Shule zilivyotelekeza mwongozo wa corona

31Jan 2021
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe Jumapili
Shule zilivyotelekeza mwongozo wa corona

KUNA msemo kwamba 'kinga ni bora kuliko tiba’, unaosisitiza umuhimu wa kuchukua tahadhari kujikinga dhidi ya jambo fulani badala ya kusubiri litokee ndipo ulitatue.

Machi 16, mwaka jana, Tanzania iliripoti kuwa na mgonjwa wa kwanza wa corona. Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), idadi ya visa iliongezeka kutoka kimoja hadi kufikia 480 Aprili 2020 huku vifo 18 vikiripotiwa kutokana na ugonjwa huo.

Serikali ilichukua hatua mbalimbali kukabiliana na virusi hivyo kuhakikisha inalinda wananchi wake dhidi ya janga hilo.

Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni kutolewa kwa miongozo ya kitaalamu kwa umma kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ikielekeza jinsi ya kuepuka maambukizi ya ugonjwa huo usio na tiba hadi sasa duniani.

Miongozo iliyotolewa ilielekeza kukaa umbali wa mita moja hadi mbili kati ya mtu na mtu hasa anayekohoa na mwenye historia ya kusafiri kutoka nje ya nchi, kunawa mikono kwa maji safi tiririka na sabuni, kuvaa barakoa na kutumia vitakasa mikono.

Mikusanyiko ya watu nayo ilizuiwa kwa muda, ikiwamo kufungwa kwa shule na vyuo ili kupunguza kasi ya kusambaa kwa ugonjwa huo nchini.

Baada ya ugonjwa huo kudhibitiwa, serikali ilitangaza kufungua shule Juni mwaka jana, huku ikitoa mwongozo uliokuwa ukiainisha mambo mbalimbali ya kufuatwa kwa wanafunzi na walimu ikiwamo kunawa mikono kwa maji safi na sabuni.

Aliyekuwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, aliagiza shule kuwa safi na kutengwa maeneo ya kunawa mikono katika maeneo ya kimkakati.

Baada ya kubainika ugonjwa huo umetokomezwa nchini, mwongozo huo wa kukabiliana na corona kwenye maeneo mbalimbali ikiwamo shule kwa sasa ni kama umetelekezwa huku wanafunzi wakiingia darasani bila kunawa mikono na maji tiririka.

Nipashe ilifuatilia katika baadhi ya shule za msingi na sekondari jijini Dodoma ikiwamo Shule za Msingi Uhuru, Makole na Sekondari ya Kisasa na kubaini taratibu za kunawa mikono kila wanapoingia na kutoka shule hazifuatwi huku zingine zikiwa na ndoo zisizo na maji.

Mbali na shule, hata wananchi wamepuuza unawaji wa mikono mitaani, licha ya vifaa vya kunawa mikono kuwapo kwenye baadhi ya maeneo.

KAULI ZA WANANCHI

Mkazi wa Chang’ombe, Stella John, anasema baada ya kutangazwa ugonjwa wa corona haupo, watu wamepuuza kunawa mikono kwa maji tiririka na wanapokuta yamewekwa, wanapita bila kunawa.

“Wataalamu wa afya wanatuambia tukinawa mikono, inasaidia kupambana na ugonjwa wa corona na magonjwa mengine ya mlipuko, tatizo sisi wananchi hadi tusukumwe kunawa mikono,” anasema.

Paul Madeha, anasema hajaona umuhimu wa kunawa mikono kila anapoingia maeneo mbalimbali mitaani kwa kuwa ugonjwa wa corona haupo.

“Kwani ugonjwa umerudi? Kama haupo, kwanini mimi ninawe mikono, yaani tunanawa tu kama tunakula,” anasema.

Zawadi Matumbi anasema baada ya kutangaziwa corona imeisha, shule zilianza taratibu kupuuza mwongozo hasa wa unawaji mikono bila kujua hali hiyo inasaidia kuwaepusha watoto dhidi ya magonjwa mengine ikiwamo kipindupindu.

Adamu Ally, anasema ameshuhudia watoto wao hanawi mikono wanapowafikisha kwenye eneo la Shule ya Msingi Kisasa kwa sababu hakuna sehemu iliyoandaliwa kwa ajili hiyo.

