanafunzi na walimu, kabla ya kuanza masomo wanafanya maombi ili kuwalinda katika masomo yao.”

Nipashe pia ilitembelea, Shule ya Sekondari Dodoma na Central kuangalia mwenendo wa mitihani ya kidato cha sita iliyoanza jana nchini na kushuhudia ulinzi ukiwa umeimarishwa na tahadhari za ugonjwa huo zikiwa zimezingatiwa.

Aidha, baadhi ya shule zimechukua tahadhari kwa kuweka vifaa vya kunawa mikono kwenye maeneo yote muhimu ya kuingia na kuzingatia uvaaji wa barakoa.

Katika Shule ya Sekondari Dodoma, Viwandani, Shule ya Msingi Mlimwa C, Kiwanja cha Ndege na Fountain Gate Academy, wanafunzi walionekana wakiingia kwa mpangilio huku wakipimwa joto na kunawa mikono.

Pamoja na mikakati ya kukabiliana na ugonjwa huo, baadhi ya shule zimeongeza muda wa masomo ili kumaliza muhtasari ya mihula inavyotakiwa.

Mkuu wa Shule ya Dodoma Sekondari, Amani Mfaume, alisema wamejipanga kufundisha hadi siku za Jumamosi kwa baadhi ya vidato ili kufidia muda wa kumaliza muhtasari waliyotakiwa kufundisha.

Naye, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Fountain Gate Academy, Abilius Wamara, alisema shule imeongeza saa mbili ili kumaliza mihula kwa muda uliopangwa.

Aidha, alisema pia wamechukua tahadhari zote za kukabiliana na ugonjwa huo ikiwamo kuwatakasa mikono wanafunzi kabla ya kupanda gari la shule na kupimwa joto na kunawa mikono kabla ya kuingia eneo la shule.

Katika hatua nyingine, Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege na Mlimwa C, baadhi ya wanafunzi wasiokuwa na barakoa walirudishwa nyumbani ili kuvaa.

Mmoja wa wanafunzi, AbdulMarik Juma, ambaye anasoma Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege, alionekana akirudi nyumbani baada ya kufika shule na alipoulizwa, alisema amekatazwa kuingia shule kwa kuwa hajavaa barakoa.

“Nimerudishwa nyumbani na mwalimu kaniambia hairuhusiwi kuingi darasani bila kuvaa barakoa,” alisema.

Naye, mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mlimwa C, Merina John, alisema amezuiliwa kuingia shule kwa kuwa hana barakoa.

Ofisa Elimu wa Shule za Msingi, Joseph Mabeyo, alisema hawezi kuzungumzia suala hilo hadi mwandishi apewe kibali na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Imeandikwa na Romana Mallya (DAR), Ibrahim Joseph na Renatha Msungu, Peter Mkwavila na Paul Mabeja (DODOMA)

Habari Kubwa