Shule zilizoharibiwa na tetemeko zakarabatiwa

22Sep 2016
Lilian Lugakingira
Nipashe
Shule zilizoharibiwa na tetemeko zakarabatiwa

SERIKALI kupitia kamati ya maafa ya mkoa kwa kushirikiana na Idara ya Uratibu wa Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, imeanza kuchukua hatua za kurejesha miundombinu ya shule za sekondari za wavulana za Ihungo na Nyakato kwa kuanza kubomoa majengo yaliyoharibiwa na tetemeko la ardhi.

Tetemeko hilo limeelezwa kuwa na ukubwa wa 5.9 katika vipimo ya majanga hayo kimataifa, na kwa mujibu wa mtandao wa kompyuta wa earthquaketrack.com ndilo kubwa zaidi katika historia kutokea nchini.

Hatua za kuanza kubomoa majengo ya shule hizo, zimeanza kuchukuliwa baada ya kamati ya maafa kutoa misaada mbalimbali kama huduma za afya kwa majeruhi, huduma za mahema na maturubai na chakula ili waathirika kujihifadhi baada ya kupoteza nyumba zao.

Hata hivyo, Serikali ya Japan ilimuahidi Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wiki iliyopita kwamba ingechukua jukumu la ukarabati wa shule zote zilizoharibiwa na tetemeko mkoani Kagera, katika hafla maalumu iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu alikitaka kitengo cha maafa katika Ofisi yake kuwasiliana na Japan kwa ajili ya kuwezesha ushiriki wa nchi hiyo katika ukarabati huo.

Lakini katika kuhakikisha miundombinu ya shule hizo inarejea katika hali yake ya awali mapema zaidi, mawaziri watatu wameungana na kamati ya maafa kuhakikisha wanafunzi wanarejea na kuendelea na masomo yao.

Mawaziri hao ni wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako; Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene; na Jenista Mhagama (Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu).

Akizungumza na waandishi wa habari katika Shule ya Sekondari ya Ihungo, iliyoharibiwa kabisa na tetemeko la ardhi, Mhagama alisema serikali imeanza kuchukua hatua za kubomoa na kusafisha majengo yaliyoharibiwa ili ujenzi uanze na kuwezesha wanafunzi turudi kuendelea na masomo.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Brigedia Jenerali Mbazi Msuya, alisema serikali imeanza kuchukua hatua ya kurejesha miundombinu huku ikiendelea kutoa misaada ya maafa.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Kagera kuanza kurejesha miundombinu yao kama serikali ilivyoanza kufanya.

Katika kurejesha miundombinu iliyoharibiwa na tetemeko la ardhi,
Kamati ya Maafa ya mkoa imezipa kipaumbele shule za Ihungo na Nyakato kwa sababu ziliharibiwa sana na kusababisha kufungwa, baada ya kuonekana kuwa majengo yake hayafai kutumika.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali (mstaafu) Salum Kijuu, alisema majengo yote ya umma na serikali, zikiwamo zahanati, hospitali na magereza, yatarejeshwa kwa utaratibu kulingana na upatikanaji wa fedha na vifaa ili kurudisha hali iliyokuwapo awali.

Tetemeko la ardhi lilitokea mkoani Kagera Septemba 10, mwaka huu na kusababisha vifo vya wananchi 17, majeruhi 440 na hadi sasa wamebakia majeruhi 17 ambao wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa mjini Bukoba.

Pia tetemeko hilo lilisababisha nyumba 2,072 kuanguka, nyumba zenye uharibifu hatarishi 14,595 na nyumba zenye uharibifu mdogo 9,471. Jumla ya nyumba zilizoanguka na zilizopata uharibifu hatarishi ni 16,667.
Aidha, wananchi walioathirika na kuhitaji misaada ili kurudi katika mfumo wa kawaida wa maisha yao ni 126,315.

Habari Kubwa