Shule zikaguliwe kabla na baada ya kuanzishwa -​​​​​​​Rais Magufuli

16Sep 2020
Lilian Lugakingira
Bukoba
Nipashe
Shule zikaguliwe kabla na baada ya kuanzishwa -​​​​​​​Rais Magufuli

​​​​​​​RAIS Dk. John Magufuli, ameziagiza Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Wizara ya Elimu kukagua na kuhakikisha shule zote zinazingatia masuala ya usalama kabla na baada ya kuanzishwa kwa shule ili kujihakikishia kama zinafuata matakwa ya kisheria-

​​​​​​​RAIS Dk. John Magufuli.

-kwa lengo la kuzuia majanga ya moto yasijirudie tena.

Dk. Magufuli ambaye pia ni mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ametoa agizo hilo katika mkutano wake wa kampeni wa kuomba ridhaa ya kuendelea kuongoza nchi, uliofanyika katika uwanja wa Gymkhana katika Manispaa ya Bukoba, kufuatia tukio la moto lililoteketeza shule ya msingi Byamungu Islamic iliyoko kata Itera wilayani Kyerwa, na kusababisha vifo vya wanafunzi kumi na majeruhi sita.

Aidha, ameagiza Jeshi la Polisi kumwachia Mkuu wa shule hiyo Suleiman Byamungu anayeshikiliwa na Jeshi hilo, huku akisema kuwa kuendelea kumshikilia ni kumwongezea uchungu wa kupoteza wanafunzi wake kumi aliokuwa akiwalea kama watoto wake.

"Nafahamu Mkuu wa shule anashikiliwa na Polisi, Mkuu wa Mkoa mwalimu huyo aachiwe maana kama kuna uzembe ulifanyika hata akiwa nje ataweza kutoa ushirikiano kwa polisi, nina imani huyu Mkuu wa Shule hana roho mbaya ya kufikia kuwachoma moto wanafunzi wake" amesema Dk. Magufuli.

Shule ya msingi Byamungu Islamic ilitetekea kwa moto usiku wa kuamkia Septemba 14, 2020 na kusababisha vifo vya wanafunzi kumi na majeruhi sita ambao walilazwa katika hospitali teule ya Wilaya ya Karagwe ya Nyakahanga, ambapo baadae wanafunzi wanne wamehamishiwa Hospitali teule ya kanda ya Bugando iliyoko jijini Mwanza.

Kwa mujibu wa muuguzi kiongozi wa wodi ya watoto katika hospitali ya Nyakahanga, Theophilda Ndibalema, amesema majeruhi waliohamishiwa hospitali ya Bugando ni  Lukumani Said Ramadhan (7), Imani Majaliwa Hatuna (12), Hashraph Mohamed (7) na Juma Seif Juma (12).

Pia ametaja majeruhi wawili waliobaki katika hospitali hiyo ya Nyakahanga kuwa Avitus Sperius (8) na Swabrudin Swaibu (11).

Habari Kubwa