Shule zashindwa kuzingatia tahadhari dhidi ya UVIKO-19

18Jan 2022
Jenifer Gilla
Dar es Salaam
Nipashe
Shule zashindwa kuzingatia tahadhari dhidi ya UVIKO-19

MRUNDIKANO wa wanafunzi kwenye vyumba vya madarasa na kutozingatia tahadhari ya UVIKO-19, umebainika katika baadhi za shule zilizofunguliwa jana jijini Dar es Salaam.

Uchunguzi wa Nipashe umebaini baadhi ya shule zilizoko Manispaa ya Temeke, Ilala, Ubungo na Kinondoni hazikuwa na vifaa vya kunawa mikono, wanafunzi na walimu kuvaa barakoa na kukaa kwa umbali unaotakiwa kwa mujibu wa mwongozo wa afya wa kujikinga na ugonjwa huo.

Baadhi ya shule za msingi zilionekana wanafunzi wakibanana, huku wazazi wakishukuru watoto wao kupata shule jirani na nyumbani kuepusha usumbufu wa kwenda umbali mrefu, bila kujali wanakaa wangapi kwenye darasa.

Aidha, kwenye baadhi ya madarasa wanafunzi walikuwa zaidi ya kiwango kilichowekwa kwenye darasa moja, huku kwenye dawati moja wakikaa wanne.

Katika Shule ya Msingi Vetenari, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, madarasa yalikuwa yamejaza wanafunzi huku wakikaa bila kupeana nafasi.

Katika shule hiyo darasa la kwanza lenye mikondo minne (A-D) kila mkondo ukiwa na zaidi ya idadi ya kiwango kinachotakiwa cha wanafunzi 40 hadi 45 kwa darasa moja.

Walimu walionekana kutozingatia uvaaji wa barakoa na kuachiana nafasi ya umbali wa mita moja tofauti na mwongozo uliotolewa na Wizara ya Afya na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Wakati Shule ya Msingi ya Ruvuma, ikiwa na wanafunzi zaidi ya idadi inayotakiwa, kulikuwa na ndoo moja pekee ya kunawia mikono na uvaaji wa barakoa haukuzingatiwa.

Hali hiyo ilionyesha kuwatia hofu baadhi ya wazazi waliokutwa nje ya shule hizo wakisubiri kuwachukua watoto wao.
“Yaani na janga hili la corona linaloendelea natamani dawati moja wakae watoto wawili ili kupunguza maambukizi, lakini sasa tutafanyaje wacha wasome tu Mungu atasaidia,” alisema Radhia Abdallah.

“Kwa hali hii tuendelee kuomba Mungu hii Omicron (kirusi kipya) isisambae nchini maana watoto wetu hawatopona na ndiyo watatuletea majumbani,” alalamika, Anastazia mzazi mwenye mtoto katika shule hiyo.

Katika Shule ya Msingi Ruvuma, Nipashe ilikuta mwalimu wa darasa la kwanza akiwa amezongwa na kundi la watoto kila mmoja akitaka kusahihishiwa daftari lake hali ambayo inahatarisha maambukizi ya kirusi hicho cha corona.

ADA ZAFUTWA

Pamoja na changamoto hiyo, wazazi walioandikisha watoto wao darasa la kwanza walipongeza maboresho sekta ya elimu hasa kwa kutodaiwa fedha yoyote.

Sakina Saidi, aliyeandikisha mtoto wake katika Shule ya Msingi JICA, iliyoko Tabata, Manispaa ya Ilala, alifurahia kutotakiwa kutoa mchango wowote wakati wa mchakato huo zaidi ya kutoa fedha kidogo kwa ajili ya kununua vifaa muhimu vya mtoto vya shule.

“Nimetoa Sh. 27,000 tu ambayo wamenipatia sweta, ‘t-shirt’, lebo pamoja na madaftari, kwa kweli hakukuwa na fedha ya ziada, naishukuru sana serikali,” alisema Sakina Saidi.

Wakati wengine walifurahia kutodaiwa hela ya chai kwa mwalimu ili kupata nafasi ya kuandikisha mtoto, kitendo ambacho wanasema kilishamiri miaka ya nyuma.

“Miaka ya nyuma huu mtindo ulishamiri sana, unaambiwa nafasi hakuna, ukibembeleza sana unaambiwa utoe Sh. 15, 000 ya chai ya mwalimu ndiyo upewe nafasi, mwanangu aliyepo darasa la sita aliingia kwa mtindo huo, nashukuru huyu aliyeingia mwaka huu japo nafasi za shida, lakini sikuombwa,” alisema.

Juhudi za gazeti hili kuwapata wakuu wa wilaya hizo kuzungumzia hali hizo hazikuzaa matunda, na pia simu ziliita bila majibu.

Habari Kubwa