Ally anaiomba shule hiyo kuendelea na  utaratibu wa  kuweka vifaa vya kunawa mikono getini na kwenye vyumba vya madarasa kwa sababu utaratibu huo ulikuwa unasaidia kuwakinga watoto dhidi ya magonjwa ya homa ya matumbo.

WALIMU WALONGA

Mkuu wa Shule ya Sekondari Dodoma, Amani Mfaume, anasema shule yao imeweka vifaa vya kunawa mikono kwa ajili ya kujikinga na magonjwa, lakini wapo wanafunzi na watumishi  wanaopuuzia kunawa  mikono yao.

Mfaume anasema shule imeweka vifaa vya kunawa mikono nje ya kila chumba cha darasa ili wanafunzi na watumishi wa shule hiyo watumie wakati wowote wakiwa shuleni.

Anataja sababu ya shule hiyo kuendelea na utaratibu wa kunawa mikono wakati wa kuingia na kutoka kuwa ni kujikinga dhidi ya magonjwa ya mlipuko, hasa yanayotokana na uchafu kwenye mikono ya mtu.

Anasema lengo la shule ni kuendelea kuhakikisha kila siku vifaa hivyo vinakuwa na maji na sabuni ili kuwakinga na magonjwa  wanafunzi na  watumishi waliopo shuleni.

Mkuu wa shule huyo anasema wageni wanapoingia shuleni, utaratibu wa kufuatwa ni huo, lakini wengine wanapita bila kunawa licha ya vifaa vya kunawa mikono na vitakasa mikono vimewekwa ofisini na getini.

OFISA AFYA

Ofisa Afya Jiji la Dodoma, Abdallah Mahia, anasema hana taarifa za shule kupuuza kutekeleza mwongozo wa Wizara ya Afya na kwamba kila shule kuna mwalimu anayeshughulika na masuala ya afya.

“Tangu kipindi kile cha maambukizi ya corona, tuliendelea kuhamasisha kwenye maeneo ya mikusanyiko ya watu kuendelea kunawa mikono ili kuepukana na magonjwa yanayotokana na uchafu kama kipindupindu, minyoo na homa za matumbo.

"Kama kuna shule ambayo imepuuzia haya mambo, nitakuwa nimesikitika sana maana ninachofahamu shule zinaendelea na taratibu za unawaji wa mikono na si kwa sababu tu ya corona.

"Kila shule imepewa vifaa vya kunawa mikono, inawezekana baadhi wamevifungia ndani. Wananchi wengi ukiwaambia mtu unawe mikono na maji tiririka na sabuni, wanauliza kama ugonjwa umerudi," anasema.

Anatoa wito kwa wananchi kujenga utamaduni wa kunawa mikono na kutumia vitakasa mikono ili kujikinga na magonjwa.

“Kunawa mikono ni msingi wa afya katika jamii, magonjwa mengi yanayoripotiwa kwenye vituo vya kutoa huduma yanatokana na uchafu ni asilimia 80 ya magonjwa yote, mikono yetu ikiendelea kuwa safi, hatutapata magonjwa,” anasema.

Anawataka walimu kusimamia ipasavyo watoto kunawa mikono ili kujikinga na maradhi.

Ni takriban mwaka mmoja tangu kuzuka kwa ugonjwa huo Desemba 2019 Wuhan, China ulikoanzia na kuenea kwa kasi duniani.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinabainisha kuwa tangu Desemba 2019 hadi Januari 25 mwaka huu, kulikuwa na wagonjwa milioni 99.4 na vifo milioni 2.13 vilivyoripotiwa kutokana na virusi hivyo.

Desemba mwaka jana, Taasisi ya Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Afrika (Afrika CDC), ilinukuliwa ikibainisha kuwa watu milioni 2.25 walipata virusi hivyo na vifo 53,543 vilitokea barani.

Hivi sasa nchi mbalimbali zimeendelea kuchukua hatua ikiwamo kuweka sharti la upimaji maambukizi hayo kwa wasafiri wanaotoka nchi moja kwenda nyingine, Tanzania ikiwamo.

Kwa mujibu wa Afrika CDC, nchi zilizoathiriwa vibaya zaidi ni Afrika Kusini, Morocco, Misri na Ethiopia.

Habari Kubwa